Mwanza. Wajawazito wametakiwa kushiriki mazoezi na mbio fupi ikielezwa kwamba yanasaidia kuimarisha mwili, mzunguko wa damu na kuzuia magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo presha, kisukari na kupunguza uzito.
Ushauri huo umetolewa Machi 21, 2025 na Mratibu wa Huduma ya Afya ya Uzazi katika Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Bertha Yohana, akieleza kuwa kutokana na umuhimu wa wajawazito kufanya mazoezi, watashirikishwa kwenye mashindano ya mbio ya utalii Kanda ya Ziwa (Lake Zone International Tourism Marathon) yatakayofanyika Juni 27 hadi 29, 2025 katika Uwanja wa Nyamagana jijini humo.
Amesema licha ya makundi hayo kuruhusiwa kushiriki mbio hizo, wajawazito wanapaswa kuchukua tahadhari kwa kuhakikisha wanafanya mazoezi mepesi yakiwemo ya kutembea taratibu kwa dakika 20 mpaka 30, kutembea sehemu salama, isiyo na mashimo ama sehemu inayoweza kumsabababishia madhara yoyote.
“Kwa hiyo, mazoezi ya kutembea yanaweza kumsaidia mjamzito kupata usingizi mzuri kwa sababu tunatamani aweze kupumzika na kulala, hivyo, mazoezi haya yatakuwa ni chachu kwa wajawazito wote wasilale tu, tunashauri wafanye mazoezi mepesi kwa ajili ya afya zao,” amesema Bertha na kuongeza:
“Sisi kama wataalamu wa afya, hii ni fursa kubwa sana kwa sababu itaweza kusaidia kutoa elimu kwa wajawazito na wanapopata hizi elimu za afya ya uzazi zitasaidia kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga.”
Amewashauri wajawazito kujitengenezea utaratibu wa kufanya mazoezi katika safari yao ya ujauzito ili kuweka mwili vizuri na kudumisha afya zao, kwani lengo ni kuhakikisha mjamzito tangu siku amejitambua ni mjamzito mpaka siku anajifungua hadi kumaliza 40 ya uzazi apate uzazi salama.
Fikira Japhari, mjamzito na mkazi wa jijini Mwanza anayejiandaa kushiriki mbio hizo, amesema kufanya mazoezi kutamsaidia kuweka mwili wake vizuri huku akiwashauri wenzake kufanya hivyo kwani uvivu wa mazoezi umesababisha wajawazito wengi kujifungua kwa njia ya upasuaji.
“Nimependa kipengele cha wajawazito kwa sababu ukiwa haufanyi mazoezi, nyonga zinajifunga, ndiyo maana oparesheni zimekuwa nyingi siku hizi tofauti na zamani, kwa hiyo nitashiriki kufanya mazoezi hayo ili kunisaidia kuweka mwili vizuri,” amesema Fikira.
Naye, Mwenyekiti mstaafu wa Chama cha Watu wenye Ualbino Wilaya ya Nyamagana, Meckzedeck Mungule amewashauri wajawazito kushiriki mbio hizo kwani mjamzito anayefanya mazoezi hapati changamoto nyingi wakati wa kujifungua kwa kuwa mishipa inakuwa tayari kuachia, huku akipongeza waandaaji kwa kuwajumuisha watu wenye ulemavu.
“Mazoezi kwa ujumla wake ni afya kwa ngozi na mwili wote, magonjwa mengi sana yanajitokeza kwa sababu watu hawafanyi mazoezi, mazoezi siyo kukimbia tu, kuna kutembea na jogging (mbio za kujifurahisha),” amesema Mungule.
Mwandaaji wa mbio hizo zinazoshirikisha kundi la wajawazito, wenye ulemavu na watoto (kilometa 2.5), hisani kwa viongozi (kilometa 5) na kilometa 10 na 21 kwa ajili ya ushindani, Mohamed Hatibu amesema lengo ni kutangaza vivutio vya utalii kwa Kanda ya Ziwa na kukuza uchumi wa wananchi kupitia matukio ya kiutamaduni.
“Tutashirikisha watoto, wanafunzi, wenye ulemavu, akina mama wajawazito, wananchi mchanganyiko na vikundi vya wafanyaji mazoezi ambapo zaidi ya watu 2,000 tunatarajia watashiriki kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa na Tanzania kwa ujumla. Tunawakaribisha Watanzania wote tushirikiane katika kuleta mafanikio ya tamasha hili,” amesema Hatibu.