Dodoma. Serikali imeainisha sababu zinazomfanya Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi, kuwa na uwezo wa kushinda katika uchaguzi wa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa kanda ya Afrika.
Nafasi ya Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika iliachwa wazi na Dk Faustine Ndugulile, ambaye alifariki dunia Novemba 27, 2024, baada ya kushinda uchaguzi wa nafasi hiyo uliofanyika Agosti 26, 2024, Congo Brazzaville.
Dk Ndugulile alikuwa mmoja wa wagombea watano waliojitokeza kurithi mikoba ya Dk Matshidiso Moeti aliyekuwa amehitimisha muhula wake wa pili.

Wagombea wengine walioshindana na Dk Ndugulile walikuwa Dk Boureima Hama Sambo wa Niger, Dk Richard Mihigo wa Rwanda, Dk N’da Konan Michel Ya wa Ivory Coast na Dk Ibrahima Socé Fall wa Senegal.
Kifo cha Dk Ndugulile kiliacha pengo katika shirika hilo, na hivyo kuhitaji uchaguzi mpya wa kujaza nafasi hiyo muhimu.
Desemba 10, 2024 akiwaapisha viongozi katika Ikulu ndogo ya Tungui Zanzibar, Rais Samia Suluhu Hassan alimtaka Profesa Janabi kujiandaa kugombea nafasi hiyo utakapofika wakati wa uchaguzi.
Rais Samia aliongeza kuwa Profesa Janabi ana uwezo mkubwa na uzoefu wa kipekee katika masuala ya afya na kwamba Serikali inamuunga mkono katika harakati zake za kushinda nafasi hiyo.
Profesa Janabi, ambaye ni mtaalamu mwenye uzoefu mkubwa katika uongozi wa masuala ya afya, anakwenda kuchuana na wagombea Profesa Moustafa Mijiyawa kutoka Togo, Dk N’da Konani Michel Yao kutoka Ivory Coast, na Mohamed Lamine Drame kutoka Guinea. Uchaguzi huu utafanyika Mei 18, 2025, mjini Geneva, Uswisi.
Akizungumza jana Jumamosi Machi 22,2025, Waziri wa Afya, Jenista Mhagama amezitaja sababu hizo ni kukua kwa kasi ya mahusiano mazuri ya kidiplomasia pamoja na ushirikiano ambao Rais Samia, ameendelea kuimarisha baina ya Tanzania na mataifa mengine.
Kwa mujibu wa Mhagama, Profesa Janabi atashinda nafasi hiyo kutokana na sifa zake za kipekee na uzoefu wake mkubwa katika masuala ya ugharamikiaji wa huduma za afya ikiwamo usimamizi wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ambayo ni moja ya vituo vikubwa na muhimu katika mfumo wa afya wa Tanzania.
Amesema Profesa Janabi ana uwezo wa kuchukua nafasi hiyo kwa ufanisi kutokana na mafanikio yake katika kuboresha huduma za afya nchini na kimataifa.
“Uzoefu wa Profesa Janabi katika masuala ya ugharamikiaji wa huduma za afya, hususan katika kipindi hiki ambapo dunia inakutana na changamoto kubwa ya kutafuta vyanzo vya uhakika vya kugharamia huduma za afya na uzalishaji wa bidhaa, pamoja na ufanisi wake katika usimamizi wa mifumo ya utoaji wa huduma za afya, unatoa nafasi nzuri ya kushinda nafasi hii,” amesema.
Ametaja sababu nyingine ni uzoefu wake ambao umedhihirika katika kuzuia na kudhibiti na kupambana na magonjwa ya mlipuko na yasiyoambukiza ambayo yamekuwa yakiongezeka kwa kasi kubwa ulimwenguni.
Mhagama amesema kampeni za wagombea wa nafasi hiyo tayari zimeshaanza kwa njia mbalimbali na hivyo Watanzania kwa umoja wao hawana budi kushirikiana kumnadi Profesa Janabi kwa nguvu zote.
“Nitoe wito kwa wananchi, mashirika na wadau wa sekta (ya afya) ya ndani na nje kuungana pamoja katika kumnadi na kumwombea dua mgombea wetu,” amesema.
Amesema wana imani kuwa kwa uongozi wake, Afrika itapiga hatua kubwa katika kuboresha mifumo ya afya, kupambana na magonjwa na kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora za afya.