Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesimulia alivyobebeshwa jukumu la kusimamia sekta ya maji akiwa Makamu wa Rais, baada ya kupewa taarifa mbaya ya usimamizi wa miradi ya sekta hiyo na Benki ya Dunia (WB).
Amesema alipewa jukumu hilo wakati ambao WB ilikosa cha kuandika katika ripoti ya miradi ya maji iliyotekelezwa kwa fedha ilizoifadhili Tanzania, baada ya kukuta zimetumika na miradi haikutekelezwa.
Amesema hayo jijini Dar es Salaam leo Machi 22, 2025 kwenye kilele cha wiki ya maji iliyoambatana na uzinduzi wa Sera ya Taifa ya Maji ya mwaka 2002, toleo la mwaka 2025.

Samia amesema akiwa makamu wa Rais, Mei 2016 alikutana na Mwakilishi Mkazi wa WB nchini, Bella Bird kuzungumza kuhusu masuala ya kilimo, mazingira na maji.
Katika mazungumzo hayo, amesema Bella alimpa orodha ya miradi ya maji iliyopatiwa fedha na benki hiyo kwa upande wa Tanzania lakini haikutekelezwa.
“Fedha hazipo, miradi haipo. Mama yule aliongea hadi akakaribia kulia, ananambia naandika nini, nasema nini? Mimi kama mkurugenzi nimeomba fedha zimekuja, nifanye nini,” amesema.
Rais Samia amesema baada ya hali hiyo, ilibidi Bella amweleze umuhimu wa Serikali ya Tanzania kuhakikisha inaongeza usimamizi katika sekta ya maji.
“Baada ya mkutano ule nilikwenda kwa bosi wangu (Rais wa awamu ya tano, hayati Dk John Magufuli) na kumweleza yote niliyosema na yule mama, alichonieleza na takwimu zote,” amesema.
Hatua hiyo, anasema ilimfanya Rais Magufuli ambebeshe jukumu la usimamizi wa sekta ya maji, akiahidi kumuunga mkono kwa kutoa bajeti ili mambo yaende.
Samia amesema huo ukawa mwanzo wa yeye kusimamia sekta ya maji, ambayo aliisimamia na matokeo ndiyo yanayoonekana sasa.
Katika hilo, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso alipozungumza kwenye maadhimisho hayo amesema miongoni mwa shuhuda mbaya ni mradi wa visima vya maji Bukoba mkoani Kagera, alikopewa taarifa vimechimbwa lakini alipokwenda eneo la tukio havikuwepo.
Jambo linalofanana na hilo, amesema lilitokea mkoani Shinyanga kwenye mradi wa gharama ya zaidi ya Sh1.3 bilioni lakini maji hayakuwa yanatoka.

‘Gridi’ ya taifa ya maji
Rais Samia amesema ni muhimu kusimamia usalama na uhakika wa maji, akisisitiza haja ya kuanzishwa mtandao wa maji wa Taifa aliotaja kama gridi ya maji, kama ilivyo kwenye umeme.
“Tunapozungumza usalama na uhakika wa maji lazima tuwe na gridi ya maji ya taifa. Kama tunavyokuwa na gridi ya taifa ya umeme ambayo umeme unakusanywa na unagawanywa katika pembe mbalimbali za Taifa,” amesema.
Amesema maji yanapaswa yakusanywe na kutengenezewa vituo katika kila kanda, kisha mgawo wake ufanywe kwa kutumia teknolojia ili kumaliza changamoto.
Rais amemtaka Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo kuhakikisha ndani ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 anaingiza suala la ‘gridi ya taifa ya maji’.
“Hilo ni agizo langu naweza nitoke nisimalize, lakini anayekuja atalimalizia. Hata mimi nimeingia nimetekeleza miradi chungu nzima. Ni vizuri kuanza ili kuonyesha njia wengine wamalize,” amesema.
Amesisitiza kulindwa vyanzo vya maji na miundombinu ili kuwaepusha wananchi na madhara mbalimbali.
“Tukiruhusu mabomba yapasuliwe, hatujui nini kitakwenda kuingia kwenye mabomba yaliyopasuka kwenda kwa watu wetu,” amesema.
Ameagiza kutunishwa Mfuko wa Taifa wa Maji kwa kuangalia vyanzo mbalimbali, jambo alilotaka litekelezwe na wataalamu.
Rais ametaka wabunifu wa teknolojia za mita za maji watumike kushirikiana na Serikali kuwatoza wananchi fedha kabla ya kuyatumia.
