Dar es Salaam. Wakati kiwango cha fedha kinachowekwa benki kupitia mawakala kikiongezeka kuliko kile kinachotolewa, wachumi wamesema inaweza kuwa moja ya hatua nzuri kueleke uchumi wa kidijitali.
Ripoti ya uchumi wa kikanda ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha kuwa katika robo ya mwaka iliyoishia Septemba 2024 zaidi ya Sh25.84 trilioni zilizowekwa benki katika kipindi hicho zilipitia kwa mawakala.
Kiwango hicho kilikuwa ni ongezeko kutoka Sh21.12 trilioni zilizowekwa kipindi kama hicho mwaka uliotangulia.
Hata hivyo kwa upande wa kutoa, ni Sh8.35 trilioni pekee ndiyo zilitolewa kupitia mawakala katika mwaka ulioishia Septemba 2024 ikiwa ni ongezeko kutoka Sh6.67 trilioni.
Mchambuzi wa masuala ya Uchumi na Biashara, Dk Donath Olomi anasema ongezeko hilo huenda limechangiwa na kupunguzwa kwa gharama za makato ambazo zinaweka urahisi watu kulipia huduma mbalimbali kwa njia ya simu kutoka benki.
“Na hii inaweza kuwa chachu pia ya watu kuongezeka katika kutumia huduma za benki kwa njia ya simu, intaneti,” amesema Olomi.
Amesema pia kitendo cha watu kuweka zaidi ni tafsiriwa na urahisi wanaoupata wanapotumia mawakala kuliko kwenda benki ambazo wakati mwingine ziko mbali na makazi wanayoishi au kulazimika kupanga foleni.
“Japokuwa kuna ATM ambazo sasa hivi unaweza kuweka hela lakini nadhani elimu hii bado haijafika vizuri na badala yake mawakala wanabaki kuwa watu rahisi kufikiwa. Katika kutoa sasa makato yanaweza kuwakimbiza wengi na ATM kuonekana rahisi,” amesema.
Amesema ikiwa matumizi ya malipo ya kidijitali yataendelea kukua kwa kasi yataondoa mianya yote ya utoaji na upokeaji rushwa katika ofisi mbalimbali kwani watu watakuwa na uwezo wa kufanya kila kitu wenyewe.
“Tunachopaswa kufanya ni kutengeneza mazingira wezeshi ili watu wengi waweze kuhamia huku na kuachana na matumizi ya fedha taslimu, baadhi ya watu bado wanakimbia makato,”
Mbali na yaliyosemwa na Dk Olomi, pia ripoti hii inaonyesha kuwapo kwa ongezeko la mawakala wa benki jambo ambalo linaweza kuwa moja ya sababu ya ongezeko la fedha zinazopitia huko.
Idadi ya mawakala imeongezeka kwa asilimia 40.3 hadi kufikia 132,543 katika robo iliyoishia Septemba 2024 kutoka mawakala 94,484 waliokuwapo kipindi kama hicho mwaka uliotangulia.
Hilo lilienda sambamba na ongezeko la idadi ya miamala iliyofanywa hadi kufikia milioni 26.257 kutoka milioni 22.889 kwa waliokuwa wakiweka, huku waliotoa miamala ikifikia milioni 13.859 kutoka miamala milioni 12.468. Miamala hiyo ni sawa na ongezeko la asilimia 14.7 na asilimia 11.2, mtawaliwa.
Akitoa maoni yake kuhusu hilo mtaalamu wa uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), Dk Lutengano Mwinuka anasema huduma nyingi za malipo sasa zinafanyika kwa njia ya simu ndiyo moja ya sababu ya kiwango kinachotolewa kuwa kidogo kuliko kinachowekwa.
“Kama watu wanaweka kuliko kutoa maana yake matumizi ya malipo njia ya mtandao yanaongezeka na kumekuwa na upokeaji mdogo wa fedha taslimu. Hili linaonekana katika maeneo mbalimbali na hata huduma nyingi za serikali ikiwemo malipo ya bili kama za maji, faini, tozo sasa hivi unalipa kwa kutumia namba maalumu (control number),” amesema.
Anasema imefanya watu kuanza kuona kuwa utaratibu huo ni wa kawaida kutumika huku akisema kundi ambalo linaachwa nyuma sasa ni lile la sekta binafsi ambalo linapaswa kuhamasishwa ili waongeze matumizi ya namba katika malipo.
“Kinachopaswa kufanywa sasa ni kuongeza ufanisi zaidi katika hili ili kuondoka kabisa katika matumizi ya fedha taslimu katika kulipia huduma mbalimbali, hili litawezekana ikiwa mtandao utaimarishwa ili kusiwe na usumbufu wa kutoa hizo namba ili watu walipie huduma wanaozihitaji katika maeneo tofauti,”
Kwa mujibu wa Dk Lutengano, matumizi ya kidijitali katika kulipia huduma mbalimbali kunarahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuwapunguzia muda wanaotumia kwenda kutafuta huduma.
Badala yake, muda ambao walikuwa wakiutumia katika foleni kusubiri huduma au kusafiri kufuata huduma za kibenki utaelekezwa katika shughuli za kiuchumi.
“Jambo hili litaongeza ufanisi katika kufanya shughuli za kiuchumi tofauti na ilivyokuwa hapo mwanzo ambapo matumizi ya fedha taslimu ndiyo yalitumika zaidi katika kulipia huduma mbalimbali,” amesema Dk Lutengano.
Kuhusu kurahisishwa kwa malipo ya kibenki katika huduma mbalimbali BoT imeshapiga marufuku kutoza ada au gharama za ziada katika miamala inayofanywa kwa kutumia mashine za malipo ya wafanyabiashara (POS) huku ikiwataka wananchi kutoa taarifa watakapokutana na hali hiyo.
Hili lilifanyika ili kuhamasisha matumizi ya malipo ya kidijitali nchini huku hatua hiyo ikilenga kuhakikisha kuwa malipo yanayofanywa kwa kutumia mashine za malipo za wafanyabiashara (Point of Sale – POS) ni bure kabisa kwa watumiaji wa kadi.
Kwa mujibu wa miongozo kuhusu ada na tozo kwa watoa huduma ndogo za fedha, 2024 kifungu cha 19, kinakataza benki au taasisi ya kifedha na mfanyabiashara kutoza ada na tozo kwa watu wanaofanya malipo kwa wafanyabiashara kupitia kadi.
Kifungu kidogo cha pili kinasema bila kuathiri Mwongozo wa 19 (1), benki itaweka vikwazo kwa wafanyabiashara endapo watatoza ada ya ziada kwa malipo ya kidijitali ya wafanyabiashara.
“19(3) Bila kuathiri Mwongozo wa 19 (1) na (2), benki au taasisi ya kifedha itafanya yafuatayo, (a) Kutunza orodha ya wafanyabiashara wasiofuata masharti kulingana na Mwongozo wa 19 (1), (b) Kuwasilisha taarifa hizo kwenye daftari kuu la taarifa na (c) Kutumia taarifa hizo kama sehemu ya uhakiki wa kina na mapitio ya mikataba,” unaeleza mwongozo huo.
Adhabu inayotajwa na mwongozo huu ni faini au adhabu isiyozidi Sh20 milioni za Kitanzania kwa taasisi ya fedha itakayoshindwa kuzingatia matakwa ya miongozo hii.