Na Belinda Joseph, Nyasa Ruvuma.
Wakazi wa Kata ya Ngumbo na Liwundi waliopo katika vijiji vitano vya Ngumbo, Mbuli, Mkili, Liwundi na Yola wapatao elfu 11080 wanatarajiwa kupata huduma ya maji safi na salama kwenye maeneo yao wanayoishi na hivyo kutumia muda mwingi kufanya shughuli za kujiongezea kipato pamoja na kupunguza magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi wa maji wa Ngumbo group awamu ya pili katika kilele cha maadhimisho ya wiki ya maji Machi 22 2025, ambayo kiwilaya yamefanyika Kijiji cha Mkili Wilayani Nyasa Mkoani Ruvuma, Kaimu Meneja wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini RUWASA Wilaya ya Nyasa Mhandisi Evath Rwekaza, ameeleza hali ya utekelezaji wa mradi huo kwa ujumla umefikia asilimia 75 ambapo jamii tayari imeanza kupata huduma ya maji kupitia vituo vilivyojengwa pamoja na maunganisho binafsi.
Ameeleza changamoto iliyojitokeza ni hali ya mvua ambazo zimeendelea kunyesha kipindi cha masika kwa nyakati tofauti wakati wa ujenzi wa mradi na kuathiri kasi ya utekelezaji, ambapo RUWASA katika kukabiliana na changamoto husika, utekelezaji wa mradi uliendelea kufanyika siku ambazo hali ya hewa iliruhusu kuendelea na shughuli, Aidha muda wa utekelezaji umeongezwa kufidia muda uliopotea.
Akizungumza Mgeni rasmi katika hafla hiyo ya kuweka jiwe la msingi kwa mradi huo wa maji Mbunge wa Jimbo la Nyasa, Eng. Stella Martin Manyanya, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan pamoja na Waziri wa Maji na Katibu Mkuu Wizara ya Maji kwa juhudi zao za kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi bila kujali hali zao za kiuchumi.
Eng. Manyanya amesisitiza kuwa sera mpya ya maji inalenga kuwafikia watu wote kwa kuhakikisha wanapata maji safi na salama, kwani maji ni chanzo cha uhai na ustawi wa jamii, Ameongeza kuwa jitihada za serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anaishi kwa ustawi kupitia upatikanaji wa huduma bora za maji.
Aidha, Eng. Manyanya alitoa pongezi kwa watumishi wote wa RUWASA kwa kujituma na kupambana kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi, ameeleza kuwa changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji katika hospitali za vijijini imepungua, na wananchi sasa wanapata huduma hii muhimu, jambo ambalo linaboresha huduma za afya na maisha ya wananchi kwa ujumla.
Madiwani wa Kata za Liwundi na Ngumbo wametoa shukrani za dhati kwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuleta maendeleo kupitia miradi ya maji katika maeneo ambayo hayajafikiwa na huduma hiyo muhimu wameeleza furaha zao mara baada ya miradi ya maji kuanza imefanikiwa kufikia vitongoji mbalimbali ndani ya kata hizo, jambo ambalo limeleta mabadiliko makubwa kwa wananchi wa maeneo hayo.
Wameweka bayana changamoto kubwa inayowakumba wakazi wa kitongoji cha Ndandawala, ambapo wananchi wanapaswa kuamka mapema saa 11 alfajiri na kwenda kufuata maji kwa zaidi ya masaa manne wameitaka serikali kusaidia wanawake wa Ndandawala kwa kuleta mradi wa maji katika eneo hilo, ili kuondoa adha ya wananchi hao na kuboresha maisha yao kwa ujumla.
Kwa upande wa Wananchi wa kata za Liwundi na Ngumbo wameonyesha furaha yao na dhamira yao kubwa waliyonayo ambapo wanatarajia kuona maendeleo katika sekta ya maji yakikamilika, jambo litakaloleta matumaini mapya ya maendeleo katika eneo hilo na jamii kwa ujumla.
Mradi wa Maji Ngumbo group awamu ya pili unatekelezwa na Mkandarasi Mzawa NIPO AFRICA ENGINEERING COMPANY LIMITED kutoka Dodoma kwa gharama ya zaidi ya Bilioni 2 ambao unatekelezwa kwa fedha ya Mfuko wa Maji wa Taifa (NWF), Serikali kuu (GoT)na P4R, mkataba uliosainiwa tarehe 25 Agosti 2023 na utekelezaji wake ulianza rasmi tarehe 1 Novemba 2023 na kutarajiwa kukamilika 30 Aprili 2024, ambapo kwasasa mradi unatarajia kukamilika tarehe 30 juni 2025, baada ya kuongezewa muda wa utekelezaji kwa vipindi vitatu tofauti.