Dar es Salaam. Watafiti wametahadharisha juu ya ongezeko la shinikizo la juu la damu kwa watoto wa shule za awali nchini, chanzo kikitajwa kuwa ni unene kupita kiasi.
Utafiti uliofanyika katika wilaya za Kinondoni na Ilala mkoani Dar es Salaam na kuchapishwa Machi 19, 2025 katika Jarida la Italian linaloangazia magonjwa kwa watoto, unaonyesha asilimia 23.3 ya watoto wa shule za awali waliohusika katika utafiti wana shinikizo la juu la damu.
Kiongozi wa utafiti huo uliofanywa na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (Muhas), Dk Jida Said amesema kati ya watoto 1,083 waliohusika katika utafiti huo, 252 walibainika kuwa na shinikizo la juu la damu.
Kwa mujibu wa utafiti huo, hali hiyo inasababishwa na mambo kadhaa, unene kupita kiasi na uzito mdogo wa kuzaliwa.
Akizungumza na Mwananchi kuhusu utafiti huo, Jida, daktari bingwa wa watoto katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), amesema uliwahusisha watoto wa miaka miwili mpaka mitano wanaosoma shule za awali, baada ya kuona tatizo hilo linaongezeka katika nchi zinazoendelea, ikiwamo Tanzania, na baadhi yao kufikishwa vituo vya afya kupata matibabu.
Dk Jida amesema matokeo ya utafiti huo uliofanyika mwaka 2020 na kuchapishwa Machi mwaka huu, yalionyesha asilimia 23.3 ya watoto walikuwa na kiwango cha juu cha shinikizo la damu.
Amesema kati ya watoto hao, asilimia 19.8 walikuwa katika hali hiyo lakini haijafikia ya juu kuliko kawaida, ila inaelekea kuwa shinikizo la juu la damu.
“Asilimia 3.5 hawa ndio walikuwa na ugonjwa wa shinikizo la damu la juu (hypertension) ambalo linatakiwa kufanyiwa matibabu, kiwango kinachohitaji uangalizi wa juu,” amesema.
Kwa mujibu wa Dk Jida, utafiti huo ni wa kwanza kufanyika Tanzania kuangalia tatizo la shinikizo la juu la damu kwa watoto wa umri wa miaka miwili mpaka mitano.
“Matokeo haya yanatufumbua macho na kuonyesha uhitaji wa tafiti kubwa zaidi eneo hili,” amesema.
Dk Jida amesema lengo la utafiti huo ilikuwa kutafuta sababu za shinikizo la damu kwa watoto na miongoni mwa visababishi walivyobaini ni uzito mkubwa kwa asilimia nne ya watoto waliohusika na utafiti na asilimia nne nyingine walikuwa na uzito mkubwa kupita kiasi.
Amesema makundi hayo mawili, wote waliongoza kwa kuwa na shinikizo la juu la damu, hivyo kubainika ni kihatarishi cha tatizo hilo.
Dk Jida ametaja kiashiria kingine ni watoto wanaozaliwa kabla ya wakati na uzito mdogo (njiti), ambao imebanika kuwa na tatizo hilo kutokana na mabadiliko yanayotokea kwao.
Amesema shinikizo la juu la damu kwa mtoto mdogo ambaye hulazimika kuanzishiwa matibabu, huendelea kutibiwa maisha yake yote.
“Yale madhara ya shinikizo la juu la damu, ikiwemo matatizo ya moyo, figo na magonjwa mengine yatajitokeza mapema zaidi kwake,” amesema.
Dk Jida amesema shinikizo la juu la damu la msingi huonekana kwa watoto wanaozaliwa na matatizo ya figo.
Kwa upande wake, Dk Kandi Muze, mtaalamu wa afya kwa watoto aliyejikita zaidi kushughulikia masuala ya unene, sukari na homoni, kutoka MNH, amesema mara nyingi wanapotoa matibabu hospitalini wakiona mtoto ana shinikizo la juu la damu ni lazima watafute sababu.
Amesema tofauti na watu wazima, wanapobaini kwa mtoto chini ya miaka mitano lazima waangalie figo zake kama zinafanya kazi vizuri.
Dk Muze amesema pia huangalia kama wana matatizo mengine ya homoni yanayosababisha kupanda kwa sukari au visababishi vya moyo.
