Moshi. Mbunge wa Siha (CCM) ambaye pia ni Naibu Waziri wa Afya, Dk Godwin Mollel amedai kuandikiwa barua na kamati ya nidhamu ya CCM Wilaya ya Siha kwa kosa alilodai kuwa ni kuwafukuza wezi waliojaribu kupora rasilimali za Siha.
Dk Mollel ameeleza hayo kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii ya Instagram na Facebook, jambo ambalo limeibua sintofahamu na kukoleza minyukano ya wanasiasa jimboni humo kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Mwananchi limemtafuta Dk Mollel kuthibitisha kama andiko hilo mtandaoni ni lake ambapo amekiri kwamba ni lake.
Dk Mollel ameandika: “Hapa nilikuwa namwambia boss (inaonekana picha akiwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa), wapinzani wangu jimboni nimewanyoosha hadi sasa wamebaki kutumia vibaraka wao waliopo kamati ya siasa; kumlazimisha Katibu CCM wa Wilaya, kuandika barua za vitisho na hata hoja kwenye barua yenyewe hamna.
“Mara ooh…unasumbua wazee wa chama, wazee wenyewe nimewapokonya Sh316 milioni walizotaka kupora Ushirika wa Siha Kiyeyu, pia, sasa wanalipa zaidi ya Sh200 milioni ambazo hazionekani.
“Na wengine nimewafurumusha nikiwa na wananchi 700 na madiwani wakiiba ardhi ya Siha kuwekeza kitapeli, ambao walitaka kuuza ardhi ya Leoni; sisi na madiwani tuliowafukuza mafisadi hawa, tumeandikiwa barua ya kamati ya nidhamu. Kicheko…! Hivi kwa akili ya kawaida, anayeitwa Polisi ni mwizi au mfukuza mwizi, ilibidi tucheke sana.”
Katika andiko hilo, Dk Mollel ameenda mbali zaidi akieleza kuwa kinachosikitisha ni wao waliofukuza wezi, ndiyo wameitwa kwenye kamati ya nidhamu, ilihali wazee waliouza ndiyo wamewashitaki kuwa wana makosa.
“Kamati hiyo ya siasa inajua fika kuwa hao wazee ndiyo wabadhirifu na Wizara ya Kilimo inajua pamoja na vyombo vimethibitisha na document (nyaraka) zipo.
“Boss ameniambia, Rais wetu, Dk Samia Suluhu Hassan anataka rasilimali za Siha zilindwe kwa gharama yoyote, na ameniambia anakuja Mei kuongeza nguvu kwenye ulinzi wa rasilimali za wanaSiha. Nimemuomba ruhusa niingie Siha kuanzia Ijumaa ili niwanyooshe hadi Jumanne nirudi bungeni.”
Alipotafutwa kuzungumzia ujumbe huo unaodaiwa kuwa wa Dk Mollel kwenye kurasa zake za mitandao yake ya kijamii, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Siha, Wilfred Mosi amesema alichokiandika mbunge huyo ni maoni yake na siyo ya chama.
Mosi amesema chama hicho kinaongozwa na katiba, kanuni na taratibu zake na kwamba kikao cha kamati ya siasa ni kikao cha ndani na kwamba kinachojadiliwa ndani ya kamati hiyo hakipaswi kutolewa nje hadharani au kuwekwa kwenye mitandao.
“Alichoandika Dk Mollel kwenye mitandao, ni maoni yake na siyo ya chama. Anajua taratibu, katiba na kanuni za chama; na kukimbilia kwenye mitandao sio tiba.
“Hatujamwomba aandike kwenye mitandao, yanayozungumzwa ndani ya kamati yanabaki kwenye kamati, siyo kupeleka kwenye mitandao,” amesema Mosi.
Mbali na ufafanuzi huo wa mwenyekiti wa wilaya, mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Wilaya hiyo, ambaye hakutaka kutaja jina lake, amesema alichokifanya mbunge huyo siyo sahihi.
“Alichokifanya mbunge wetu… kwenda kutoa taarifa kama hizo na kukitukana chama, siyo jambo jema kabisa.
“Kilichotokea hata mimi nimeshangaa, nimemwona kwenye mtandao wa Instagram na kwenye group letu la kamati ya siasa ya wilaya na kwenye magroup yetu mengi ya WhatsApp ya Wilaya ya Siha.
“Chama Cha Mapinduzi kinaongozwa na taratibu na kanuni na kama kuna barua aliandikiwa ya onyo, naamini ni barua ya siri, sasa sikutarajia kilichotokea, hakupaswa kufanya hivyo.”
Suala jingine, kwamba katibu amelazimishwa na kamati ya siasa kwenye andiko hilo, ameandika kwamba katibu kalazimishwa, lakini naamini kwamba katibu ni mtendaji mkuu wa chama na yupo kama mjumbe wa siasa; na Mollel naye ni mjumbe wa siasa. Hivyo, naamini hakuna chochote kilichofanywa kwa ubaya, ni katika kurekebishana.”
Akizungumzia jambo hilo, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Siha, Meijo Laizer amesema alichokifanya mbunge wao ni kuonyesha kiburi kwa chama ambacho kimempa dhamana ya kuwa kiongozi na kwamba anapaswa kuwajibishwa.
“Alichoandika mbunge ni kuonyesha kiburi kwenye chama na kuonyesha kuwa chama siyo chochote kwake. Kutotambua heshima aliyopewa na watu wa Siha na chama kwani hata hiyo nafasi ya unaibu waziri ameipata kwa sababu yeye ni mwanaCCM,” amesema Laizer.
Ameongeza kuwa: “Hata yale aliyoandika, mimi binafsi kama kiongozi, maoni yangu ni kwamba anapaswa kuchukuliwa hatua kwa sababu sidhani kama kiongozi mkubwa kama yeye ambaye amepewa heshima ya kuwa mbunge na naibu waziri anaweza kuonyesha dharau kwa kamati ya siasa.
“Amedharau dhamana aliyopewa na watu wa Siha, kwa maana ya wana CCM na wananchi wote wa Siha. Huyu anapaswa kuwajibishwa na mamlaka.”
Desemba 14, 2017, Dk Godwin Mollel aliyekuwa mbunge wa Chadema wakati huo, alitangaza uamuzi wa kujivua uanachama wa chama hicho na kujiunga na CCM kupitia kile kilichoitwa kampeni ya kuunga mkono juhudi. Desemba 15, 2025, alikabidhiwa kadi ya CCM.
Dk Mollel, ambaye alikuwa mgombea ubunge wa Siha (CCM) mwaka 2020, alishinda kiti hicho kwa kupata kura 22,172 akimwacha kwa mbali mpinzani wake wa siku nyingi, Elvis Mosi (Chadema), aliyepata kura 8,614.
Wagombea wengine ni Leslie Kileo (NCCR Mageuzi) aliyepata kura 306 na Amedeus Kitali (ACT Wazalendo) aliyepata kura 418.