Dar es Salaam. Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Wilbrod Slaa amewaomba radhi wanachama wa chama hicho huku akishukuru kurejeshewa uanachama kuendeleza harakati za kudai mabadiliko.
Dk Slaa ametoa kauli hiyo leo Machi 23, 2025 kwenye mkutano wa uzinduzi wa kampeni ya ‘No reforms, no election’ unaofanyika Viwanja vya Ruanda Nzovwe jijini Mbeya.
Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi wote wa juu wa Chadema wakiongozwa na mwenyekiti wao, Tundu Lissu.
Akizungumza baada ya kutangazwa kurejeshwa tena Chadema, Dk Slaa amesema kama ni mfarakano uliotokea baina yake na chama kwa sasa umekwisha rasmi na ameomba kurejea upya kuanza mapambano kudai mabadiliko.
“Niombe msamaha na radhi kwa wanachama, mfarakano uliotokea kwa sasa umeisha rasmi nakuja kuanza upya mapambano. Niko tayari kwa mabadiliko ambayo wengine hawataki,” amesema Dk Slaa ambaye amewahi kuwa mbunge wa Karatu kupitia chama hicho.
Mwaka 2015 wakati Chadema ikijiandaa na uchaguzi mkuu, Dk Slaa alitangaza kuondoka ndani ya chama hicho na baadaye kutimkia nje ya nchi na baadaye kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Canada.
Akimkaribisha kabla ya kumkabidhi kitambaa cha chama, Lissu amesema Dk Slaa amekuwa kiongozi wa muda mrefu ndani ya Chadema na kwamba, amekuwa na mafanikio makubwa katika harakati za kuendesha chama.
Amesema Dk Slaa ndiye alimkabidhi Lissu kadi ya chama hicho Julai, 2004 na katika uongozi wake alifanikiwa kwa kiasi kikubwa hasa wakati akiiongoza ushirikiano wa vyama vya upinzani, maarufu Ukawa. Katika kipindi hicho, Lissu amesema idadi ya wabunge kutoka vyama vya upinzani ilipanda hadi kufikia 117 bungeni.
“Sasa kama mtu kaja na kakiri kukosea akaomba msamaha iweje tushindwe kumsamehe, Katiba yetu iko wazi na bahati nzuri Dk Slaa hakufukuzwa, tulitofautiana naye akaondoka mwenyewe na leo amerejea mwenyewe.
“Kama mtu kafukuzwa katiba inaelekeza aombe upya kwa Kamati Kuu iliyomfukuza na hadi sasa wapo wengine wawili tuliowatimua wamewasilisha barua kuomba kurejea,” amesema Lissu.
Awali akitoa salamu, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Bara, Aman Gorugwa amesema Dk Slaa walitibuana naye na kabla ya kumpokea upya wamejiridhisha kuanzia uhalali wa kadi yake.
“Tumekaa naye kwanza tukasema kwakuwa aliondoka mbele ya vyombo vya habari, arudi mbele ya vyombo vya habari na wananchi wakiona,” amesema Gorugwa.
Chadema imeanza ziara ya kampeni yake ya ‘No reforms, no election’ leo Machi 23, 2025 katika Kanda ya Nyasa (Njombe, Iringa, Mbeya, Songwe na Rukwa).
Baada ya uzinduzi huo leo, kampeni itakwenda mikoa ya Kanda ya Kusini yenye mikoa ya Ruvuma, Mtwara na Lindi. Aprili 4 hadi 10, 2025 watakwenda Kanda ya Kusini kisha Kanda ya Kati (Dodoma, Singida na Morogoro) kuanzia Aprili 12 hadi 13, 2025 na kuhitimisha Kanda ya Magharibi (Tabora, Katavi na Kigoma) kuanzia Aprili 14 hadi 17, 2025.
Baada ya mapumziko ya Pasaka, ziara hiyo itaanza upya Kanda ya Victoria (Geita, Mwanza na Kagera) kuanzia Aprili 22 hadi 24, 2025. Kanda ya Serengeti (Mara, Shinyanga na Simiyu) Aprili 26 hadi 28,2025 wakati Kanda ya Kaskazini (Tanga Kilimanjaro, Arusha na Manyara), itakuwa Aprili 29 hadi Mei 3, 2025.
Baada ya hapo, ziara hiyo itahamia kisiwani Pemba Mei 4, 2025 kisha Unguja Mei 5, 2025 na kumalizia Kanda ya Pwani inayohusisha mikoa ya Dar es Salaam na Pwani kati ya Mei 7 hadi 10, 2025.

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu akipokewa na viongozi na wafuasi wa chama hicho alipowasili kwenye Viwanja vya Ruanda Nzovwe jijini Mbeya kuzindua kampeni ya ‘No reforms, no election’ leo Jumapili, Machi 23, 2025.
Lissu amewasili kwenye viwanja hivyo akiwa ameongoza na aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Wilbrod Slaa. Pia, alikuwepo Makamu Mwenyekiti wa Chadema-Bara, John Heche ambao walipokewa na Mwenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’.