Stars yapewa refa ‘nuksi’ Morocco

REFA asiye na historia nzuri na timu za Tanzania, Alhadi Allaou Mahamat kutoka Chad, ndiye amepangwa kuchezesha mechi ya ugenini ya Taifa Stars’ dhidi ya Morocco, Jumatano Machi 26, 2025 ya kuwania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2026.

Mchezo huo utachezwa kwenye Uwanja wa Manispaa, mjini Oujda, kuanzia saa 6:30 usiku kwa muda wa Afrika Mashariki.

Kumbukumbu zinaonyesha katika mechi tano ambazo timu za Tanzania zimekutana na refa huyo kwenye mashindano ya kimataifa, ni moja tu ambayo timu ya hapa ilipata ushindi lakini michezo mingine minne zilipoteza.

Timu pekee ya Tanzania iliyowahi kupata ushindi pindi refa huyo aliposhika filimbi ni Yanga iliyoichapa US Monastir kwa mabao 2-0 katika mechi ya hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, Machi 13, 2023.

Lakini hiyo hiyo Yanga ilikutana na kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa CR Belouzdad katika mchezo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa Novemba 24, 2023 ambao mwamuzi wa kati alikuwa ni Mahamat.

Ndiye refa ambaye alichezesha mechi ya hatua ya makundi ya Fainali za Mataifa ya Afrika iliyochezwa Januari 17, 2024 huko Ivory Coast ambayo Taifa Stars ilipoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya Morocco.

Katika mchezo huo, refa Mahamat alitoa kadi nane, moja ikiwa nyekundu kwa kiungo wa Taifa Stars, Novatus Dismas na kadi nyingine saba zikiwa za njano, mbili akiwaonyesha wachezaji wa Morocco na tano kwa wachezaji wa Tanzania.

Hapana shaka Simba ndio timu ambayo haitamani hata kumsikia refa Mahamat kwani mechi zake mbili alizowahi kuichezesha ilipoteza, moja ilifungwa mabao 2-0 na Al Ahly msimu uliopita na nyingine kwa bao 1-0 kisha kufungwa kwa mikwaju ya penalti na Wydad ya Morocco katika msimu wa 2022/2023, mechi zote zikiwa ni za Ligi ya Mabingwa Afrika.

Related Posts