Mwanza. Jumla ya taasisi 98,000 binafsi na za umma zinazokusanya na kuchakata taarifa binafsi za watu zimeshindwa kujisajili ndani ya muda uliopangwa na kujiweka katika hatari ya kupigwa faini na kupelekwa mahakamani.
Hayo yameelezwa leo Jumamosi Machi 22, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC), Dk Emmanuel Mkilia wakati akitoa mafunzo ya kuwajengea uwezo waandishi wa habari jijini Mwanza.
Dk Mkilia amesema jumla ya taasisi 100,000 nchini zinazojihusisha na kukusanya na kuchakata taarifa binafsi za watu zinapaswa kujisajili, hata hivyo ni taasisi 2,000 pekee zilizojisajili hadi Desemba 30, 2024 ambayo ilikuwa tarehe ya mwisho iliyopangwa huku Mkoa wa Mwanza taasisi 20 pekee zikijisajili.
Amesema kujisajili ni takwa la Sheria namba 11 ya mwaka 2022 ya ulinzi wa taarifa binafsi, hivyo PDPC imeongeza muda hadi Aprili 30, 2025 na taasisi ambayo itashindwa kutekeleza agizo hilo itakumbana na hatua kali za kisheria ikiwemo kupigwa faini na kufikishwa mahakamani.
“Baada ya hiyo tarehe, taasisi itakayokuwa inakusanya na kuchakata taarifa binafsi za watu atakuwa anatenda kosa, lengo ni kulinda faragha za watu na kuhakikisha taarifa za watu zinatumika ipasavyo katika kupata huduma,” amesema Dk Mkilia.
Ameongeza: “Natoa wito kwa wakuu wa taasisi zote za Serikali na binafsi wahakikishe kwamba taarifa za taasisi zao zimesajiliwa kwa sababu hili ni takwa la kisheria kwani ni makosa kisheria kama taarifa za mtu ulizonazo unazitumia nje ya matakwa na matumizi yaliyokusudiwa.”
Mkurugenzi huyo amesisitiza kwamba kujisajili kwenye mpango huo kutawezesha mifumo ya Serikali na taasisi binafsi katika kutoa huduma kusomana na kusaidia kufanya usimamizi wa taarifa hizo, huku kasi ndogo ya kujisajili ikichangiwa na uelewa mdogo ambapo wameamua kutoa elimu ukiwemo Mwanza ambao ni taasisi 20 pekee zilizojisajili.
Mkurugenzi wa Usajili na Uzingatiaji, Stephen Wangwe amesema katika kipindi cha mwaka mmoja tangu kuanzishwa kwa taasisi hiyo wamepokea jumla ya malalamiko 60 ya wanancho wakidai taarifa zao kutumika vibaya, huku taasisi za mikopo mitandaoni zikiongoza kulalamikiwa.
“Malalamiko haya ni kutoka kwa wananchi wa kawaida na yaliyo mengi ni yanayohusiana na udhalilishaji hasa taasisi za mikopo chechefu mitandaoni zinatumia taarifa za wateja kusambaza uzushi na uzalilishaji.
“Hili tumejitahidi kulidhibiti tumeshirikiana na BoT (Benki Kuu ya Tanzania) kuzifungia japo bado zipo lakini tunaendelea na ufuatiliaji kuhakikisha walio nyuma ya hizo wanachukuliwa hatua kali za kisheria,” amesema Wangwe.
Wangwe amesema mlinzi wa kwanza wa taarifa za mtu ni yeye mwenyewe kwa kuwa makini na taarifa anazokubali kutoa mitandaoni, huku tume hiyo ikifanya jitihada mbalimbali za kutoa onyo kwa taasisi zinazovunja kanuni katika matumizi ya taarifa binafsi za watu.
Innocent Mungy, Mkuu wa Uhusiano kwa Umma na Mawasiliano amesema taarifa binafsi zinalindwa ili zisitumike vibaya, zisifutwe ama kuharibiwa na zinatakiwa zidhibitiwe kwa heshima na kwa faragha.
Ametaja madhara ya taarifa hizo kwenda sehemu ambayo hazijakusudiwa kuwa ni kuibiwa utambulisho wa kifedha, kuharibu haki zako, kuumizwa kisaikolojia na kukosa usimamizi wa taarifa zako.