Dk Nchimbi atuma salamu kwa wabadhilifu CCM

Dodoma. Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi ametuma ujumbe kwa wanachama wasio waadilifu ndani ya chama hicho, akisema wanaendelea kuwaandaa watu waadilifu kama Mwekahazina wa CCM, Dk Frank Hawassi.

Dk Nchimbi ameyasema hayo leo, Jumamosi Machi 22, 2023 kwenye ibada ya kumuaga mke wa Dk Hawassi, marehemu Damaris Hawassi, iliyofanyika katika Kanisa la Assemblies of God Tanzania (AGT), Miyuji jijini Dodoma.

Amesema kadri CCM inavyopata viongozi waadilifu kama Dk Hawassi, ndivyo nchi itakavyopata maendeleo kwa haraka.

“Kabla ya kikao cha Kamati Kuu kilichokutana hivi karibuni, nilimjulisha mwenyekiti wetu kuhusu maendeleo ya mgonjwa wetu (mke wa Dk Hawassi), na kuwa Hawassi ataendelea kukosekana ofisini kwa kuwa alikuwa akimhudumia mke wake kwa zaidi ya miezi sita,” almesema.

Kwa mujibu wa Dk Nchimbi, Mwenyekiti wa Taifa wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan alimtaka kuwasilisha suala hilo katika kikao cha Kamati Kuu, ambapo ilikubaliwa kuwa Dk Hawassi aendelee kumhudumia mke wake hadi apate nafuu kabla ya kurejea kazini.

Dk Nchimbi amesisitiza kuwa mchango wa Dk Hawassi ndani ya chama ni mkubwa kiasi kwamba hata anapokuwa hayupo kwa muda mrefu, hakuna anayejali muda huo, bali wanathamini mchango wake kwa chama na nchi.

“Watu ambao walizoea kuiba fedha za CCM bila utaratibu hawana raha na utendaji wa Hawassi. Tumempa kazi ya kutengeneza watu wa aina yake, na kazi inaendelea vizuri. Kwa hiyo, maumivu ndani ya CCM yataendelea kwa muda mrefu kwa sababu tunaandaa wengine wa kutosha,” amesema Dk Nchimbi.

Ameeleza kuwa mafanikio ya chama katika kudhibiti na kusimamia rasilimali zake yatasaidia pia katika usimamizi bora wa rasilimali za nchi kwa ujumla.

Makamu Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Abdulrahman Kinana, kwa niaba ya wastaafu wenzake, amesifu uadilifu wa Dk Hawassi na kuwataka wengine kumuiga.

“Unajua kuna sifa za usomi, kazi, lakini kuna sifa za tabia. Kama kuna binadamu mwenye mfano wa tabia njema basi ni Hawassi – muungwana, mtaratibu, mnyenyekevu na mchapakazi. Si kawaida kwa mtu ndani ya CCM kutofurahia kujulikana au kusifiwa, lakini yeye ndivyo alivyo,” amesema Kinana.

Amesema watu wengi wanapoulizwa kuhusu Mwekahazina wa CCM, hawamjui kwa sura, lakini kazi yake inaonekana na inazaa matunda.

Kwa upande wake, Kapteni Mstaafu John Chiligati, kwa niaba ya wadhamini wa CCM, amesema kuwa Dk Hawassi ndiye aliyeanzisha mfumo wa control number ili malipo ya chama yaingie kwa utaratibu huo.

“Tulimwambia kama mfumo wa control number unadhibiti uvujaji wa mali za CCM na kuongeza mapato ya chama, basi wazo hilo lina baraka zetu. Aendelee kuchapa kazi kuhakikisha hakuna ufujaji wa rasilimali za CCM,” amesema Chiligati.

Related Posts