KOCHA wa Trident FC, Arnold Malisawa amemtabiria mshambuliaji wa Kitanzania, kinda Mourice Sichone atakuja kuwa hatari miaka ya mbele akimtaka aongeze bidii na nidhamu tu.
Kinda huyo (18) alisajiliwa msimu huu kwenye dirisha dogo akitokea Mpulungu Harbour FC ya nchini Zambia alikocheza mechi 12 na kufunga mabao manne na asisti tano.
Akizungumza na Mwanaspoti, Malisawa alisema ni mmoja kati ya washambuliaji hatari ambao watakuja kuwa na msaada kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars.
Aliongeza kuwa licha ya namba zake uwanjani kutisha anatamani kumuona bora zaidi hasa anapokuwa na mpira kuwa na umakini, akimtabiria anaweza kufunga mabao mengi msimu huu.
“Ni mchezaji mzuri sana, nimekuwa nikimpa moyo aendelee kupambana na ndio maana naendelea kumpa nafasi, naamini bado ni mdogo ana mambo mengi ya kufanya,” aliongeza.
“Vijana wadogo wana vitu vingi hasa Sichone ana nguvu, anakosa utulivu kidogo, kama kocha naendelea kuzungumza nae na kumuelekeza kuwa na nidhamu ndani na nje ya uwanja.”
Hadi sasa Sichone amecheza mechi nne na kufunga mabao matatu na asisti nne akianza kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo inayopambana kupanda daraja msimu ujao.