Rome. Hatimaye, Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki, Papa Francis, amerejea nyumbani baada ya kulazwa hospitalini kwa zaidi ya wiki tano akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa nimonia ulioathiri mapafu yake.
Katika hali ya udhaifu, Papa Francis alionekana akiwa amebebwa kwenye gari maalumu kutoka Hospitali ya Gemelli mjini Roma, alikokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa nimonia, hali iliyomlaza hospitalini kwa muda mrefu zaidi kuliko ilivyowahi kutokea tangu alipochaguliwa kuwa Papa mwaka 2013.
Shirika la Habari la Reuters liliripoti kuwa Papa Francis ameruhusiwa kutoka hospitalini leo, Jumapili, Machi 23, 2025, baada ya kupona ugonjwa huo ambao ulikuwa tishio kwa uhai wake.
Alipokuwa akirejea nyumbani, alifanya ziara fupi katika basilika anayoiabudu, kabla ya kuanza mapumziko ya miezi miwili aliyoagizwa na madaktari ili kupata ahueni kamili.

Safari ya kurudi nyumbani
Msafara wa gari lililombeba Papa huyo (88) ulipitia lango la Perugino la Vatican, huku Papa akiwa ameketi kwenye kiti cha mbele cha gari akitumia mirija ya pua inayompa oksijeni ya ziada.
Katika safari hiyo, alifanya mapumziko mafupi katika basilika ya Mtakatifu Maria Mkuu, ambapo aliabudu picha ya Bikira Maria anayoiabudu kila baada ya ziara yake nje ya nchi.
Hata hivyo, Papa hakushuka kutoka kwenye gari, bali alikabidhi shada la maua kwa Kardinali ili aliweke mbele ya sanamu ya Salus Populi Romani, picha ya Kizantino inayoheshimiwa sana na Warumi.
Wakati akiondoka hospitalini, Papa alionyesha ishara ya kidole gumba kuashiria kuwa yuko vizuri, na alikamua mikono kuwashukuru waumini waliokusanyika kumuona.
Madaktari walitangaza kuwa Papa Francis anahitaji mapumziko kamili na ahueni kwa kipindi cha miezi miwili, wakati huu ambapo atapaswa kuepuka mikusanyiko mikubwa na shughuli zinazohitaji nguvu nyingi.
Walieleza kwamba, ingawa atakuwa akihitaji msaada wa oksijeni kwa muda, atakuwa na uwezo wa kurejea kwenye shughuli zake za kawaida baada ya kipindi cha mapumziko.
Kurudi kwa Papa nyumbani baada ya kulazwa hospitalini kwa muda mrefu zaidi katika kipindi cha miaka 12 ya upapa wake kumeleta ahueni kubwa kwa Vatican na waumini wa Kanisa Katoliki, ambao wamekuwa wakifuatilia kwa wasiwasi hali yake ya afya kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Madaktari, waumini walivyofurahi
Daktari Rossella Russomando kutoka Salerno, ambaye hakumtibu Papa lakini alikuwa hospitalini Gemelli, amesema, “Leo ninajisikia furaha kubwa. Hii ni ishara kwamba maombi yetu yote, rozari zote kutoka duniani kote, yameleta neema hii. Maombi yetu yamejibiwa.”
Kwa upande mwingine, makasisi waliendelea kujumuika katika Basilika ya Mtakatifu Petro kwa ajili ya Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa 2025, huku watu wengi wakiwa wamejaa Uwanja wa Mtakatifu Petro wakishuhudia kupitia skrini kubwa hotuba ya Papa aliyokuwa akitoa akiwa hospitalini.
Wengi wa waumini na wafanyakazi wa hospitali walielezea furaha yao kubwa walipoona Papa akitoka hospitalini baada ya miezi mitano ya matibabu.
Mario Balsamo, ambaye ni mmiliki wa duka la kahawa lililopo mbele ya Hospitali ya Gemelli, amesema: “Kwa bahati mbaya, kulikuwa na wakati ambapo wengi walihisi kwamba huenda Papa asipone, na ilikuwa maumivu kwa sisi sote. Lakini leo, tunapomwona ameruhusiwa kutoka hospitalini, tunafurahi sana.”
Mkuu wa Matibabu na Upasuaji katika Gemelli, Dk Sergio Alfieri, amethibitisha kwamba si wagonjwa wote wenye nimonia kali kama hii wanaweza kupona, na kusema:
“Maisha ya Papa yalikuwa hatarini mara mbili wakati wa shida za upumuaji, lakini alijibu kwa kusema, ‘Nipo hai bado!’ Tulijua basi alikuwa amepona.”
Dk Alfieri ameeleza kuwa ingawa Papa bado ana matatizo ya kuzungumza kutokana na uharibifu wa mapafu na misuli ya kupumua, alitabiri kuwa hali yake itaimarika kadri anavyoendelea kupata nafuu.
Papa Francis, mzaliwa wa Argentina, ana historia ya ugonjwa sugu wa mapafu na aliwahi kuondolewa sehemu ya pafu moja akiwa kijana. Alilazwa Hospitali ya Gemelli Februari 14, 2025, baada ya kukumbwa na changamoto za kupumua.
Madaktari waligundua kuwa alikuwa na maambukizi mchanganyiko ya bakteria, virusi, na fangasi katika mfumo wake wa upumuaji, hali ambayo ilisababisha nimonia kwenye mapafu yake yote mawili.
Madaktari walifafanua kuwa ugonjwa wa nimonia alioathiriwa nao ni miongoni mwa magonjwa hatari, na hata iliwalazimu kutoa kiasi kikubwa cha makohozi kutoka kwenye mapafu yake kwa njia ya ‘aspiration’ ili kumsaidia kupumua vizuri.
Licha ya matatizo hayo, yuko nyuma Papa hakuwahi kuwekwa kwenye mashine ya kupumulia wala kupoteza fahamu, na alionyesha hali ya ushirikiano na ufanisi mkubwa wakati wote wa matibabu.
Ugonjwa, changamoto za upumuaji
Madaktari walieleza kuwa ugonjwa wa nimonia ulisababisha upungufu wa damu (anemia), kiwango cha chini cha chembe sahani za damu, na dalili za kufeli kwa figo, lakini baada ya kufanyiwa usafishaji wa damu kwa awamu mbili, hali hiyo ilirejea kuwa ya kawaida.
Daktari wake binafsi, Dk Luigi Carbone, ameeleza matumaini yake, kwamba Papa atapunguza hitaji la msaada wa kupumua kadri mapafu yake yanavyoendelea kupona.
Amesema: “Kwa siku tatu au nne amekuwa akiuliza lini atarudi nyumbani, hivyo ana furaha sana kwa kuwa sasa amepona.”