Dar es Salaam. Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imeongeza siku mbili (Machi 24 na 25) za uboreshaji wa daftari la mpigakura kwa Mkoa wa Dar es Salaam kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi.
Taarifa ya INEC imetolewa leo Machi 23, 2025 na Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji Jacobs Mwambegele ikiwa ni siku moja tangu Mwananchi iripoti wingi wa watu vituoni na malalamiko ya baadhi kushindwa kuboresha taarifa zao.
Uboreshaji wa taarifa huo awali mkoani Dar es Salaam ulianza Machi 17 na ulitakiwa kumalizika leo Jumapili Machi 23, 2025.
“Kama mnavyofahamu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi inaendelea na hatua ya uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura kwa Mkoa wa Dar es Salaam, hatua ambayo kwa mujibu wa ratiba ilianza Machi 17, 2025 na ilitarajiwa kukamilika Machi 23, 2025.
“Kutokana na mwitiko mkubwa Tume ilichukua hatua za kuongeza mashine za BVR Kits pamoja na watumishi katika maeneo yote yaliyoonekana kuwa na watu wengi na hatua hii imewezesha shughuli hiyo kuendelea kwa utulivu katika maeneo yote. Hatua hiyo imewezesha kuongeza kasi ya kuwahudumia wananchi na kupunguza kwa kiasi kikubwa misongamano kwenye baadhi ya maeneo,”imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa: “Licha ya hatua zilizochukuliwa na Tume, bado katika maeneo kadhaa kuna mwitikio mkubwa wa wananchi. Hivyo basi, napenda kuwatangazia wananchi wote wa mkoa wa Dar es Salaam kuwa Tume imeongeza siku mbili za uboreshaji wa daftari kwa Machi 24 na 25, 2025.”
Malalamiko ya wananchi waliojitokeza kwenye vituo mbalimbali kujiandikisha wameiambia Mwananchi kero kubwa ni uchache wa vifaa pamoja na watumishi.
Changamoto hizo mbili zinawafanya wananchi hao kukaa muda mrefu vituoni wakisubiri kujiandikisha huku muda wa kujiandikisha uliotangazwa awali mwisho ukiwa ni leo Machi 23, 2025.
Mtaa wa Tabata Kisiwani mkoa wa Dar es Salaam James Julias aliiambia Mwananchi jana alifika kituoni kujiandikisha lakini alishindwa kutokana na wingi wa watu.
“Mashine ilikuwa moja na watu walikuwa wengi, unapewa namba hadi inafika 800 hii ni changamoto, ni kama hawakujipanga waijua wananchi ni wachache na hata muda waliouweka ni mdogo sana kwa watu waliojitokeza,”amesema.
Kero hiyo haitofautiani na malalamiko ya MC Weki aliyoitoa kupitia mtandao wake wa Instargram akisema “nimekaa foleni siku mbili ya Ijumaa na Jumamosil lakini sijafanikiwa kujiandikisha ,
“Watu ni wengi hasa wale makundi muhimu, wazee, wajawazito, wanaonyonyesha na wagonjwa. “Tunaomba hatua hii liongezwe muda au vituo na watoa huduma waongezwe,”alisema.
Naye Mponeja Simbe mkazi wa Dar es Salaam aliandika kupitia mtandao wake wa Istagram kuwa ni muhimu kuongeza siku tatu na kuendelea kwani idadi ya watu ni kubwa na siku hazitoshi.
Hata hivyo wito wa Tume kuongeza muda uliambatana na onyo kwa wananchi kutokujiandikisha zaidi ya mara moja kwani ni kosa na mtu akibainika anaweza kufungwa, kutozwa faini au vyote viwili kufungwa jela na kutozwa faini.
Katika uboreshaji wa daftari hilo jijini Dar es Salaam, wapigakura wapya 643,420 wanatarajiwa kuandikishwa.