Morogoro. Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linamshikilia dereva wa lori la mafuta la kampuni ya Meru, Abubakar Mwichangwe anayetuhumiwa kula njama na kuiba mafuta aliyokuwa akisafirisha kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Lubumbashi, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kisha kuchoma moto gari hilo kwa lengo la kupoteza ushahidi.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama dereva huyo alikamatwa Machi 18, 2025, hata hivyo kutokana na sababu za kiuchunguzi, hakueleza zaidi mazingira na namna dereva huyo alivyokamatwa.
Mkama amesema baada ya kukamatwa kwa dereva huyo, idadi ya watu waliokamatwa kwa tuhuma za wizi huo imefikia wanne baada ya awali mameneja watatu wa vituo vya mafuta vya Simba Oil kushikiliwa wakihusishwa na njama hizo.
“Hawa mameneja wa Simba Oil wanatuhumiwa kuhusika kwenye wizi huu wa mafuta kwa sababu huyu dereva alikwenda kuyamimina kwenye vituo vya Simba Oil eneo la Mkambarani na katikati ya mji wa Morogoro,” amesema Kamanda Mkama.
Amewataja mameneja wanaotuhumiwa na wizi huo kuwa ni Hamidu Sudi (50), mkazi wa Dar es Salaam, Abiner Shalon (25), mkazi wa Morogoro na Abdalah Nihed (30), mkazi wa Morogoro.
Amesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea kwa kushirikiana na mamlaka nyingine – Mamlaka ya Nishati na Maji (Ewura) na Mamlaka ya Mapato (TRA) na baada ya kukamilika kwa uchunguzi huo, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watuhumiwa hao.
Machi 17, 2025, Kamanda Mkama, aliieleza Mwananchi kuwa dereva huyo baada ya kuiba mafuta hayo aliendesha gari hilo hadi eneo la Msimba, Barabara ya Morogoro – Iringa na alipofika eneo hilo, aliangusha gari korongoni na kuliwasha moto akijaribu kuliteketeza kupoteza ushahidi.
Hata hivyo, kabla ya moto huo haujashika, walitokea wasamaria wema na kufanikiwa kuuzima kisha kutoa taarifa polisi.
Amesema mafuta wanayodaiwa kuibiwa na watuhumiwa hao ni aina ya dizeli, lita 35,700, yenye thamani ya Sh77.112 milioni.
Awali, mmoja wa wanafamilia wa wamiliki wa kampuni hiyo, Alif Mbaraka amesema vituo hivyo vimefungwa kwa wiki moja sasa, huku mameneja wake wakiendelea kushikiliwa.
Mbaraka amesema maofisa wa polisi pamoja na Ewura walifika na kufunga tepu nyekundu kuzunguka mashine za kutolea mafuta.
“Wakati wanafunga nilikuwa naswali, nilipomaliza kuswali, kushuka chini, nikakuta wanamalizia kufunga pampu na muda huo tayari meneja alikuwa amekamatwa, ilibidi niende polisi kufuatilia, ndipo niliwakuta mameneja wetu wawili wa hapa mjini na Mkambarani,” amesema Mbaraka.
Akizungumzia hasara waliyoipata, Mbaraka amesema ni kubwa kwa kuwa zipo kampuni za minara ya simu ambazo zinachukua mafuta kwenye vituo vya Simba Oil.
“Kuna kampuni za minara ya simu ambazo zinachukua mafuta hadi lita 2,000 kwa wiki kwa ajili ya kupeleka kwenye minara, wateja hao wote tumewapoteza kwa siku tatu hizi, lakini pia tukio hili limechafua kampuni yetu,” amesema M