Trump awafutia kibali cha kupata taarifa za usalama Clinton, Harris na Biden

Washington. Rais wa Marekani, Donald Trump, ameanzisha hatua kali kwa kufuta vibali vya kupata taarifa za usalama kwa baadhi ya viongozi na maofisa wastaafu wa Serikali, hasa kutoka Chama cha Democratic.

Miongoni mwa waliokumbwa na hatua hiyo ni Kamala Harris, Hillary Clinton, familia ya Rais Joe Biden, na baadhi ya maofisa wakuu wa utawala wa zamani.

Uamuzi huu umeleta mjadala katika siasa za Marekani, huku wengi wakisema kuwa ni hatua ya kisiasa na kisasi dhidi ya wapinzani wake na wakosoaji wa utawala wake.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka vyombo vya habari, Trump alitangaza Februari 2025 kuwa alifuta vibali vya usalama kwa Rais mstaafu Joe Biden, akieleza kuwa ilikuwa ni muhimu kubatilisha ruhusa ya usalama ya Biden na “mtu yeyote mwingine” katika familia yake.

ilikuwa ni sehemu ya hatua yake ya kupunguza ufikiaji wa taarifa za kiusalama kwa viongozi wa zamani na maofisa walio na historia ya kuikosoa Serikali ya Trump.

Kufutwa kwa vibali vya usalama kuna maana kubwa kwa wale waliokumbwa na marufuku hii, kwani hawawezi tena kupata taarifa za kiusalama ambazo zilikuwa zinapatikana kwa viongozi wa zamani kwa misingi ya heshima.

Taarifa za kiusalama za taifa, kama vile muhtasari wa kila siku wa rais, na taarifa nyingine za siri zinazoshikiliwa na vyombo vya ujasusi, sasa hazitopatikana kwa watu hawa, ikiwemo wakosoaji na maofisa wa zamani wa Serikali.

Trump amesisitiza kuwa amechukua hatua hiyo kwa masilahi ya taifa, akidai kuwa “si kwa manufaa ya kitaifa” kwamba watu hao waendelee kuwa na ufikiaji wa taarifa za siri za usalama wa taifa.

Kwa kawaida, sheria za Marekani zimekuwa zikitoa mwanya kwa marais wa zamani na baadhi ya maofisa wa serikali kuwa na ufikiaji wa taarifa za kiusalama, kwa ajili ya kutoa ushauri au kushirikiana na viongozi wa sasa.

Hata hivyo, Trump ameweka wazi kuwa hataki viongozi na maofisa wa zamani wa chama cha upinzani kuwa na ufikiaji wa taarifa hizo muhimu.

Agizo la Trump linawahusu pia baadhi ya viongozi wa Serikali ya Biden, wakiwemo Waziri wa Mambo ya Nje, Antony Blinken, Mshauri wa usalama wa taifa, Jake Sullivan, Naibu mwanasheria mkuu, Lisa Monaco na wengine wengi waliotajwa kuwa wapinzani au wakosoaji wa utawala wake.

Viongozi hao wakiwa katika nafasi muhimu katika Serikali ya Biden, wamepoteza kibali cha kupata taarifa za usalama wa taifa, hatua ambayo inatajwa kama ya kipekee na inayoweza kuchochea mivutano zaidi katika siasa za Marekani.

Pia, Trump ameongeza idadi ya watu waliopoteza vibali vya usalama kwa kulenga maofisa wa zamani wa utawala wake, ikiwa ni pamoja na Fiona Hill na Alexander Vindman, ambao walitoa ushahidi muhimu wakati wa kesi yake ya kwanza ya kumvua madarakani mwaka 2019.

Vilevile, Trump ameendelea kuwalenga wapinzani wake wa chama cha Republican, akiwemo Liz Cheney na Adam Kinzinger, ambao walikuwa sehemu ya uchunguzi kuhusu shambulio la Januari 6, 2021, dhidi ya Bunge la Marekani.

Hatua hii pia imeathiri mawakili na waendesha mashitaka ambao walishirikiana na utawala wa Trump au walikuwa sehemu ya kesi za kisheria dhidi yake.

Miongoni mwa waliopoteza ruhusa za usalama ni Mwanasheria Mkuu wa New York, Letitia James, ambaye amefungua kesi nyingi dhidi ya Trump na familia yake.

Aidha, Mwendesha Mashitaka wa Manhattan, Alvin Bragg, ambaye alimshtaki Trump kwa kosa la kufanya malipo ya kumnyamazisha mtu, pia amepoteza vibali vya usalama.

Kufutwa kwa ruhusa za usalama kwa wanasheria na mawakili, wakiwemo Andrew Weissmann na Norm Eisen, kunaweza kuwa na athari katika ufanisi wa kesi zinazowahusu, kwani hawawezi tena kupata taarifa muhimu za kiusalama ambazo zingewasaidia katika kuchunguza au kushughulikia mashitaka dhidi ya Trump.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.

Related Posts