Wanawake wa ADC wajitosa kusaka mwarobaini mikopo ya ‘kausha damu’

Mwanza. Wakati mikopo umiza hususan ‘kausha damu’ ikitajwa kuwa kikwazo cha wanawake kufikia malengo yao kiuchumi, Jumuiya ya Wanawake wa chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) imejitosa kusaka mwarobaini wa changamoto hiyo.

Akizungumza leo Jumamosi Machi 22, 2025, walipofanya ziara katika ofisi ya Mwananchi Communications Limited (MCL), Kanda ya Ziwa, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wanawake wa ADC Taifa, Ester John amesema chama hicho kimebaini wanawake wanajiingiza kwenye mikopo umiza kutokana na kukosa elimu ya matumizi sahihi ya fedha.

Amesema ili kujenga uelewa huo miongoni mwa jamii hususan wanawake, ADC imeitisha kongamano litakalowakutanisha wanawake wa Kanda ya Ziwa na wataalamu wa uchumi na fedha ambalo litafanyika Jumanne Machi 25, 2025 wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Ester amesema mbali na kukwamisha uchumi wao, mikopo umiza huchochea vitendo vya ukatili, migogoro kwenye uhusiano (ndoa) na kusababisha wakopaji kutokomea na kutelekeza familia wakikwepa marejesho yanayoambatana na masharti magumu.

“Tumeamua kuwaita wataalamu wa uchumi na fedha waje watupige msasa na kutupatia mbinu za kukopa na kutumia mkopo kwenye mambo yenye tija. Pia, watatuelekeza biashara ambazo tukifanya tutaweza kurejesha mkopo,” amesema Ester.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa ADC Mkoa wa Mwanza, Christina Christopher amesema amewahi kushuhudia wanawake wakitelekeza familia zao na kutokomea kusikojulikana baada ya kushindwa kurejesha mkopo waliochukua ambao umeambatana na masharti magumu.

“Utakuta mwanamke ana jukumu kubwa la kulea familia ambayo wakati mwingine imetelekezwa na baba (mumewe), sasa akikosa msaada anaamua kutafuta njia rahisi ya kupata fedha ambayo ni mkopo wa haraka, lakini wenye masharti magumu,” amesema.

Christina amesema mwanamke wa aina hiyo, bila kujua, hujikuta akitumia fedha aliyopewa kwa masharti ikiwemo riba kubwa kuhudumia familia badala ya kuizalisha ili aweze kulipa deni analodaiwa kwa sababu ya kukosa elimu.

“Hivyo, namna pekee ya kuwajengea uelewa wanawake wenzetu na jamii ni kuwakutanisha na wataalamu wa fedha na uchumi ambao watatupatia ujuzi wa uelewa wa mkopo isiyo na madhara na biashara unayoweza kufungua ukapata faida na kurejesha mkopo,” amesema Christina.

Kauli ya Christina inaungwa mkono na Halima Idd ambaye ni mwanachama wa ADC ambaye amedokeza kuwa hata mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri nchini, vikundi vingi (bila kutaja idadi) vimeshindwa kurejesha ipasavyo kwa kukosa elimu sahihi ya matumizi yake.

“Wengine wakipokea tu fedha wanaenda kufanya sherehe, kutumia kwenye starehe, kula vizuri na kwenda saluni kutengeneza mionekano bila kujua kuwa wanapaswa kuurejesha. Matokeo yake wakishtuka fedha imekaribia kuisha na isiyoweza kufanya biashara waliyoiombea,” amesema.

Halima amewaomba wanawake wa Mkoa wa Mwanza na mikoa jirani kujitokeza kwa wingi kushiriki kongamano hilo ili kujengewa uwezo na mbinu za kutumia fedha kujikwamua kiuchumi.

Mbali na kujengewa elimu ya fedha, kongamano hilo linalofanyika Jumanne Machi 25, 2025, katika ukumbi wa ‘The Breeze’ uliopo Kiseke wilayani Ilemela mkoani humo, litahusisha uundaji wa chama cha kuwezeshana kiuchumi kitakachotumika kuweka akiba na kukopeshana ili kuwaepusha kujiingiza kuchukua mikopo yenye riba kubwa.

Mgeni rasmi katika kongamano hilo anatarajiwa kuwa Mwenyekiti wa ADC Taifa, Shaban Itutu na viongozi wa Serikali na vyama vingine vya siasa nchini watashiriki.

Related Posts