Unguja. Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman amesema kuna haja Serikali kuongeza kasi ya utoaji elimu ya magonjwa yasiyoambukiza kwa kuwa yanaonekana kuongezeka kwa kasi.
Othman amesema hayo alipokuwa ziarani Pemba na Unguja kuangalia wagonjwa, wazee na watu wasiojiweza.
Akizungumza baada ya kukamilisha ziara Mkoa wa Mjini Magharibi leo Jumapili Machi 23, 2025, Othman ambaye pia ni Mwenyekiti Taifa wa wa Chama cha ACT- Wazalendo, amesema katika maeneo yote aliyopita, amebaini watu wengi wanasumbuliwa na magonjwa hayo.
“Katika ziara hizi, tumegundua kwamba, asilimia kubwa maradhi yanayowasibu watu wengi ni yale yasiyokuwa ya kuambukiza; hili linaweza kusababishwa na vyakula tunavyotumia, hivyo elimu juu ya vyakula inahitajika ili kupunguza ongezeko la matatizo haya,” amesema Othman.

Desemba 2024, Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Pharm Access, ilizindua kampeni maalumu ya kuhamasisha jamii kufanya mazoezi mara kwa mara ili kupambana na magonjwa hayo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Afya, takwimu zinaonyesha ufanyaji wa mazoezi na kuishughulisha miili umeshuka kutoka asilimia 52 mwaka 2011 hadi kufikia asilimia 33 mwaka 2013, ugonjwa wa kisukari umepanda kutoka asilimia 3.8 mwaka 2011 hadi asilimia 7.5 mwaka 2023.
Kwa upande wa shinikizo la damu, limependa kutoka asilimia 33 mwaka 2011 hadi asilimia 43 mwaka 2023, uzito na unene kupitiliza vimepanda kufikia asilimia 43.4 kutoka asilimia 36.6 huku matumizi ya tumbaku yakiongezeka kutoka asilimia 7.3 hadi kufikia asilimia 10.3.
Katika hatua nyingine, Othman amesema wajibu wa kuongoza ni kuwafikia wanyonge, kuwasikiliza na kutatua changamoto zao bila kujali itikadi zao za vyama wala dini.
Amesema wajibu huo ni jambo lililotokana za mwenendo na tamaduni za wazee wa visiwa hivyo.
“Tunapaswa kuwa na imani zaidi ili kuifanya jamii inayotuzunguka kuishi kwa umoja, upendo, amani na ushirikiano,” amesema kiongozi huyo.
Amewataka viongozi wengine kuisaidia jamii kutokana na wingi wa wahitaji.
Baadhi ya wagonjwa akiwamo Safia Abdallah Othman amesema ni faraja kwao kutembelewa na kiongozi mkuu wa nchi.
“Hii ni faraja tosha tunapoona viongozi wakuu wanakuja kututembelea, tunawaombea mema inshallah Mwenyezi Mungu awape maisha marefu,” amesema Jina Haji.
Mwenyekiti wa ACT- Wazalendo Mkoa wa Magharibi B, Unguja, Ali Juma Ali ameshukuru ujio wa Othman katika maeneo yao akisema amesema ni faraja kubwa na ishara njema ya ushirikiano wa dhati kutoka kwa viongozi wa juu, kushuka chini kuonana na kuifariji jamii.
“Hiki unachofanya siyo faraja kwa wagonjwa pekee, bali umetuonyesha hasa athari njema za kiongozi anayejali utu na watu wake,” amesema Ali.