SIMBA imeendelea kufanya umafia kwenye michuano ya kimataifa baada ya kumaliza kazi mapema kabla ya mchezo wao wa kwanza wa hatua ya robo fainali dhidi ya Al Masry ya Misri, huku ikipangua mambo matatu kwa mpigo.
Simba inatarajiwa kuvaana na Al Masry Aprili 2, kwenye mchezo wa kwanza wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, ukitarajiwa kupigwa kwenye Uwanja wa New Suez nchini Misri.
Simba ilifuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ya pili kwa ukubwa Afrika baada ya kufanikiwa kumaliza kinara wa Kundi A ikiwa na pointi 13, huku wapinzani wao wakifuzu baada ya kushika nafasi ya pili kwenye Kundi D wakiwa na pointi tisa.
Mabosi watatu wa Simba zaidi ya siku 14 walikuwa nchini Misri kuhakikisha kuwa wanaweka mambo sawa, ili mastaa wao watakapofika hapo wikiendi ijayo wakute kila kitu kipo sawa.
Hii ni kawaida ya Simba, hata wakati wanaitupa nje Zamalek mwaka 2003, kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika walifanya umafia huo na ndiyo uliwasaidia kupata ushindi huo wa mikwaju ya penalti.
Kitendo hicho kimeifanya Simba ikamilishe mambo matatu kwa mpigo, ambayo yanaweza kuwasaidia kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo muhimu na kuepuka hujuma.
Chanzo cha ndani kutoka ndani ya Simba ambacho kilikuwepo nchini Misri kimesema kuwa tayari wameshapata uwanja mzuri wa mazoezi kwa msaada wa timu moja kubwa nchini Misri (jina kapuni) na utaratibu wote wa kuutumia umeshakamilika.
“Uwanja tumepata karibu kabisa na sehemu ambayo mchezo utafanyika, haikuwa kazi rahisi kwa kuwa kulikuwa na hofu kwa kila mmoja kuwa wakitupa sehemu ya mazoezi itakuwa kama usaliti lakini mabosi wetu walitusaidia kuwasiliana na jamaa wa klabu moja kubwa hapa wakatufanyia utaratibu wa kuupata huo uwanja, hili ni jambo ambalo huwa gumu sana hapa Misri kwa timu ambayo inaweza kufika siku mbili au tatu kabla ya mchezo,” kilisema chanzo.
Chanzo hicho kiliendelea kusema kuwa tayari wameshakamilisha utaratibu wote wa hoteli ambayo timu itafikia na sasa wapo kwenye hatua ya mwisho kabisa ya kufanya malipo, lakini kikubwa ambacho wamekifanya ni kuchukua hoteli nzima.
“Hii hoteli siwezi kuitaja kwa sasa, lakini wewe tambua kuwa tumeshapata aina ya hoteli ambayo tulikuwa tunaitaka na siyo ngeni kwetu kwani tuliwahi kufikia hapa miaka kadhaa iliyopita, jambo pekee ambalo tumefanya tofauti na miaka mingine ni kwamba sasa tumeichukua yote, badala ya kipindi cha nyuma ambacho tulikuwa tukikodi baadhi ya vyumba, kwa sasa tukishatua hapa ndani tutakuwa ni sisi wenyewe hakuna atakayeruhusiwa kuingia wala kutoka nje ya wachezaji, benchi la ufundi na viongozi ambao wataandamana na Simba hapa.”
Hata hivyo, inaelezwa kuwa mabosi hao wa Simba walifanikiwa kutazama mchezo mmoja wa Ligi Kuu ya Misri ambao wapinzani wao walicheza juzi dhidi ya ZED na kumalizika kwa sare ya bao 1-1, ingawa inadaiwa walibadilisha kikosi.
“Tulipata nafasi ya kutazama mchezo wa Kombe la Ligi hapa Misri na mechi ilimalizika kwa sare ya bao 1-1, tulikuwa na mtu mmoja wa benchi la ufundi la kwetu lakini akatueleza kuwa jamaa wamebadilisha sehemu kubwa ya kikosi chao zaidi ya wachezaji saba walikuwa benchi kwa kuwa ulikuwa mchezo wa ligi, lakini tulijifunza vitu vingi ikiwemo aina yao ya kucheza, kushambuliaji, kukaba na hata jinsi ambavyo wanatoka nyuma ya mipira, tunafikiri kocha atapata pa kuanzia,” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, takwimu zinaonyesha kuwa Al Masry wamekuwa na matokeo mchanganyiko kwenye michezo yao huku wakionekana kuruhusu mabao mengi na wastani wao wa kufunga ukiwa hauridhishi.
Kwenye Ligi Kuu ya Misri timu hiyo ipo nafasi ya nne kwenye msimamo ikiwa imecheza michezo 18 imefunga mabao 19 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 11, ikiwa imepoteza mchezo mmoja na kutoka sare saba.
Imefanikiwa kushinda michezo minne nyumbani na minne ugenini, takwimu ambazo ni tofauti na Simba ambayo imecheza michezo 22, imefunga mabao 52 na kuruhusu nane tu, imeshinda michezo 18 imetoka sare mitatu na kupoteza mmoja tu.
Ugenini Simba imeonekana kuwa bora ikishinda mechi 10 na kutoka sare moja, huku ikicheza 11 ugenini, imeshinda nane sare mbili na kupoteza moja, ikiwa inaonekana kuwa bora zaidi kwenye eneo la ulinzi na ushambuliaji.