Watanzania saba kati ya kumi, sawa na asilimia 68, wanaridhishwa na jitihada za Serikali katika utoaji wa huduma za afya hata hivyo wametaka nguvu kubwa iongezwe katika uboreshaji wa huduma hizo.
Hiyo ni kulingana na utafiti wa Afrobarometer kuhusu Afya ya Jamii nchini Tanzania uliofanyika mwaka 2024 na matokeo yake kutolewa Machi mwaka huu.
Akizungumza wakati wa uwasilishaji matokeo ya utafiti huo utafiti huo Mkurugenzi wa Utafiti na Mafunzo wa Repoa, Dk Lucus Katera amesema asilimia 40 ya Watanzania waliripoti kukosa dawa au matibabu angalau mara moja katika mwaka uliopita.
Amesema katika utafiti huo ulilenga kuangalia jinsi huduma za afya zilivyoboreshwa asilimia 17 ya wahojiwa wamesema wanakosa huduma ya matibabu mara moja au zaidi ya mara moja.
Utafiti huo unaonesha pia bado kuna baadhi ya maeneo huduma za afya ziko mbali ambapo asilimia 30 ya wahojiwa hasa wa maeneo ya vijijini wameeleza hivyo.
“Serikali imewekeza kwa kiasi kikubwa katika maeneo mengi, kama vile vifaa vya matibabu na dawa, hivyo tukaangalia kama watu wanaridhishwa na huduma za afya zinazotolewa.
“Tumeona katika ripoti hiyo kwamba, pamoja na changamoto kama vile upungufu wa watumishi wa afya na masuala mengine, Watanzania bado wanaridhishwa na jinsi serikali inavyotoa huduma za afya,” amesema Dk Katera na kuongeza.
“Hata hivyo unapokuwa umejenga kituo cha afya au zahanati katika kona fulani inawezekana kwa wengine kuifikia ikawa mbali,”.
Katika hilo Dk Katera ameshauri Serikali na wadau wengine waangalia namna ambavyo wanaweza kusaidia huduma za afya kuwafikia watu kwa njia rahisi ikiwemo kliniki zinazotembea.
Amesema, “Inawezekana hizi kliniki zinazotembea zipo ila hazipo kwa kiasi cha kutosheleza, uwekezaji zaidi ungefanyika kwenye eneo hili ili kufikisha huduma maeneo ya pembezoni,”.
Ripoti hiyo pia imebainisha kuwa wananchi wawili kati ya watatu sawa na asilimia 34 kwa kiasi fulani na asilimia 32 wana wasiwasi wa kutoweza kumudu huduma za afya ikiwa wao au wanafamilia wataugua.
Akizungumzia ripoti hiyo, Dk Eva Matiko wa taasisi ya Tanzania Health Promotion Support (THPS) ameeleza kuwa majibu ya Watanzania yanatia moyo kwa sababu asilimia kubwa ya watu wameridhika, hali inayoonyesha kuwa serikali inatekeleza wajibu wake vizuri.
Hata hivyo, alibainisha kuwa bado kuna maeneo machache ambayo wananchi wametoa kero, kama vile kutotosha kwa watoa huduma.
“Sisi kama wadau tutashirikiana zaidi na Serikali katika kuboresha maeneo yote yaliyotajwa, matokeo haya yanatupa moyo kuendelea kufanya kazi zaidi.
“Tunakubaliana na uelekeo wa Serikali wa kwenda kwenye bima ya afya kwa wote, suala la gharama za matibabu halijalishi kipato cha mtu kila aliyehojiwa analalamika kuhusu gharama na ndiyo tunaona umuhimu wa bima ya afya kwa wote,” amesema Dk Eva.
Akizungumzia matokeo hayo, Hellen Sule mkazi wa Temeke, amesema yana uhalisia kwa kiasi kikubwa kwa sababu upatikanaji wa huduma za afya kwa sasa umeongezeka ikilinganishwa na ilivyokuwa hapo awali.
“Huduma ni kweli zinapatikana tena siku hizi hadi zile ambazo tulikuwa tunalazimika kuzifuata Muhimbili tunazipata hospitali za huku chini ikiwemo hii Temeke, hili jambo linatupa ahueni watu wa kawaida.
“Hata hivyo nikiri kuwa suala la gharama bado linatusumbua wengi, ni kweli tumeletewa huduma lakini kuna wakati mtu anakufa kwa sababu hana uwezo wa kugharamia matibabu,” amesema Hellen.
Kwa upande wake Jeremia Maganja mkazi wa Mbozi mkoani Songwe amesema bado kuna changamoto ya watoa huduma hali inayosababisha kutumia muda mrefu kwenye kusubiri matibabu.
“Mtu unakwenda zahanati unakaa zaidi ya masaa matatu, daktari ni mmoja sasa ukifikiria ugonjwa wenyewe ni homa unaona bora ukameze Panadol usipoteze muda kusubiri huduma. Kwa hiyo ombi langu watoa huduma waongezwe ili tufaidi hizo huduma za afya,” amesema.