Tanzania mbioni kuiuzia umeme kampuni ya Zambia

Dar es Salaam. Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) lipo katika mchakato wa kuuza umeme kwa kampuni ya Kanona ya nchini Zambia.

Tanesco imethibitisha uwepo wa mazungumzo hayo katika taarifa yake iliyotolewa leo Jumamosi Machi 22, 2025, ikisema mazungumzo hayo yalikuwa katika hatua ya awali.

Meneja wa maendeleo ya biashara wa Tanesco, Magoti Mtani, amesema ni matarajio ya Tanesco kuwa mafanikio ya biashara hiyo yataongeza na kuimarisha mapato ili kuhakikisha utendaji kazi unafanyika.

Kwa sasa, Tanzania inazalisha Megawati 3,431 za umeme, ambapo asilimia 58 inazalishwa kwa maji, asilimia 35 ya gesi na asilimia 7 kutoka vyanzo vingine vinavyoweza kurejeshwa.

Mtani amesema lengo ni kuongeza uwezo huu kwa Megawati 2,463, kwa kutumia nishati ya jua, upepo, jotoardhi na vyanzo vingine vinavyoweza kutumika tena ifikapo 2030.

“Shirika limefanya majadiliano na Kampuni ya Umeme ya Kanona ya Zambia, lengo likiwa ni kuangalia namna makampuni hayo yanavyoweza kujihusisha na biashara ya umeme katika ukanda wa Kusini, biashara hii pia inatarajiwa kuenea hadi nchi jirani, na sisi kama Tanesco tunatarajia kuimarisha uwezo wetu wa kifedha,” amesema.

Pia, ametoa shukurani kwa uongozi wa awamu ya sita w kwa kutekeleza miradi ya kimkakati ya maendeleo hususan katika sekta ya umeme.

Amesema Serikali imekuwa ikigharamia shughuli za Tanesco ili kuhakikisha miradi hiyo ya kimkakati inakamilika kwa wakati.

Wakati huo huo, Mkuu wa Idara ya Biashara katika Kampuni ya Umeme ya Kanona, Nsofwa Sikanika, amesema kuwa mkutano huo wa majadiliano ya ushirikiano wa kibiashara ni hatua ya awali ya kukamilisha makubaliano ya biashara ya umeme, ambayo yanatarajiwa kusainiwa hivi karibuni.

Kukamilika kwa makubaliano haya kutaruhusu biashara kuanza rasmi, kuimarisha upatikanaji wa huduma za umeme na kuchangia ukuaji wa uchumi katika nchi za Afrika.

Tanzania ni mwanachama wa masoko ya kanda ya umeme ya Eastern Africa Power Pool (EAPP) na Southern African Power Pool (SAPP), ambayo yatainufaisha Tanzania kwa kuiruhusu kununua na kuuza umeme na nchi nyingine za Afrika.

Related Posts