Majaliwa aiagiza Wanging’ombe kukamilisha ujenzi wa bwalo

Njombe. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe kutenga fedha kupitia mapato yake ya ndani kukamilisha ujenzi wa bwalo la chakula katika shule ya sekondari ya wasichana ya Mkoa wa Njombe.

Majaliwa ametoa agizo hilo leo Machi 22, 2025 wakati akikagua ujenzi wa shule hiyo iliyopo katika Kijiji cha Usalule Wilaya ya Wanging’ombe mkoani Njombe.

Amesema shule ya wasichana ya sekondari haiwezi kuwa na zaidi ya wanafunzi 400 lakini wakawa wanahangaika kwa kuwa hawana bwalo kwa ajili ya kulia chakula.

Ameeleza kwamba matamanio ya wananchi ni kuona miundombinu hiyo inakamilika kwa kuwa fedha kutoka serikali kuu zilitolewa na sehemu inayotumika kwa sasa haiwezi kuwa ya kudumu.

“Kwa kuwa mmeshakusanya fedha za Januari hadi Machi, mwezi ambao haujaisha, mtakuwa na fungu lenu la miezi mitatu na mtakuwa na miezi mitatu mingine, lazima mlete fedha hapa,” amesema Majaliwa.

Amesema halmashauri nyingi zimejisahau kutoa fedha kwa ajili ya miradi yake na kutegemea fedha kutoka Serikali Kuu pekee, jambo linalosababisha kuchelewa kukamilika kwa miradi.

Waziri Mkuu amesema ujenzi wa shule za wasichana nchini ni msukumo unaowafanya watoto wa kike kufikia ndoto zao licha ya kukabiliana na changamoto nyingi kuliko watoto wa kiume.

Amesema kuwakusanya pamoja wanafunzi wa kike katika shule moja ni kuwapa nafasi ya kushughulika na masomo kuliko mambo mengine ambayo hayana manufaa kwa upande wao.

“Tunajua mtoto wa kike anapokuwa nyumbani lazima awe karibu na mama kumsaidia majukumu kupika, kutafuta kuni kuchota maji na kutwanga, jambo ambalo linamnyima nafasi ya kusoma,” amesema Majaliwa.

Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe, Zakaria Mwansasu amesema halmashauri hiyo imeendelea kutenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa bwalo hilo ambapo kwa bajeti iliyopo ili kulikamilisha zinahitajika Sh750 milioni.

“Ndani ya miezi miwili ijayo, tutakamilisha kwa kutumia mapato ya ndani ili bwalo la wanafunzi liwe na sehemu salama kwa ajili ya chakula,” amesema Mwansasu.

Amesema katika kuhakikisha kuwa wanaondoa matumizi ya kuni katika shule hiyo, wameanza mazungumzo ili kujenga miundombinu ya gesi ili kusaidia katika kupika.

Kwa upande wake, mbunge wa Wanging’ombe, Festo Dugange amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa Sh4.3 bilioni huku Halmashauri ya Wilaya ya Wanging’ombe ikiongeza Sh400 milioni kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo.

“Shule hii Mheshimiwa Waziri Mkuu, ni mkombozi mkubwa kwa sekta ya elimu hususani wanafunzi wetu watoto wa kike, kwanza ina mabweni ya kutosha, maktaba na maabara za sayansi,” amesema Dugange.

Mkazi wa Kijiji cha Usalule, Albert Mgeni ameishukuru Serikali kwa kujenga shule hiyo katika eneo hilo kwani watoto wao watafikia ndoto zao za elimu kupitia shule hiyo.

Related Posts