Unguja. Changamoto ya gharama inayowakabili wazazi ambao watoto wao wana matatizo ya moyo, huenda imepata ufumbuzi baada ya kampuni ya simu ya Vodacom kulipia asilimia 30 ya gharama za matibabu.
Kwa kawaida visiwani hapa watoto wenye matatizo ya moyo asilimia 70 ya gharama za matibabu hutolewa na Serikali huku asilimia 30 ikitolewa na wazazi wa mtoto husika hivyo kwa hatua iliyochukuliwa na Vodacom sasa itakuwa ni bure.
Pamoja na utaratibu uliokuwepo wa Serikali kuchangia sehemu kubwa ya gharama za matibabu, bado asilimia 80 ya wazazi hawamudu gharama ya asilimia 30 ambapo kiwango cha gharama za upasuaji kwa mtoto mmoja ni kati ya Sh4 milioni hadi Sh15 milioni.
Akizungumza katika futari iliyoandaliwa na Vodacom kuwafutarisha wadau na watoto wanaoishi katika mazingira magumu Zanzibar usiku wa kuamkia leo Machi 22, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Philip Besiimire amesema wameguswa na namna ambavyo watoto na wazazi wao wanavyopitia wakati mgumu hivyo wakaamua kuja na mpango huo.
“Mpango huu wa miaka mitatu ambapo kila mwaka tutahudumia watoto 50 nchi nzima, kwa hiyo kwa miaka mitatu jumla ya watoto 150 tutawalipia asilimia 30 ya gharama,” amesema.
Katika mpango huo ambao unaanza mara moja, amesema tayari wameshapokea watoto sita ambao wapo tayari kufanyiwa upasuaji na wote wanatoka Zanzibar.
Mbali na hilo pia wataleta wataalamu wa kufanya uchunguzi ili kusaidia kuwagundua watoto wenye matatizo hayo ambao hawajajitokeza kwenye hospitali ili waanzishiwe matibabu.
Hata hivyo, mpango wa kulipia watoto hao, utahusu watoto wale watakaokuwa wanatibiwa katika taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) na sio wanaokwenda kutibiwa nje ya nchi.
Akizungumza katika futari hiyo, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ambaye alikuwa mgeni rasmi, amesema mpango huo ni wa kupongeza kwani eneo hilo ni moja ya matatizo ambayo yanawatesa wazazi licha ya serikali kuchukua jukumu la kugharamia asilimia 70 ya matibabu.
“Ni sahihi kabisa kwamba Vodacom watakuwa wameokoa maisha ya watoto wengi ambao vinginevyo wasingemudu kulipia gharama zinazotakiwa,” amesema Dk Mwinyi
Amesema serikali ina jukumu kuhakikisha kwamba wananchi wake wanaishi katika mazingira mazuri lakini wanatambua kwamba hawawezi kufanya kila jambo kwa hiyo inapotokea wakapata wadau kama hao wakasaidia katika nyanja mbalimbali, yote ni faida kwa serikali.
“Kwa hiyo nachukua fursa hii kuishukuru Vodacom kuwasaidia wale yatima na wanaoishi katika mazingira magumu kama tulivyoelezwa hapa,” amesema
Mkurugenzi wa Tehama Vodacom, Athumani Mlinga amesema tangu Ramadhani ianze tayari Vodacom wamefuturisha watu zaidi ya 6,178 wakiwemo yatima zaidi ya 780 na wajane zaidi ya 160 katika mikoa ya Kigoma, Dar es Salaam, Ruvuma, Mjini Magharibi, Chakechake, Morogoro na Tanga.
“Tunaamini kusaidia wenye hali ya chini au duni ni moja kati ya kuweka na kushirikiana na jamii husika huku wakilenga kusaidia jamii ya watu wasiojiweza zaidi.
Watoto wawili kati ya 100 huzaliwa na tatizo la moyo nchini kila mwaka, huku wataalamu wakibainisha kuwa wengi hawagunduliki mapema na hufariki wakitibiwa magonjwa mengine ikiwemo kukosa pumzi kifua kikuu na nimeona. Watoto wengi huzalia na hitilafu ya moyo na kinachosumbua ni tundu kwenye moyo.