Unguja. Wakati yakifanyika mashindano ya kuhifadhi Quran kwa Afrika, Mohamed Amejair (23) kutoka Afrika Kusini ameibuka kidedea na kujinyakulia kitita cha Sh30 milioni, huku Rais Hussein Mwinyi akisema yanaitangaza Zanzibar kimataifa.
Mashindano hayo yamefanyika leo Machi 22, 2025 katika Uwanja wa Aman Complex, Unguja mgeni rasmi akiwa Dk Mwinyi. Yamewashirikisha vijana 10 waliohifadhi Quran juzuu 30.
Katika mashindano hayo, mshindi wa pili Omar Belo kutoka Nigeria amepata cheti na Sh20 milioni, huku mshindi wa tatu ni kijana kutoka Algeria, Abdulrahman Mosi ambaye amepata Sh10 milioni.
Washindi wengine ni Hassan Is-haka kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), aliyepata Sh5 milioni.
Kwa upande wao, Rashid Masoud (Tanzania), Mahamoud Abdul (Senegal), Hija Nassor Hija (Zanzibar), Masnur Haji (Nigeria), Abdurahim Abdurahim (Comoro) na Muhamed Said (Kenya) kila mmoja amepata cheti na Sh3 milioni.
Rais Mwinyi amewapongeza vijana hao kwa juhudi zao binafsi katika kuendeleza elimu hiyo, akisema hatua hiyo inaendeleza mshikamano na umoja miongoni mwa mataifa ya Afrika.
“Hili ni jambo la kupongeza, kuwa na mashindano haya katika nchi zetu si tu kukuza elimu na maadili lakini pia tunaongeza mshikamano na kuleta umoja miongoni mwa mataifa yetu,” amesema.
Amesema kufanyika mashindano hayo Zanzibar ni fursa ya kujitangaza kimataifa, akitumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi waliojitokeza kushiriki.
“Kwa kweli mwitikio wenu ni fursa ya kujitangaza kimataifa kwamba nchi yetu ina amani, umoja na mshikamano. Tunaomba Mwenyezi Mungu azidishe hili,” amesema.
Ameipongeza ofisi ya Mufti Mkuu kwa kuendelea kuwajengea uwezo vijana.
Rais Mwinyi amesema mashindano hayo yanazidi kuwa tukio kubwa na muhimu linalowaleta washiriki pamoja nchini kutoka mataifa mbalimbali na kuitangaza Zanzibar.
“Hii ni hatua muhimu inakwenda sambamba na dhamira ya Serikali ya kuimarisha utalii ya kubuni matukio mbalimbali na matamasha ambayo yatawavutia washiriki wengi kutoka ndani na nje ya nchi kama tunavyoshuhudia kupitia mashindano haya,” amesema.
Amewapongeza walimu wanaowakuza vijana hao katika maadili na tabia njema, akieleza katika kuwasomesha wanafanya hivyo wakitegema ujira na malipo yao kutoka kwa Mwenyezi Mungu.
Amewataka kuendela kufanya ibada wapate fadhila nyingi ili kila mmoja apate kinachotakiwa.
Kuhusu waandaaji amewataka kuyakuza mashindano hayo ambayo yametoka ya Afrika Mashariki sasa yamekuwa ya Afrika, hivyo wanatakiwa yafikie hatua ya kimataifa.
“Tulifanya ya Afrika Mashariki yakafana, leo tumefanya ya Afrika yamefana sioni sababu kwa nini na sisi sasa tusifanye ya kimataifa ya mabara yote, kama ni mahudhurio uwanja umejaa na watu wapo wengi,” amesema.
Amesema wana uwezo wa kujaza uwanja kwa hiyo walitazame suala hilo na kufanya mashindano hayo yawe makubwa zaidi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Haroun Suleiman Ali amesema hali imeendelea kuimarika na usalama, hivyo waendelee kufanya hilo hadi kufikia mwakani yatakapofanyika mashindano mengine.
Katibu Mtendaji wa Ofisi ya Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume amesema jambo hilo wengi wamelifahamu na kuhamasika kushiriki kuhifadhi Quran.
Amewataka wananchi kushirikiana kuendeleza jambo hilo kila mwaka
Wakati huohuo, washindi wa mashindano ya kuhifadhi Quran kwa watu wazima, wamepatiwa fursa ya kwenda Macca kushiriki ibada ya hija.
Wakizungumza baada ya kuibuka na ushindi Machi 20, 2025 washindi hao wawili wenye umri zaidi ya miaka 50, Sheikh Abdalla Hamad na Kibunya Makame Ahmed walieleza hawakutarajia wangekwenda hija.
“Tunashukuru, kwenye jamii kuna watu hawana uwezo lakini wanatamani wafike katika ibada tukufu isiwe tu kwenye ndoto, kwa hiyo kupitia mashindano haya ni utaratibu ambao utawezesha wengi kufika kupitia uwezo wao,” amesema Abdalla (57) mkazi wa Kidimni Mkoa wa Kusini Unguja aliyeibuka mshindi wa kwanza kwa upande wa wanaume.
Kwa upande wa wanawake aliyeshinda ni Kibunya Makame Ahmed (55), mkazi wa Kitope Kaskazini Unguja, aliyesema alipopata taarifa za mashindano hayo alijitosa lakini hakujua kama angeweza kupenya.
“Sikutarajia hata kufika Pemba lakini Mwenyezi Mungu alivyokuwa mkarimu nimefika na ninajisikia faraja sana kwenda hija maana nimetamani sana miaka mingi lakini sikuwa na uwezo,” amesema.
Mwenyekiti wa Kidundo Haji Umrat Travel Agency, Khalid Iddi Haji walioandaa mashindano hayo amesema lengo ni kuwapa nafasi watu wazima kushiriki ibada hiyo, ambayo watagharimia kila kitu kuazia safari ya kwenda na kurudi na siku zote watakazokaa Macca.
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Ayoub Mohamed Mahmoud amesema jambo hilo ni jipya katika eneo hilo lakini kwa sababu ya ubunifu umesaidia kuleta mawazo mapya.