Dar es Salaam. Serikali imewaita kazini walimu wapya 189 ambao walifanyiwa usaili na baadhi waliopo katika kanzidata.
Walimu hao wameitwa kazini ikiwa ni siku tisa tangu Serikali iwaite kazini walimu wengine wapya 319 wa fani mbalimbali, ambapo halmashauri saba zilinufaika na ingizo hilo jipya.
Tangazo hilo limetolewa jana Ijumaa Machi 21, 2025 na Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma likisema: “Katibu anapenda kuwataarifu waombaji kazi wa nafasi mbalimbali waliofanya usaili kati ya Januari 5, 2025 na Februari 24, 2025 kuwa matokeo ya waombaji kazi waliofaulu usaili huo ni kama yalivyoorodheshwa katika tangazo hili.”
Taarifa hiyo imeeleza pia orodha ya majina hayo pia inajumuisha baadhi ya wasailiwa waliokuwa kwenye kanzidata kwa kada mbalimbali, ambao wamepangiwa vituo vya kazi baada ya nafasi kupatikana.
“Waombaji waliofaulu usaili wanatakiwa kuchukua barua za kupangiwa kituo cha kazi katika Ofisi za Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, zilizopo katika Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), kwenye Majengo ya Dk Asha Rose Migiro, Masjala ya wazi ndani ya siku saba kutoka tarehe ya tangazo hili,” imeeleza taarifa hiyo ikifafanua kuwa barua ambazo hazitachukuliwa na wahusika zitatumwa kupitia anuani zao za Posta
Katika awamu hii jumla ya halmashauri tano zimepata mgawo wa ingizo hilo jipya ambazo ni: Manispaa ya Shinyanga, Wilaya ya Rorya, Manispaa ya Kahama, Wilaya ya Nyang’hwale na Wilaya ya Bukombe.