CCM yaahidi ilani itakayotatua changamoto za ajira kwa vijana

Bukoba. Katika kukabiliana na uhaba wa ajira Tanzania, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) -Bara, Stephen Wasira amesema chama hicho kitakuja na ilani bunifu kwenye uchaguzi mkuu 2025 ili kuongeza kasi ya mapato kwa wananchi wote ikiwemo vijana kufanikiwa kiuchumi.

Amesema ilani hiyo itasaidia kukabiliana na changamoto ya uchache wa ajira na lawama kubwa zinazotolewa kwa Serikali inayoundwa chama hicho kutoka kwa vijana wanaohitimu vyuo mbalimbali nchini na nje ya nchi.

Wasira anatoa kauli hiyo katika kipindi ambacho baadhi ya makundi yameanza kujitokeza hadharani ikiwemo walimu wasio na ajira nchini, kufanya mikutano na vyombo vya habari kuishinikiza Serikali kuwapa ajira.

Akizungumza leo Machi 22, 2025 kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Viwanja vya Kemondo, Tarafa ya Katerero Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, Wasira amesema kilio cha ajira wanakisia lakini Watanzania na vijana wanapaswa kufahamu chama hicho kimefanya makubwa na maendeleo yanavyokuja yanakuwa na changamoto zake.

Amesema pamoja na changamoto mpya kama kuwa na wasomi wengi, chama hicho ni lazima kije na mkakati wa kuwalinda hasa vijana kutokana na umuhimu wao.

“Tumeshakubalina tutakuja na ilani bunifu katika uchaguzi mkuu wa 2025 itakayotoa upendeleo maalumu kwa vijana, kuja kuongeza kasi ya mapato kwa vijana ili waweze kufanikiwa kiuchumi,” amesema.

Wasira amesema hawawezi kulitenga kundi hilo kwa kuwa ni kubwa na lina ushawishi mkubwa, hivyo wanalitegemea katika kuleta mageuzi ya kiuchumi Tanzania.

“Katika kamati ya kutengeneza ilani, mimi mwenyewe ni mjumbe, ninachosema nina uhakika nacho, lazima tuje na ilani bunifu kukabiliana na tatizo la ajira, vijana wanahitaji kumiliki uchumi,” amesema nakuongeza:

“Tumekubaliana lazima vijana wapewe nafasi maalumu kama wanafanya kazi ya uvuvi, lazima wafanye shughuli hiyo kisasa, lazima tuwasaidie zana za kazi za kisasa,” amesema.

Wasira amesema kulingana na mazingira ya sasa, wamefanya tathmini na kutambua vijana hawahitaji fedha za kusubiria kwa muda mrefu na badala yake wanataka fedha za haraka haraka.

“Ndiyo ujana huo wala huwezi kuwalaumu kwa sababu tumewasomesha halafu tumewapa simu za kupangusa na kidole, dunia nzima iko kiganjani mwao na wanafuatilia yanayojiri duniani,” amesema.

Amesema chama hicho kimetafakari kuna miradi wakileta itakuja kunufaisha vijana ikiwemo kufanya uvuvi wa kisasa kwa kuwapatia vifaa vinavyokidhi mahitaji hayo.

“Kama unafanya kilimo, basi tunaangalia mazao ya muda mfupi, wanalima na kuvuna kama bustani za nyanya wanalima na kuvuna wanauza na kununua vocha, maana vijana wapo tayari kulala njaa ili mradi tu wapate vocha,” amesema.

Katika hatua nyingine, mbunge wa Bukoba Vijijini, Jasson Rwekiza amesema katika kipindi cha miaka minne Serikali imefanya vizuri hasa kwenye sekta ya maji, walipokea fedha ya utekelezwaji miradi 38 ikiwemo Lukindo, Katare na Lubale.

“Miradi mingi imekamilika na baadhi imeanza kufanya kazi, maeneo mengi yataanza kunufaika na huduma ya maji safi na salama, jumla ya miradi yote ni zaidi ya Sh25 bilioni,” amesema.

Katika sekta ya elimu, Sh29.6 bilioni wamejenga madarasa 194, matundu ya vyoo 195 na shule zingine ili kuwarahisishia wanafunzi kusoma mazingira mazuri na rafiki huku katika sekta ya afya Serikali ikiwapa zaidi ya Sh3 bilioni.

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Richard Kasesela amesema dhambi kubwa inayowatafuna wanaCCM pale tunapopata madaraka ni kiburi na kujisahau kwa sababu ya madaraka.

“Jambo lingine tamaa, ulafi, jamani madaraka anatoa Mungu, waacheni nao wagombee ili ukishinda nawe ushinde kwa haki bila nongwa,” amesema.

Awali, mjumbe wa halmashauri kuu Taifa kutoka Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselela amesema kutokana na utekelezwaji wa ilani katika kuleta maendeleo, anaamini uchaguzi ujao wanaenda kushinda kwa kishindo.

“Kazi iliyobaki ni wanaCCM kuwa pamoja kushirikiana na kuzungumza lugha moja kukabiliana na vyama vya upinzani,” amesema.

Related Posts