“Kuliko hizi za kuagiza ikiharibika kipuri haki mpaka uwapigie uende, hadi kifike tayari wananchi wanakosa maji,” amesema.
Amezungumzia sababu za mageuzi ya kisera, akisema ni kwa sababu idadi ya watu inaongezeka na siasa za dunia zinaelekea katika sekta ya maji.
Amesema maji ni muhimu na chanzo cha utulivu, kwani yasipotoka watu wanachukia.
Samia amesema kiongozi mzuri ni yule anayefananishwa na maji ambayo hayachagui wala kubagua hata yakichafuliwa.
“Ndiyo maana maji yanafafanishwa na viongozi wazuri katika dunia hii, wanasema kiongozi mzuri lazima awe kama maji. Kwa sababu maji ukiyatumia kusafisha, yanasafisha vitu vyote bila ubaguzi bila hukumu.
“Nenda kayatibue maji saa tatu asubuhi uyakoroge au kuweka uchafu, kisha sogea pembeni katika maji masafi, kosha miguu yako itakusafisha bila kinyongo. Na kiongozi anatakiwa kuwa hivyo, usafishe watu wote bila kusema huyu hakunipa kura, huyu alinitukana au kunisema vibaya, kiongozi mzuri ni yule anayehudumia watu wote, ndiyo sifa ya maji,” amesema.
Rais Samia ametunukiwa tuzo ya kuwa kinara wa sekta ya maji Afrika na kuteuliwa kuwa mlezi wa sekta ya maji na usafi wa mazingira Afrika, aliyopewa na Shirika la WaterAid la Uingereza.
Kutokana na tuzo hiyo, kampeni ya kumtua ndoo mama kichwani inatanuka kutoka Tanzania na kuwa Afrika kwa ujumla.
Pia amekabidhiwa tuzo ya kuwa kinara wa mabadiliko ya sekta ya maji iliyotolewa na Wizara ya Maji.
Akieleza mageuzi yaliyofanyika katika sekta ya maji, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema kumekuwa na utofauti wa ongezeko la wastani wa upatikanaji wa maji hasa vijijini.
Profesa Kitila aliyewahi kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji mwaka 2017 hadi 2020, amesema mwaka 2000 upatikanaji wa maji vijijini ulikuwa asilimia 32, mwaka 2005 asilimia 38, mwaka 2010 asilimia 48 na mwaka 2015 asilimia 47.
Katika kipindi hicho, amesema wastani wa ongezeko la upatikanaji wa maji lilikuwa kwa asilimia tano, lakini baada ya mwaka 2015 mambo yalibadilika.
Mwaka 2015, amesema Rais Samia akiwa Makamu wa Rais, alianzisha kampeni ya kumtua ndoo mama kichwani na wastani wa upatikanaji maji kutoka 2015-2020 uliongezeka hadi asilimia 70.1.
Mwaka 2020/24 amesema upatikanaji wa maji vijijini uliongezeka na kufikia asilimia 79.1 na kwa kipindi cha miezi mitano hadi sasa umefikia asilimia 83.
Katika kipindi chote hicho, amesema pamoja na Ziwa Victoria kuwa asilimia 51 upande wa Tanzania, maji yake yalitumika kidogo kwa ajili ya kunywa.
Lakini, uongozi chini ya Rais Samia amesema umeanzisha mradi wa maji kutoka ziwa hilo kwenda Dodoma kupitia Singida na kunawekwa mabomba mawili la maji ya kunywa na umwagiliaji.
“Katika utekelezaji huo, pamoja na bomba la maji ya kunywa kwenda Singida, pia kuna bomba la umwagiliaji kwa ajili ya mikoa ya Morogoro, Dodoma, Singida, Shinyanga na Tabora.
“Haya ni mapinduzi na sehemu ya kutekeleza ndoto yako ya Tanzania kulisha Bara la Afrika na kuwa miongoni mwa wazalishaji wakubwa watatu wa chakula wa mwanzo,” amesema.
Profesa Kitila amezungumzia pia Bwawa la Kidunda, akisema mradi ulibuniwa mwaka 1954 na ulibaki kwenye karatasi za Serikali lakini sasa umeshaanza kutekelezwa.
“Ukiacha mageuzi kwenye upatikanaji wa huduma, ni katika miundo. Katika kipindi chako (Rais Samia) imewekwa mifumo imara ya kusimamia sekta ya maji na kikubwa ni kuanzisha wakala maalumu wa kusimamia sekta ya maji vijijini,” amesema.