Hujafa hujaumbika! Said Ismail (42), mkazi wa Mbagala Kilungule alikuwa mzima kama walivyo watu wengine lakini kwa sasa, hali yake inahuzunisha.
Yupo katika maumivu makali baada ya jicho lake moja kutoka nje, akihitaji shilingi milioni tatu, laki saba na elfu ishirini (3,720,000) ili aweze kufanyiwa upasuaji.
Ikiwa hatapata matibabu hayo, jicho lake linaweza kusababisha madhara makubwa zaidi ikiwa ni pamoja na kupoteza maisha, lakini kama jicho hilo litafanyiwa upasuaji, anaweza kurudi kwenye hali yake kama zamani.
Akizungumza na Global TV Online, Said alisema kuwa jicho lake lilijeruhiwa wakati akikata kuni shambani, aliporukiwa na kijiti kidogo kilichoingia ndani ya jicho.
Alishindwa kwenda hospitalini kutokana na kukosa fedha, hivyo alijaribu kutibu maumivu kwa kukanda na maji ya moto tu hadi hali hiyo ikafikia pabaya.
Hatimaye, aliamua kuja jijini Dar es Salaam kutoka Kilwa ili kupata msaada.
Alianzia Hospitali ya Temeke na baadaye akapelekwa Muhimbili kwa uchunguzi zaidi, ambapo anatakiwa kiasi hicho cha fedha ili afanyiwe upasuaji wa haraka.
Iwapo unataka kumsaidia apate matibabu ya haraka, unaweza kutuma chochote kupitia namba yake ya simu 0718 912998 iliyosajiliwa kwa jina la ndugu yake, Zaituni Hamisi.