Dar es Salaam. Wakati kilio cha ajira kwa vijana kikiendelea kushika kasi nchini, Serikali imeahidi kuendelea kushirikiana na wadau katika kutengeneza fursa mbalimbali kwa kundi hilo.
Fursa hizo ni zile zitakazowajengea uwezo vijana na kuwapa maarifa yatakayowawezesha kujiajiri na kuajiri wengine.
Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi wakati akizindua mradi wa Vijana Plus unaoendeshwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Save the Children na Tanzania Bora Initiative.
Mradi huo utakaowafikia vijana 700,000 katika kipindi cha miaka mitatu unalenga kuimarisha uwezo wa mashirika ya kiraia yanayoongozwa na vijana na kuwapa uwezo wa kuwa madhubuti katika kuleta na kutekeleza miradi bunifu ya kimaendeleo.
Katambi amesema mradi huo ni hatua muhimu katika kuimarisha na kuwajenga vijana hasa katika kutimiza mipango mikakati ya maendeleo ya nchi.
Amesema sera na mipango ya nchi imeandaliwa ili kuimarisha ajira kwa vijana, kukuza maendeleo ya ujuzi na kuhakikisha kuwa sauti za vijana zinasikika katika uongozi na ngazi mbalimbali za uamuzi.
“Mipango hiyo ni pamoja na utekelezaji wa Sera ya Maendeleo ya Vijana ya mwaka 2007 Toleo la Mwaka 2024, Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDG 2030).
“Nimefurahi pia kusikia katika kipindi chote cha utekelezaji, mradi utazingatia ushirikiano na maofisa maendeleo vijana katika ofisi yangu na mikoa yote ya mradi. Hii itachangia kwa sehemu kubwa uendelevu wa mradi hata baada ya muda wa ufadhili kukamilika,” amesema Katambi.
Mkurugenzi wa Shirika la Save The Children, Angela Kauleni amesema mradi huo unatarajiwa kuwafikia mashirika 40 ya vijana na vijana viongozi 150 kujengewa uwezo kwenye masuala ya uongozi, ubunifu na stadi mbalimbali zinazolenga kuongeza uwezo wao wa kujiajiri na kuajirika pamoja na kushiriki kwenye ngazi mbalimbali za uamuzi.
Amesema mradi huo unalenga kuwawezesha vijana kuwa viongozi bora kwenye taasisi, kampuni, na katika vyombo vya uamuzi wenye uthubutu, na nia njema na nchi na wenye misingi bora ya uongozi na maendeleo.
“Kwenye shirika letu la Save the Children, tunaamini kuwa kila mtoto na kila kijana anastahili kupata fursa ya kufikia malengo yake, kushiriki katika fursa za maendeleo na kuchangia mendeleo katika jamii zinazowazunguka.
“Ni mradi utakaoimarisha uwezo, ujuzi, maarifa na kutoa ruzuku kwa mashirika yanayoongozwa na vijana kwa lengo la kuwawezesha vijana kuwa viongozi wabunifu, wenye uwajibikaji, wenye kujiamini, huru na wenye maono ya mbele ili waweze kufanya uamuzi sahihi utakayowanufaisha wanajamii wa Tanzania,” amesema Angela.