YANGA imeweka ngumu ikisema haitatia timu kwenye mchezo namba 184 dhidi ya Simba ambao uliota mbawa, baada ya kushindwa kuchezwa Machi 8, 2025 pale Uwanja wa Benjamin Mkapa, lakini mabosi wa juu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wanasema mechi itapangwa na watacheza.
Mpaka sasa mvutano huo haujapata mwafaka wa kipi kitamaliza sakata hilo au upande upi utaamua kushusha silaha chini na kukubaliana na hoja za mwingine huku kukiwa na mambo sita yaliyoshikilia hatma hiyo.
Ukiitazama Yanga, utagundua msimamo wa kwamba haitapeleka timu unatoka kwa mashabiki na wanachama wao, ambao tangu Machi 9 wamekuwa wakitoa kauli uongozi wao hautakiwi kupeleka timu uwanjani kwa namna yoyote endapo mchezo huo utapangiwa tarehe mpya.

Msimamo huo umewasukuma viongozi wa juu wa klabu hiyo, nao kulazimika kusimama upande wa wanachama na mashabiki wao, kwa kile kinachoonekana kutotaka kuonekana wasaliti hasa wakiaminishwa na wadau wa Sheria ambao ni wanazi wa Yanga kwamba klabu yao iko salama kwenye maamuzi hayo kwa kuwa hawakuvunja sheria wala kanuni yoyote.
Yanga imeshafungua kesi Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi ya Michezo (CAS) juu ya kupinga maamuzi ya Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) kuahirisha mechi hiyo huku ikitaka kupewa ushindi wa pointi tatu kufuatia wao kupeleka timu.
Nje ya maamuzi yatakayotoka CAS, ni vigumu kwa Yanga kupeleka timu uwanjani ambapo hatma ya msimamo huo itatokana na maamuzi ya mahakama hiyo kufuatia shauri hilo.
Endapo Yanga ikigomea kupeleka timu pindi Bodi ya Ligi ikipanga tarehe ya mchezo huo, kanuni ya Ligi Kuu toleo la 2024 zitaihukumu kama ilivyoeleza.
Kanuni ya 31 (1) inayozungumzia ishu ya Kutofika Uwanjani, inabainisha hivi: “Timu yoyote itakayokosa kufika uwanjani bila ya sababu za msingi zinazokubalika kwa TFF/TPLB na/au kusababisha mchezo usifanyike itakabiliwa na adhabu zifuatazo: 1.1 Kutozwa faini ya shilingi milioni tano (5,000,000/-) ambapo shilingi milioni mbili na laki tano(2,500,000/-) itachukuliwa na Bodi ya Ligi Kuu na shilingi milioni mbili laki tano (2,500,000/-) italipwa kwa timu pinzani. 1.2 Kulipa fidia ya maandalizi/uharibifu wowote unaoweza kujitokeza.
“1.3 Kupokwa alama 15 (kumi na tano) katika msimamo wa Ligi na viongozi waliosababisha jambo hilo watachukuliwa hatua zaidi za kinidhamu. 1.3.1 Endapo timu itakuwa na alama pungufu ya 15, itakuwa na alama hasi kwa kiasi kinachopungua kwenye msimamo wa Ligi. 1.3.2 Endapo timu itamaliza msimu wa Ligi ikiwa na alama hasi, itaanza na alama hizo hasi katika msimamo wa Ligi kwenye msimu unaofuata wa Ligi ya hadhi yake.”

YANGA INAPELEKA TIMU, INASHINDA
Hebu tufikirie uongozi wa Yanga umeamua kufunika kombe na kupisha mwanaharamu apite kisha ikapeleka timu uwanjani na ikashinda, endapo ikiwa hivyo, haitakuwa ishu sana kwani mashabiki na wanachama watajiondoa kwenye akili ya mgomo na kuchekelea ushindi katika kukaribia kutetea taji lao.
YANGA IKIFUNGWA, SIMBA BINGWA
Hapa ndio balaa litazuka na kuanzia kiongozi aliyeipeleka timu uwanjani na wengine wote watakuwa wamekalia kuti kavu endapo tu timu yao itapelekwa uwanjani na kisha kupoteza mchezo huo.
Mchezo huo pia ndiyo unaweza kutoa taswira ya timu ipi itakuwa bingwa na kama Simba itashinda kuna nafasi kubwa ya kwenda kuwa bingwa msimu huu, hiyo itazidi kuchochea moto kwa kiongozi yeyote atakayeipeleka timu hiyo uwanjani kwa kuwa watani wao watatamba kwa mambo mawili wakionekana wamebana na wameachia kwa kwenda uwanjani, pia wakiutema ubingwa.

Mtego mwingine ambao upo katika sakata hili ni mpasuko wa aina tatu unaoweza kutokea ndani ya mvutano huu kati ya Yanga, TFF na TPLB.
Mpasuko wa kwanza ni wa ndani ya uongozi wa Yanga na mpaka sasa Mwanaspoti linafahamu kuna Wajumbe wa Kamati ya Utendaji wameshakaa mkao wa kung’atuka endapo tu italazimishwa timu yao kwenda uwanjani.
Viongozi hao hawataki kuonekana wasaliti kwa mashabiki na wanachama wao ambao wamesimama na kauli moja hawataki mchezo huo ufanyike.
Endapo itatokea presha ya kutakiwa mchezo huo kuchezwa ni wazi uongozi wa Yanga utagawanyika vipande viwili kwa wale ambao hawakutaka kuwasaliti wafuasi hao na wale ambao watapuuza maamuzi ya watu hao.
Mpasuko wa pili ni kati ya Yanga na TFF, TPLB kupitia shauri la CAS Yanga kama ikishinda mamlaka hizo za juu za soka hazitakuwa kwenye maelewano mazuri tena na klabu hiyo kwa kuwa tayari imeonyesha kupingana na wakubwa wake.
Yanga baada ya sakata hili inatakiwa kuishi maisha ya uhakika mbele ya TFF na TPLB kwani kosa lolote hakuna busara itakayoweza kutumika kwa kile ambacho kitaitwa kukomoana.
Yanga kama ikishinda CAS, uongozi wao utakuwa umejizolea ushindi mzuri ambao utawabeba mbele ya mashabiki wao kwa kusimamia maamuzi yao lakini pia utakuwa ushindi kwa kwanza kwao kwenye mamlaka hiyo katika kesi mbili ambazo imewahi kuziwasilisha, lakini ikiwa tofuati, italazimika kwenda kucheza mechi tarehe itakayopangwa.

Ulimuona Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma maarufu kwa jina la Mwana FA pale Tanga? Aligoma kutia neno juu ya hatma ya sakata hilo wakati kikosi cha Taifa Stars kikiagwa kwa safari ya Morocco.
Mwana FA hakufanya kwa bahati mbaya kwani Serikali bado inataka kuona TFF inaheshimiwa kwa maamuzi yake, lakini kitu kikubwa ni bado hawajaona ni wapi wanaweza kuingilia hilo kwa kutafuta suluhu.
Serikali inalazimika kulitazama sakata hilo kwa akili kubwa ili isiharibu mahusiano yake na umma wa watu wa Yanga ikiona itajiharibia kisiasa hasa kwenye mwaka huu ambao kutakuwa na uchaguzi mkuu, pia haiwezi kuikandamiza TFF ikiona inaweza kujichongea kwa kuingilia maamuzi ya kimichezo kama ambavyo Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) inavyokataza.