Mfumo wa ‘Force Acount’ waipa matokeo chanya IAA

Dar es Salaam. Kamati ya kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) imesema imeridhishwa na ufanisi na ubora wa majengo yanayoendelea kujengwa ndani ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), kupitia mapato ya ndani kwa kutumia wataalamu wa ndani yaani mfumo wa ‘Force Account’

Hayo yamebainishwa katika ziara ya kikazi ya kamati hiyo, baada ya kufanya ziara chuoni hapo na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la shahada ya juu, bweni na jengo kuu la utawala.

Kamati imeeleza pia kuridhishwa na ubora wa kazi na thamani ya fedha inayoonekana katika utekelezaji wa miradi hiyo.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) Japhet Hasunga ameupongeza uongozi wa chuo kwa ujenzi huo ambao amesema umetumia gharama nafuu, majengo yamejengwa katika viwango bora na kuonyesha thamani ya fedha kwenye miradi hiyo.

“Tumetembea sehemu nyingi tumeona wengi wao wameshindwa kutumia vizuri mfumo wa huu lakini hapa mmefanikiwa kwa hilo ninawapongeza sana na muendelee hivyohivyo,” amesema Hasunga.

Hasunga ameongeza kuwa IAA kimekuwa chuo cha mfano kutokana jitihada zinazofanyika katika kuboresha na kuongeza miundombinu ili kuendana na mipango yake ya kuongeza wanafunzi, ambapo kwa mwaka huu wa masomo kuna zaidi ya wanafunzi 17,000 katika kampasi zake hapa nchini ikiwemo Arusha, Dar es salaam, Dodoma, Babati na Songea

Kwa upande wake Mkuu wa chuo hicho, Profesa Eliamani Sedoyeka amesema miongoni mwa masuala yaliyochangia IAA kufanikiwa katika matumizi ya mfumo wa Force Account ni usimamizi wa karibu, uwajibikaji wa watalaamu katika utekelezaji wa miradi.

Aidha, Profesa Sedoyeka ameongeza kuwa IAA imeunda kamati zinazosimamia miradi na kamati hizo zina mahitaji yote ya wataalamu wanaopaswa kuwepo katika utekelezaji wa mradi.

“Sisi IAA tuna Kamati ya Force Account na chini yake zipo kamati ndogondogo za wataalamu ambao hata kama ni mkandarasi angetekeleza miradi hii angekuwa nao.”

Awali akiwasilisha taarifa ya miradi hiyo Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi IAA, Dk Daniel Shayo amesema miradi hiyo ilianza Januari mwaka 2021 na inategemewa kukamilika Juni mwaka huu na imegharimu Sh24 bilioni.

Naye Mjumbe wa kamati hiyo Mbunge wa jimbo la Momba, Kondesta Sichalwe amejivunia kusoma IAA na kusisitiza elimu aliyoipata inaishi kwani ndio iliyompa nafasi aliyonayo kwa sasa, hivyo ametoa rai kwa Watanzania kuifanya IAA chaguo la kwanza katika masomo ya elimu ya kati na ya juu.

Related Posts