Mayanga aanza na mabao Mashujaa

SIKU chache baada ya kuungana na Mashujaa FC, Kocha mkuu wa timu hiyo, Salum Mayanga amesema hawapi majukumu washambuliaji pekee kufunga katika kikosi hicho, bali amewapa uhuru wachezaji wote kuifanya kazi hiyo.

Kwa sasa Mashujaa inajiandaa na mchezo wa Kombe la Shirikisho (FA) Machi 29, 2025 dhidi ya Pamba Jiji, huku timu hiyo katika mechi 23 za Ligi Kuu Bara msimu huu imefunga mabao 19 pekee, kitu ambacho kimemshtua kocha huyo na kuwataka wachezaji wote kutumia nafasi wanazozipata bila ya kuwategemea washambuliaji pekee.

Kinara wa upachikaji mabao Mashujaa, ni kiungo mshambuliaji David Ulomi aliyeingia kambani mara nne kati ya mabao 19 yaliyofungwa na timu hiyo huku wakiruhusu nyavu zao kutikiswa mara 28.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mayanga alisema wachezaji wote wana kazi ya kutafuta matokeo uwanjani, hivyo ni lazima watumie nafasi wanazozipata bila kujali nafasi zao.

“Unaona kwenye mabao tuliyofunga, washambuliaji wetu hawajafunga mengi. Ipo hivyo kulingana na namna wachezaji wanavyoshirikiana kwenye kutimiza majukumu.

“Hakuna mchezaji ambaye kazi yake ni kufunga, kila mmoja anaweza kufanya hivyo, sasa naamini hili likifanyiwa kazi tutaongeza idadi ya mabao, pia mabeki wanatakiwa kupunguza makosa ili kuwa salama eneo hilo,” alisema Mayanga.

Mayanga ambaye amechukua mikoba ya Abdallah Mohammed ‘Bares’, tayari ameungana na timu na anaendelea kuinoa kuelekea mchezo huo wa Kombe la FA dhidi ya Pamba Jiji ambao utakuwa wa kwanza kwake tangu ajiunge na kikosi hicho akitokea akitokea Mbeya City.

Related Posts