Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo; Tundu Lissu , Makamu wake Bara John Heche pamoja na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho Godbless Lema wamekutana na kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya Raila Odinga.
Viongozi hao wa CHADEMA wamekutana na Odinga leo Machi 22, jijini Nairobi nchini Kenya baada ya kutoka Zanzibar walipokwenda kujitambulisha kwa wanachama wao waishio Kenya.
Kupitia mtandao wa X Odinga ameandika “Nilifanya mazungumzo na viongozi wa upinzani wa Tanzania waliokuwa ziarani, ambao walinitembelea kwa heshima. Tulibadilishana mawazo kuhusu kuimarisha demokrasia barani Afrika, ikiwemo mchango madhubuti wa vyama vya siasa ndani na nje ya serikali katika maendeleo ya taifa.”
Odinga ameongeza kuwa amewahimiza CHADEMA kufanya mazungumzo na kushirikiana na serikali katika kuilinda demokrasia na amani ya nchi.
“Niliwahimiza kutilia mkazo mazungumzo na ushirikiano wa kujenga na serikali yao kwa maslahi ya taifa na kulinda demokrasia ya Tanzania. Natarajia uchaguzi wa amani na uwazi katika uchaguzi ujao wa Tanzania.”
Kupitia mtandao wa X Lema ameandika “Leo katika Jiji la Nairobi tumekuwa na kikao kizuri na Mheshimiwa Raila Odinga, tumejadili masuala mengi ya maendeleo ya dunia na zaidi sana msingi wa demokrasia, siasa safi na utawala bora katika ukanda wetu wote wa Afrika Mashariki.”
Stori Na Elvan Stambuli, GPL