Dar es Salaam. Watu 112,952 wameitwa kwenye usaili wa mchujo wa kuandika (Written Interview), baada ya kukidhi vigezo vya maombi ya ajira katika nafasi 1596 zilizotangazwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania( TRA).
Februari 6, 2025, TRA ilitangaza nafasi za ajira 1596 katika fani mbalimbali, ambapo watu 135,027 waliomba nafasi hizo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo jioni, Machi 21, 2025, kuhusiana na mchakato wa kuwapata waombaji hao, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali Watu na Utawala kutoka TRA, Moshi Kabengwe, amesema TRA ilipitia kwa umakini maombi ya kazi 135,027 na kupata maombi 112,952 ambao ndio wenye vigezo vya kuitwa kwenye usaili.
Amesema majina ya watu hao waliokidhi vigezo hivyo, yatatangazwa kesho Machi 22, 2025 katika tovuti ya Mamlaka hiyo ya mapato.
“TRA imepitia kwa umakini mkubwa maombi yote 135,027 yaliyopokelewa na kupata waomba kazi 112,952 ambao wamekidhi vigezo vilivyowekwa na hivyo wanastahili kuitwa kwenye usaili wa mchujo wa kuandika( Written Interview) unaotarajia kufanyika Machi 29 na Machi 30, 2025 katika kanda tisa zilizoanishwa na TRA,” amesema Kabengwe na kuongeza.
“Mbali na majina kuwekwa kwenye tovuti ya TRA, pia taarifa itatumwa moja kwa moja kwa kila muombaji kupitia barua pepe yake aliyotumia wakati wa kuomba kazi, vilevile tarehe, mahali na muda wa usaili zimeonyeshwa kwenye wito huo” amefafanua.
Amesema mwitikio wa watu kuomba nafasi za kazi umekuwa mkubwa, kwani TRA ilitangaza nafasi za kazi 1,596, lakini hadi Februari 19, 2025 walipokamilisha siku ya mwisho ya kupokea maombi walioomba walikuwa ni 135,027.
Kabengwe amebainisha kuwa usaili wa mchujo huo utafanyika katika mikoa tisa, ambapo Dar es Salaam itahusisha waombaji kutoka Dar es Salaam na Pwani.

Mkurugenzi wa Usimamizi wa Rasilimali watu na Utawala kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania( TRA) Moshi Kabengwe, akizungumza na waandishi wa habari ( hawapo pichani) wakati akitangaza idadi ya watu walioitwa kwenye usaili wa mchujo wa awali, baada ya kukidhi vigezo vya maombi ya kazi yaliyotangazwa na Mamlaka hiyo. Picha na Hadija Jumanne
“Kituo cha usaili cha Zanzibar itahusisha waombaji kutoka Unguja na Pemba, wakati kituo cha usaili cha Dodoma itahusisha waombaji kutoka mikoa ya Morogoro, Dodoma, Singida, Iringa na Tabora” amesema.
Amesema kwa upande wa kaskazini, kituo cha usaili kutakuwa Arusha, ambapo kitahusisha waombaji kutoka mkoa wa Manyara, Kilimanjaro, Arusha yenyewe na Tanga.
Kwa upande wa mikoa ya Kusini, eneo la usajili litakuwa Mtwara ambapo itahusisha waombaji kutoka Lindi, Mtwara na Ruvuma.
“Pia Mwanza itakuwa ni kituo cha usaili kwa waombaji kutoka mikoa ya Shinyanga, Mara, Mwanza na Simiyu,” amesema.
Vilevile kwa upande wa Nyanda za Juu Kusini, kituo cha usaili kitakuwa Mbeya ambapo kitahusisha waombaji kutoka Songwe, Mbeya na Rukwa.
Vilevile kituo cha usaili cha Kigoma, kitahusisha waombaji kutoka mkoa wa Katavi na Kigoma yenyewe wakati kwa kituo cha usaili cha Kagera kitahusisha waombaji kutoka Geita na Kagera yenyewe.
“Utaratibu maalum umeandaliwa kwa waombaji kazi wenye mahitaji maalum waliofanikiwa kuitwa kwenye usaili wa mchujo wa kuandika ili waweze kufanya usaili huo bila usumbufu” amesema.
Kabengwe alifafanua kuwa mchakato huo wa ajira utaendeshwa na Mshauri mtaalamu na Mamlaka itasimamia kwa karibu ili kuhakikisha haki inatendeka kwa waombaji wote.
“Waombaji watakao faulu kwenye usaili wa mchujo wa kuandika wataitwa kwenye usaili wa mahojiano kwa tarehe itakayopangwa” amesema.
Vilevile, ameitaka jamii pamoja na waombaji wa nafasi hizo za kazi kuepuka utapeli unaoweza kufanywa na watu ambao sio waaminifu na kwamba TRA itaweka namba maalumu kwa ajili ya mawasiliano baina ya waombaji ili kuepuka utapeli.