MECHI za kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026 kwa Ukanda wa Afrika zinatarajiwa kuendelea leo Jumapili na nyota wawili wanaocheza Ligi Kuu Bara katika timu za Yanga na Singida Black Stars, watakuwa wakilitumikia taifa lao la Kenya.
Nyota hao ni kiungo wa Yanga, Duke Abuya na mshambuliaji wa Singida Black Stars, Elvis Rupia ambao walishuhudia mchezo wa kwanza nyumbani wakitoka sare ya mabao 3-3 dhidi ya Gambia anayoitumikia Gibril Sillah wa Azam.
Katika mchezo huo dhidi ya Gambia, Abuya aliingia dakika ya 67 kuchukua nafasi ya Richard Odada, wakati Rupia akiishia benchi walipokuwa ugenini.
Mchezo wa leo ambao Kenya itakuwa nyumbani, itaikaribisha Gabon ukiwa ni wa Kundi F utakaochezwa Uwanja wa Nyayo uliopo Nairobi na wenyeji hao watakuwa na kazi kubwa ya kufanya kupata ushindi ili kusogea nafasi za juu.
Msimamo wa Kundi F unaonyesha Ivory Coast inaongoza ikiwa na pointi 13 ikifuatiwa na Gabon (12), Burundi (7), Kenya (6), Gambia (4) na Seychelles ikiburuza mkia haina pointi baada ya timu zote kucheza mechi tano.
Kocha wa Kenya, Benni McCarthy raia wa Afrika Kusini, huu utakuwa mchezo wake wa pili tangu akabidhiwe mikoba ya kukinoa kikosi hicho.
Wakati Abuya na Rupia wakiwa na Kenya, Banele Sikhondze atakuwa na kikosi cha Eswatini kitakachoikaribisha Mauritius katika mchezo wa Kundi D.
Sikhondze ni beki wa Tabora United ambaye mchezo uliopita dhidi ya Cameroon alianza kikosi cha kwanza na kucheza kwa dakika 84 wakati timu hizo zikitoka 0-0.
Katika Kundi D, Eswatini inaburuza mkia ikiwa na pointi moja iliyoipata katika suluhu hiyo dhidi ya Cameroon huku ikiwa imecheza mechi tano. Vinara wa kundi hilo ni Cape Verde wenye pointi 10, wakifuatiwa na Cameroon (9), Libya (8), Angola (7) na Mauritius (4).