“Utafiti huu umebaini uzito walionao watoto unachangia kwa kiasi kikubwa,” amesema.
Kwa mujibu wa Dk Muze, uzito na urefu wa mtoto chini ya miaka mitano hutafsiriwa kupitia kadi la kliniki ambalo mtoto anatakiwa kuendelea kupimwa mpaka anapofikisha umri huo.
“Kadi ya kliniki ina mwongozo mzuri,” amesema.
Dk Jida ameshauri wazazi wasione uzito mkubwa una tathmini afya nzuri kwa mtoto na uzito mdogo kadhalika. Amesema mtoto kuwa na uzito uliozidi ni kiashiria cha hatari vilevile akiwa na uzito wa chini.
“Mzazi aangalie vyakula anavyompa mtoto viwe vya mlo unaofaa, visiwe na sukari nyingi na vinywaji vilivyoongezwa sukari pia havifai vinasababisha uzito mkubwa.
“Watoto wale matunda kwa wingi, mbogamboga, nafaka zisizokobolewa, vyakula ambavyo vitasaidia kupunguza tatizo la uzito mkubwa na kupata virutubisho vinavyostahili,” amesema.
Dk jida amesema watoto wengi hawaushughulishi mwili, wengi wanakaa kuangalia katuni na kucheza gemu za video vitu vinavyochangia uzito mkubwa.
Daktari bingwa wa watoto na figo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Francis Furia amesema ni muhimu kwa wazazi kuangalia visababishi vya shinikizo la juu la damu kwa watoto, ikiwemo uzito mkubwa na unene kupita kiasi.
Dk Furia aliyeshiriki kufanya utafiti huo amesema matumizi ya vyakula vyenye chumvi kupita kiasi na sukari, ikiwemo ya viwandani ndiyo sababu.
Amewataka wazazi kuangalia mtindo wa maisha ili kuondokana na changamoto hiyo.
Kwa upande wake, Dk Muze amesema watoto wa mijini wengi wana uzito mkubwa kuliko wa kijijini kutokana na kutofanya mazoezi.
“Wanaondoka nyumbani na mabasi ya shule, wanarudi nayo. Shule nyingi suala la michezo hawalitilii maanani, watoto hawachezi na kufanya mazoezi.
“Akirudi nyumbani amepewa ‘homework’ nyingi, mazoezi hakuna vyakula si salama. Watoto wa vijijini wanacheza, wanatembea kwenda shule kwa hiyo shida kubwa ni ulaji wa mijini tofauti na vijijini, wenzetu wanakula vyakula vya asili. Mijini mama yupo ‘bize’ anarudi na baga au piza hana muda wa kuandaa chakula bora,” amesema.
Baadhi ya wazazi wa maeneo ya mijini wanasema changamoto za kimaisha zinasababisha baadhi ya watoto kuwa na uzito kupita kiasi kama anavyoeleza mkazi wa Tabata Chang’ombe, Honoratha Swai.
“Watoto wangu wanasoma mbali, lazima watumie gari la shule kwa kuwa nami nashinda kazini siwezi kuwa na amani wakienda wenyewe shuleni. Hata wakirudi nimemwagiza binti wa kazi wacheze ndani wasitoke nje kwa sababu za kiusalama,” anasema.
Anasema matamanio yake ni watoto wake kuwa huru lakini sababu za kiusalama zinachangia wakae ndani muda mwingi, hivyo kuwa na uzito kupita kiasi.
Akizungumzia kuhusu uzito unaotakiwa kwa watoto, Mtaalamu wa Afya ya Jamii, Dk Ali Mzige amesema hupimwa kwa kuchukua umri wake ukazidisha mara mbili ukajumlisha na nane akitoa mfano wa mtoto wa miaka miwili anapaswa kuwa na kilo 12 (2×2+8= 12).
“Mtoto mwenye umri wa miaka miwili anapaswa kuwa na uzito wa kilo 12 na mwenye umri wa miaka mitano anapaswa kuwa na uzito wa kilo 18 hii haijalishi anaishi Ulaya au Tanzania, hii ndiyo kanuni ya afya,” amesema Dk Mzige aliyewahi kuwa Mkurugenzi wa Kinga Wizara ya Afya mwaka 2005.