Unguja. Wakati Zanzibar ikizindua sera mpya ya maji na usafi wa mazingira ya mwaka 2025, ushirikishwaji wa sekta binafsi unatajwa kuleta mabadiliko ya upatikanaji wa huduma hiyo hasa vijijini.
Sera ya Maji ya Taifa ya mwaka 2004 inaonyesha kuwa na upungufu, hivyo kusababisha kutokuwapo kwa ufanisi katika utoaji huduma ya majisafi na salama kisiwani hapa.
Akizungumza wakati wa uzindua wa sera hiyo jana Jumamosi Machi 22, 2025, Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema Serikali imepanga kushirikisha sekta binafsi katika utoaji huduma za maji ikiwa ni sehemu ya kuwajengea uwezo watendaji na kuimarisha upatikanaji wa huduma ya uhakika na kwa haraka.
Dk Mwinyi amesema wamepata uzoefu huo baada ya kushirikisha sekta binafsi katika utoaji wa huduma kwenye afya, uwanja wa ndege na uendeshaji wa bandari.
“Mifumo ya usimamizi majitaka itaimarishwa na hatimaye kupunguza uchafuzi wa mazingira katika miji na vijiji kwa kuhakikisha kuwa, mazingira yanatunzwa kwa faida ya jamii nzima,” amesema.
Amesema lengo kuzishirikisha sekta binafsi ni kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za maji na kuleta ubunifu utakaohakikisha huduma hizo zinapatikana kwa haraka, kwa ubora na kwa usawa Unguja na Pemba.
Mbali na upatikanaji wa huduma bora, ushirikishaji huo utakuza ushirikiano serikalini, sekta binafsi na mashirika ya kiraia katika utekelezaji wa miradi ya maji na usimamizi wa usafi wa mazingira.
Dk Mwinyi amesema pamoja na kuimarisha usimamizi wa rasilimali maji na kuhakikisha upatikanaji wa majisafi na salama kwa kila mwananchi, pia, itasaidia juhudi za kupunguza athari za tabianchi zinazotokana na uchafuzi wa mazingira.
Kadhalika, sera hiyo itaimarisha elimu ya umma kuhusu umuhimu wa usafi wa mazingira, matumizi sahihi ya maji na hatari za uchafuzi wa mazingira kwa afya ya jamii.
“Hivyo kwa kushirikisha sekta binafsi ni matarajio yetu tutaimarisha sekta hiyo kwa kuleta teknolojia mpya, kujenga na kuimarisha miundombinu ya maji,”amesema.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Joseph Kilangi amesema umuhimu wa kuwa na sera ya maji ulijitokeza baada ya uzinduzi mpango wa sekta ya maji wa mwaka 2022/27.
“Hii sera imezingatia maoni ya wananchi na wadau katika uandaaji wake na zimetumiwa mbinu za kisasa katika kufanya tathmini ya maoni ya wadau kujua maeneo ya kipaumbele,” amesema Kilangi.
Amesema wizara imetayarisha mpango wa utekelezaji katika mawasiliano, mwongozo wa ufuatiliaji na tathmini ya sera yenyewe.
Baadhi ya miongozo inayotolewa na sera mpya ni kujumuisha usimamizi wa maji safi na usafi wa mazingira kama inavyofanyika kwenye nchi nyingine huku ikiwapunguzia mamlaka ya maji majukumu ya usimamizi wa rasilimali maji na usafi wa mazingira.
“Sera imetoa fursa kwa sekta binafsi katika uwekezaji na kutoa huduma katika sekta ya maji na usafi wa mazingira na kutoa mwongozo kuhusu kutafuta vyanzo vya maji ikiwamo kuchakata maji na uvunaji maji ya mvua na kuyabadilisha maji chumvi kuwa safi na salama,” amesema Katibu Mkuu.
Mwakilishi wa Shirika la Kimataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef), Lawrence Oundo amesema ukosefu wa maji unaathiri moja kwa moja afya, elimu, tija ya kiuchumi na usawa wa kijinsia.
Ameipongeza Zanzibar kwa jitihada inazochukua na kuongezeka kwa maji kutoka asilimia 89 mwaka 2009 hadi asilimia 97 mwaka 2022.
Hata hivyo, amesema changamoto zinabaki, asilimia 34 ya watoto wa Zanzibar wana lishe duni kwa sababu ya maji na usafi na mazingira.
“Katika muongo mmoja uliopita, tumetoa klorini kwa utakaso wa maji, kuunga mkono ujenzi wa vyoo vya shule na mifumo ya usambazaji wa maji, kuwezesha uvumbuzi wa dijiti katika sekta ya maji na kukuza vifaa vya kunawa mikono kwa watoto wa shule na jamii,” amesema Oundo.
Amesema uwekezaji wa Unicef, sekta ya maji Zanzibar, umezidi Dola 10 milioni za Marekani (Sh23 bilioni).
“Na tunabaki kujitolea kufanya kazi kando na Serikali na washirika ili kuhakikisha maendeleo endelevu,”amesema Oundo.
“Wacha tuhakikishe sera hii inatafsiriwa kuwa mabadiliko halisi ya kudumu kwa kila kaya, shule na kituo cha afya. Wacha tuwekewe katika huduma salama za maji, na hali ya maji na mazingira ya usafi wa mazingira ili kupata mustakabali mzuri kwa wote.”