Warsha ya Usalama wa Anga Afrika Yafungwa Jijini Dar es Salaam

 Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Bw. Salim Msangi, ameifunga rasmi warsha ya kikanda kuhusu usalama wa anga iliyoshirikisha washiriki 72 kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika. Warsha hiyo ya siku tano, iliyoanza Machi 17 na kuhitimishwa Machi 21, 2025, jijini Dar es Salaam, ililenga kujadili na kuimarisha mikakati ya kuboresha usalama wa anga, ufanisi wa usambazaji, na uendelevu wa sekta hiyo kwa kuzingatia teknolojia ya kisasa na miongozo ya kimataifa.

Akizungumza wakati wa kufunga warsha hiyo, Bw. Msangi alisisitiza kuwa mjadala wa washiriki umewezesha kutambua changamoto zinazoikabili sekta ya usafiri wa anga barani Afrika na njia bora za kuzitatua.

“Katika warsha hii, washiriki wamejadili changamoto zinazozikabili nchi zao na taasisi zao za usafiri wa anga, hususan kuhusu mifumo ya mawasiliano ya usafiri wa anga. Kupitia majadiliano haya, tumepata fursa ya kujadili namna bora ya kushughulikia changamoto hizi kwa pamoja, kwa sababu hakuna nchi inayoweza kufanya kazi peke yake,” alisema Msangi.

Aliongeza kuwa washiriki wa warsha wameahidi kushirikiana kwa karibu ili kuhakikisha sekta ya anga inakuwa salama na yenye ufanisi zaidi.

“Mimi kama Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, nina hakika kwamba kwa kushirikiana na wenzetu wa Afrika, Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (ICAO), na Shirika la Usalama wa Anga la Jumuiya ya Afrika Mashariki (CASSOA), tutaendelea kuboresha usalama wa anga na kuhakikisha kuwa anga letu ni salama kwa abiria na ndege zote zinazopita katika anga la Tanzania na Afrika kwa ujumla,” alisisitiza.

Kwa upande wake, mshiriki wa warsha hiyo kutoka Kenya, Bw. Ruben Kyema, alisema kuwa majadiliano yaliyofanyika yamekuwa ya manufaa makubwa kwao, kwani yamewasaidia kutambua changamoto na kuzitafutia ufumbuzi kwa mustakabali wa sekta ya anga barani Afrika.

Warsha hii ni sehemu ya juhudi za kikanda katika kuhakikisha sekta ya usafiri wa anga inakuwa salama, yenye ufanisi, na inazidi kuimarika kwa mujibu wa viwango vya kimataifa.

Related Posts