Dodoma. Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (Cosota) imesema imepokea jumla ya migogoro 136 inayohusiana na masuala ya hakimiliki ambapo migogoro 118 imefanyiwa kazi na kumalizika, migogoro 10 imefikishwa mahakamani huku migogoro minane ikiwa kwenye hatua mbalimbali za utatuzi.
Ofisi hiyo imeshiriki kutoa ushahidi kwenye migogoro 10 inayohusu hakimiliki ambayo inaendelea mahakamani mpaka sasa.
Hayo yamebainishwa Ijumaa Machi 21, 2025 na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Cosota, Doreen Sinare wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya ofisi yake kwa kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita jijini Dodoma.
Sinare amesema migogoro hiyo ni ongezeko kubwa kuwahi kutokea kwani kwa kipindi cha nyuma walikuwa wanapokea migogoro minne kwa mwaka jambo ambalo linaonyesha kuwa wasanii wa kazi za sanaa wamepata elimu kuhusu hakimiliki ya kazi zao.
Amesema asilimia kubwa ya malalamiko hayo ni kutoka kwa wasanii wa muziki pamoja na waigizaji huku sanaa nyingine migogoro yao ikiwa kwa kiasi kidogo.
Amesema kutokana na mabadiliko ya Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki namba 7 ya mwaka 1999 yaliyofanyika mwaka 2022 na 2023 kupitia sheria za fedha za mwaka 2022 na 2023 yalianzisha chanzo kipya cha mapato cha tozo ya hakimiliki.
Ameongeza kuwa vifaa vinavyotumika kusambaza, kuzalisha na kuhifadhi kazi za sanaa na fasihi hutozwa asilimia 1.5 kila vinapoingia, kuzalishwa au kuundwa hapa nchini.
“Lengo kuu la kuanzishwa kwa tozo hiyo ni kuwajengea uwezo wa kiuchumi wadau wa sanaa na uandishi nchini wakiwemo wasanii, waandishi na wabunifu ambao kwa muda mrefu kazi zao zimekuwa zikitumika katika mazingira ya kijamii kama vile kuhifadhi, kubebea na kusambaza kazi sanaa na uandishi na kuwanufaisha wadau wengine pamoja na watu binafsi bila ya wenye kazi kupata haki zao,” amesema Sinare na kuongeza:
“Kupitia chanzo hiki, Cosota imekusanya jumla ya Sh1.4 bilioni kuanzia Septemba 2023 hadi Februari 2025 ambapo ofisi imefanikiwa kupokea fedha za tozo ya hakimiliki za mwaka wa fedha 2023/2024 kutoka Wizara ya Fedha, Sh847.9 milioni.”
Amesema kiasi cha Sh508.7 milioni kitagawiwa kwa wasanii ambacho ni asilimia 60 ya tozo ya hakimiliki na kiasi cha Sh84.7 milioni sawa na asilimia 10 kinaenda mfuko wa sanaa na utamaduni ambapo fedha hizo pia ni kwa ajili ya wasanii.
Hivyo wasanii na waandishi watanufaika na jumla ya kiasi cha Sh593.5 milioni zilizokusanywa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024, gawio la serikali ni Sh142.8 milioni na gharama ya uendeshaji Cosota ni Sh285.6 milioni.
“Ofisi imeandaa mgawo wa mapato haya kama mirabaha kutokana na fedha za tozo ya hakimiliki utakaofanyika hivi karibuni. Mgawo huu unategemewa kunufaisha makundi ya kazi za muziki, filamu, maandishi, sanaa za ufundi na sanaa za maonyesho. Kila daraja litapata kiwango sawa na madaraja mengine,” amesema Sinare.
Katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, usajili wa kazi zinazolindwa na Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki umeongezeka kwa asilimia 70 ukilinganisha na miaka ya nyuma ambapo kuanzia mwaka 2021 hadi Februari 2025, Cosota imesajili kazi za sanaa na uandishi 11,519 na wabunifu 3,436.
Amesema idadi hii ya wabunifu pamoja na kazi zao imetokana na utoaji wa elimu na mafunzo ya hakimiliki na usajili kupitia vyombo vya habari, mitandao ya kijamii, semina, pia, kushiriki matukio mbalimbali ya wadau ambapo Cosota ilipata fursa ya kuelimisha wadau kuhusiana na hakimiliki na uhamasishaji wa usajili wa kazi za hakimiliki.
Katika kipindi hicho, kamati maalumu ya usajili ndani ya Cosota inayojihusisha na masuala ya usajili, imefanikiwa kutoa mafunzo na ufafanuzi kuhusiana na hakimiliki kwenye kazi zilizopokelewa katika kipindi hicho kwa idadi ya wabunifu 167.
Vilevile, katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita, Cosota imetoa jumla ya vyeti 7,679 vya uthibitisho wa umiliki wa hakimiliki kwa wabunifu waliosajili kazi zao.
Kwa mwaka 2021 – 2025, Cosota imefanikiwa kufanya migawo miwili kama alivyoahidi Rais Samia alipolihutubia Bunge mwaka 2021 ambapo alisisitiza katika kipindi cha uongozi wake, Serikali itahakikisha wabunifu wote wananufaika na kazi zao.
Mgawo wa kwanza ambao ulikuwa wa ishirini na tatu ulifanyika Januari 28, 2022 na ulikuwa Sh312.2 milioni ambapo wasanii 1,123 walinufaika, na ulitokana na matumizi ya kazi 5,924 za muziki ambazo zilitumika katika vituo 11 vya redio, ikiwemo redio katika ngazi ya kitaifa, mkoa, wilaya, kijamii na za kidini.
Mgawo wa pili ulifanyika Julai 21, 2023 na ulikuwa ni mgawo wa 24 wa mirabaha kwa kazi za muziki na Cosota iligawa Sh396.9 milioni ambapo wasanii wa muziki 8,165 walinufaika kupitia kazi zao 61,490.
“Hivi ni viwango vikubwa zaidi kuwahi kufanyika katika migao ya mirabaha ambayo Cosota imekuwa ikigawa kwa miaka ya nyuma kabla ya uongozi huu wa serikali ya awamu ya sita ambao ulianzisha kampeni ya kusisitiza watumiaji wa kazi za sanaa katika maeneo ya biashara kulipia matumizi ya kazi hizo,” amesema.