Uzinduzi operesheni ‘No Reforms No Election’ Chadema waiva Mbeya

Mbeya. Maandalizi ya mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) yanaendelea kuwekwa sawa, huku viongozi wakieleza usalama ulivyo na matarajio ya tukio hilo.

Chadema inatarajia kufanya mkutano wake leo, Machi 23 katika viwanja vya Ruanda Nzovwe jijini Mbeya ambapo pamoja na mambo mengine watazindua operesheni za chama hicho ambazo ni  ‘No Reforms, No Election’, ‘Stronger Together’ na ‘Tone Tone’.

Mkutano huo utaongozwa na Mwenyekiti wake Taifa, Tundu Lissu huku viongozi wengine wa chama hicho wakishiriki tukio hilo kabla ya kusambaa katika mikoa ya Kanda ya Nyasa.

Mwananchi imefika eneo la uwanja huo na kushuhudia shughuli za kufungwa kwa majukwaa huku baadhi ya makada wakianza kuingia eneo hilo.

Katibu wa Chadema mkoani humo, Hamad Mbeyale amesema maandalizi yako salama na hakuna tatizo lolote ambapo matarajio yao ni kufanikisha mkutano huo.

Amesema viongozi wanatarajia kuanza kuingia viwanjani hapo kuanzia saa 8 mchana, akiwaomba wananchi na wafuasi wa chama hicho kujitokeza kwa wingi akiwahakikishia usalama wa kutosha.

“Jukwaa kuu limekamilika, usalama ni wa hali ya juu hatuna tatizo lenye kuzuia shughuli, wananchi waje kwa wingi kwakuwa viongozi wataingia kwa pamoja” amesema Mbeyale.

Baada ya mkutano huo, Lissu ataelekea mkoani Rukwa ambapo atafanya vikao vya ndani na mikutano ya hadhara kwa siku nne kisha kutua mkoani Songwe.

Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho, Taifa John Heche atafanya ziara mkoani Mbeya kisha kutinga mkoani Njombe kabla ya vigogo hao kuhitimishia ziara yao mjini Iringa Machi 29 kwa mkutano wa hadhara.

Related Posts