Kipa Azam amgomea Sadio Mane

KIPA wa Azam FC, Mohamed Mustafa alikuwa langoni kulitumikia taifa lake la Sudan na kuambulia pointi moja katika mchezo uliomalizika kwa matokeo ya 0-0 dhidi ya Senegal iliyokuwa ikiongozwa na Sadio Mane anayecheza Al Nassr ya Saudi Arabia.

Mchezo huo wa Kundi B kuwania kufuzu Kombe la Dunia 2026, ulichezwa juzi Jumamosi kwenye Uwanja wa Martyrs of Benina uliopo Benghazi nchini Libya huku Sudan ikiwa mwenyeji.

Mbali na Mane, Senegal iliundwa na nyota wengine wanaocheza soka barani Ulaya akiwemo Ismaila Sarr (Crystal Palace, England), Lamine Camara (Monaco, Ufaransa), Pape Matar Sarr (Tottenham, England), Boulaye Dia (Lazio, Italia) na Assane Diao (Como, Italia).

Licha ya Senegal kuundwa na safu kali ya washambuliaji kama Mane, lakini ilishindwa kumfunga kipa huyo namba moja wa Azam FC na Sudan.

Senegal ambao ni mabingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2021, walikaribia kupata bao mapema dakika ya kwanza baada ya makosa ya kipa wa Sudan, Mohamed Mustafa, lakini alifanikiwa kurekebisha hali hiyo kwa haraka na kukaa imara. Matokeo hayo yanaiweka Sudan kileleni mwa Kundi B ikiwa na pointi 11 kwenye mechi tano ikifuatiwa na DR Congo (pointi 10), Senegal (pt9), Togo (pt.4), Mauritania na Sudan Kusini zikiwa na pointi mbili kila moja.

Wakati Mustafa akimgomea Mane, kipa wa Simba na timu ya taifa ya Guinea, Moussa Pinpin Camara, juzi hakuwa sehemu ya mchezo wao dhidi ya Somalia ambao nao ulimalizika kwa timu hizo kutofungana ukiwa ni wa Kundi G.

Baada ya mchezo huo, Guinea inatarajiwa kukutana na Uganda katika mchezo unaofuata utakaochezwa kesho Jumanne kwenye Uwanja wa Mandela nchini Uganda ambapo Camara atakutana na kiungo wa Yanga, Khalid Aucho na mshambuliaji Steven Mukwala anayecheza naye Simba.

Related Posts