NETUMBO NANDI-NDAITWA
RAIS Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, alikuwa miongoni mwa wageni mashuhuri waliohudhuria hafla ya kuapishwa kwa Rais mpya wa Namibia, Mhe. Netumbo Nandi-Ndaitwah, iliyofanyika leo tarehe 21 Machi 2025 katika jiji la Windhoek.
Katika picha ya pamoja iliyopigwa mara baada ya tukio hilo la kihistoria, Dkt. Kikwete anaonekana katikati, huku pembeni kulia kwake akiwa ni mwenyeji wake – Rais mpya Mhe. Netumbo Nandi-Ndaitwah.
Kushoto kwa Dkt. Kikwete ni Jenerali Epaphras Denga Ndaitwah, ambaye ni mume wa Rais mpya – akiweka historia kama “First Gentleman” wa kwanza katika historia ya Namibia.
Kushoto kwa picha hiyo ni Rais aliyemaliza muda wake, Mhe. Nangolo Mbumba, aliyehudhuria hafla hiyo na kukabidhi rasmi madaraka kwa mrithi wake. Kulia kabisa ni Mama Sustjie Mbumba, mke wa Rais Mstaafu wa Namibia.
Hii ni mara ya kwanza kwa Namibia kupata Rais mwanamke, jambo lililopokelewa kwa shangwe si tu ndani ya nchi hiyo, bali barani Afrika kwa ujumla. Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt Samia Suluhu Hassan pia alihudhuria hafla hiyo, na kushuhudia kwa furaha wakati Mwanamke mwenzie akitwaa madaraka kwa mara ya kwanza nchini humo, kama alivyofanya yeye miaka minne iliyopita.
Tanzania na Namibia zina historia ya muda mrefu ya uhusiano wa kindugu na kidiplomasia, hususan kuanzia enzi za harakati za ukombozi wa kusini mwa Afrika.