UNAMFAHAMU yule kipa raia wa Nigeria Amas Obasogie, ambaye anaichezea Singida Black Stars, sasa anaonekana kwenye uzi wa timu ya Taifa ya Nigeria na inafahamika kuwa yupo hapa nchini kwa tiketi ya Yanga akiwa anatarajiwa kuwa kwenye uzi wa Wanajangwani hao msimu ujao.
Lakini takwimu zake pia zinaonyesha kuwa ni mtu haswa, akiwa ameshafanya mambo makubwa kwenye michezo ya Ligi Kuu Bara ambayo ameshacheza tangu ajiunge na Singida kwenye usajili wa dirisha dogo.
Ndani ya muda mfupi aliocheza katika kikosi cha Singida Black Stars, kipa huyo raia wa Nigeria kameonekana kuwa na sifa zinazoelekea kufanana na zile za Djigui Diarra ambaye anaweza kuwa katika vita ya kuwania nafasi ya kucheza katika lango la Yanga msimu ujao.
Obasogie ameonyesha uwezo mkubwa wa kuchezea mpira kwa miguu na kupiga pasi ambazo zinafikia walengwa kwa usahihi kama ambavyo Diarra amekuwa akifanya lakini pia ameonyesha uwezo wa kuondosha hatari ambazo amekuwa akielekezewa.
Na haishangazi kuona tangu alipoanza kuitumikia Singida Black Stars baada ya kipindi cha usajili wa dirisha dogo, kipa huyo ameruhusu nyavu zake kutikiswa katika mchezo mmoja tu huku washambuliaji wa timu pinzani wakishindwa kuziona nyavu zake katika michezo minne.
Mechi ambayo Obasogie amefungwa mabao ni dhidi ya Pamba katika Ligi Kuu ambayo ilichezwa Februari 23 mwaka huu na kumalizika kwa sare ya mabao 2-2.
Kipa huyo hajafungwa bao katika mechi tatu za Ligi Kuu dhidi ya KMC, Namungo FC, Mashujaa SC na JKT Tanzania.
Jambo lingine linalomuweka Obasogie katika muelekeo wa kufanana na Diarra ni namna ambavyo makipa wote wawili wamejihakikishia nafasi katika vikosi ya timu wanazochezea ambapo wote wawili wamefanikiwa kuwa chaguo la kwanza golini baada ya kumzidi kete, kipa Metacha Mnata.
Diarra alishinda vita ya kuwania namba dhidi ya Metacha mara baada ya kujiunga Yanga na hadi sasa amekuwa kipa namba moja na sasa Obasogie naye amejihakikishia utawala wa lango la Singida Black Stars kwa kumnyang’anya nafasi Metacha.
Obasogie pia licha ya kutokea katika taifa ambalo lina kundi kubwa la wachezaji wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi yao hasa wengi wakicheza Ulaya, amefanikkiwa kupenya na kuwa miongoni mwa makipa watatu wanaounda kikosi cha timu ya taifa ya Nigeria kinachocheza mechi za kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026 ingawa hana uhakika wa kuanza katika mechi.
Ni hadithi inayofanana na Diarra ambaye amekuwa ana uhakika wa kuitwa ingawa yeye ana uhakika wa kucheza katika kikosi cha timu ya taifa ya Mali.
Akizungumzia wawili hao, kocha wa zamani wa makipa wa Taifa Stars, Juma Pondamali alisema pamoja na kiwango kizuri ambacho Obasogie ameanza kukionyesha, ana kazi kuba ya kufanya kufikia daraja la Diarra.
“Diarra ameshacheza hapa kwa muda mrefu na aliyofanya ni makubwa na kumfananisha na kipa ambaye hajafikisha hata mechi 10 sio sawa.
Nimemuona ni kipa wa sasa na nampongeza kwa kuonyesha kiwango kizuri kwa mechi chache alizocheza na kuaminiwa na Nigeria lakini kiukweli anatakiwa atuthibitishie kwamba ni mchezaji wa daraja la juu kama alivyofanya Diarra,” alisema Pondamali.
Hata hivyo, alisema kitendo cha kuaminiwa na taifa kubwa kama Nigeria kinaonyesha kuwa ni kipa wa daraja la juu.