Dar es Salaam. Wakati uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura mkoani Dar es Salaam ukihitimishwa kesho Machi 23, 2025, baadhi ya wananchi wameibua changamoto za kusibiri muda mrefu vituoni, baadhi wakilazimika kwenda alfajiri kupanga foleni ili kujiandikisha.
Pia, wametoa wito kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kuongeza mashine zinazotumika kwenye uandikishaji (BVR) pia siku za uandikishaji ziongezwe.
Uandikishaji mkoani hapa ulianza Machi 17, 2025.

Baadhi ya wananchi wa Tabata kisiwani wakitaka kuingia ndani ya kituo cha kujiandikishia baada ya kulalamika kukaa muda mrefu kituoni hapo. Picha na Baraka Loshilaa
Ummy Boniface, mkazi wa Mtaa wa Zingiziwa, Kata ya Zingiziwa akizungumza na Mwananchi leo Machi 22, 2025 amesema wanatumia muda mrefu vituoni kutokana na wingi wa watu, hivyo ameshauri BVR ziongezwe.
Khalid Abbas, mkazi wa Mtaa wa Lubakaya, Kata ya Chanika ameomba muda wa uandikishaji uongezwe.
“Serikali itumie busara kuongeza siku kwa kuwa Dar es Salaam ina wakazi wengi ukilinganisha na mikoa mingine, watu wengi nafasi zao huwa mwisho wa juma,” amesema.
Ofisa Mwandikishaji Jimbo la Kibamba na Ubungo, Lawi Bernard amesema uandikishaji unakwenda vizuri akiamini watafikia lengo. Amesema wapigakura wapya wenye miaka 18 wanaotarajia kuandikisha ni 114,973.
Akizungumzia changamoto ya foleni kubwa vituoni, amesema zinatokana na sababu kadhaa ikiwemo baadhi ya watu kutokuwa na taarifa sahihi za nani anapaswa kwenda kuboresha taarifa zake.

Wananchi katika Mtaa wa Zingiziwa, Kata ya Zingiziwa wakiwa katika kituo cha kujiandikisha ofisi za serikali wa mtaa huo. Picha na Nasra Abdallah
“Utakuta mtu kadi yake ya kupigia kura haina tatizo lolote, wala hajahama eneo lake alilojiandikisha (kata) lakini kashakaa kwenye foleni muda mrefu na kuzuia wale wanaotakiwa kufanya hivyo,” amesema.
Amesema katika baadhi ya maeneo walilazimika kuongeza BVR ili kutatua changamoto hiyo.
Bernard amesema wapo baadhi ya watu kadi zao hazi matatizo lakini wanataka mpya.
Ili kupunguza muda wa kukaa kwenye foleni ameshauri kuboresha taarifa kupitia mfumo wa mtandao kazi inayoweza kufanyika kwa kutumia simu na kwenda kituoni kukamilisha taratibu kwa muda mfupi.
Katika eneo la Tabata Kisiwani, Pamela James amesema tangu jana (Machi 21) anahangaika kujiandikisha lakini wingi wa watu umekuwa kikwazo.
“Tunaambiwa mashine ni moja siku ya pili leo nakuja na bado idadi ya watu ni kubwa, ikiwezekana tunaomba siku ziongezwe kwa sababu tunaambiwa kesho (Machi 23) ndiyo mwisho maana yake nisipojiandikisha leo uwezekano wa kujiandikisha tena haupo,” amesema.
Sebastian Julius, mkazi wa Tabata Kisiwani amesema muda uliowekwa wa uandikishaji wapigakura ni mdogo na idadi ya watu iliyojitokeza ni kubwa, pia hakuna utaratibu mzuri wa watu kuandikishwa.
Katika Mtaa wa King’ong’o, Kata ya Saranga, licha ya watu wengi kujitokeza kwa kiasi kikubwa wakiwa vijana, watu wenye mahitaji maalumu, wajawazito na wenye watoto wachanga walipewa kipaumbele.
Amina Shabani mkazi wa eneo hilo anasema amejitokeza kujiandikisha ili aweze kutumia haki yake ya kikatiba kumchagua kiongozi anaemtaka.
Sheila Abdul, amesema alifika kituoni saa 12:30 asubuhi ili kuwahi kujiandikisha.
INEC inatarajia kuandikisha wapigakura wapya 643,420 mkoani Dar es Salaam ambako vituo 1,757 vinatumika kwenye uboreshaji mwaka huu ikiwa ni ongezeko la vituo 96 kulinganisha na 1,661 vilivyotumika kwenye uboreshaji mwaka 2019/20.
Katika kuhakikisha wote wenye sifa za kuandikishwa wanaandikishwa Tume imelisema inatumia BVR zaidi ya 5,000 ikieleza ina watendaji wa kutosha kwa ajili ya kazi hiyo.
Tayari Tume imekamilisha uboreshaji wa daftari katika mikoa 29.
Kwa mujibu wa Tume wapigakura wapya wanaotarajiwa kuandikisha (643,420) ni sawa na ongezeko la asilimia 18.7 ya wapigakura 3,427,917 waliopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura.