Roma. Kiongozi wa Kanisa Katoliki, Papa Francis (88) anatarajiwa kutolewa hospitalini leo Jumapili Machi 23, 2025, baada ya kukaa zaidi ya mwezi mmoja akitibiwa maradhi ya nimonia ya mapafu.
Taarifa ya Papa Francis kutolewa hospitalini baada ya afya yake kuimarika imetolewa jana (Jumamosi) jioni na Sergio Alfieri, ambaye ni Mkuu wa timu ya madaktari wanaomuhudumia kiongozi huyo wa kiroho.
“Baba Mtakatifu atatolewa kesho (leo) akiwa katika hali thabiti ya kiafya, akiwa na maagizo ya kuendelea kwa kiasi fulani na matibabu ya dawa pamoja na kipindi cha angalau miezi miwili cha kupona na kupumzika,” Alfieri aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano wa Jumamosi uliofanyika Hospitali ya Gemelli.
“Tunafurahi kusema kwamba kesho (leo) atakuwa nyumbani,” aliongeza.
Msemaji wa Vatican, Matteo Bruni amesema leo Jumapili kuwa Papa pia anatarajiwa kuonekana hadharani mbele ya umma wakati akirejea kwenye makazi yake ya Casa Santa Marta anakoishi tangu alipochaguliwa mwaka 2013.
Kwa mujibu wa Naibu Mkurugenzi wa Huduma za Afya za Vatican, Luigi Carbone, Francis, ambaye amekuwa hospitalini tangu Februari 14, amepona nimonia iliyokuwa katika mapafu yake yote mawili, bado hajapona kabisa maambukizi hayo.
“Sauti ya Papa inaimarika lakini bado anahitaji muda wa kupona,” amesema Carbone.
Carbone amesema Papa huyo ataendelea na tiba pamoja na mazoezi ya mwili baada ya kutoka hospitalini.
Ofisi ya habari ya Vatican ilisema pia kuwa Francis atatoa baraka na salamu kwa waumini mwishoni mwa sala ya Angelus ya Jumapili.
Francis kwa kawaida huongoza sala hiyo na kutoa tafakari kila wiki, lakini hajafanya hivyo kwa takriban ibada tano za Jumapili.
Waumini wa Kikatoliki kutoka Jiji la Vatican hadi Argentina, anakotoka Papa Francis, wameonekana kufurahia na kusherehekea habari hizo.
Wengi walikusanyika katika Uwanja wa Mtakatifu Petro jijini Vatican Jumamosi usiku kuendelea kumwombea Papa kama walivyokuwa wakifanya tangu alipopelekwa hospitalini. Lakini, leo maombi yao yaliambatana na faraja.
“Ni furaha kubwa kwa sisi sote, kwa waumini wote, kwa sisi wote tuliokuja hapa kila jioni kuomba,” Richard Gundel, mmoja wa waumini, aliliambia shirika la habari la Reuters uwanjani hapo.
“Sasa tumepokea habari njema, furaha kubwa,” alisema Gundel.
Katika Mji Mkuu wa Argentina, vipande vya video vimewaonyesha waumini wakiwa na picha ya Papa ikiwa imewekwa katika fremu ndani ya kanisa moja mjini Buenos Aires Jumamosi, huku waumini wakihudhuria misa ya kumuombea afya njema.
“Niliposikia habari leo (Jana ), mwili wangu ulinisisimka,” mmoja wa waumini, Raquel Martinez, aliiambia Reuters nje ya kanisa huku akiwa na tabasamu pana usoni. “Niliguswa sana, ni kitu kisichoelezeka.”
Ingawa hajaonekana hadharani kwa wiki kadhaa, uwepo wake umekuwa ukihisiwa kupitia ujumbe mfupi wa sauti uliotolewa na Vatican, pamoja na picha iliyomuonyesha akiomba katika kanisa la hospitali hiyo wiki iliyopita.
Tangu Papa alipolazwa hospitalini katikati ya Februari, kulikuwa na vipindi viwili hatari ambavyo maisha yake yalikuwa mashakani, kulingana na Vatican na timu ya madaktari wake.
Carbone aliwaambia waandishi wa habari katika mkutano wa hospitali Jumamosi kwamba Papa yuko katika hali nzuri ya kiakili na amekuwa akiomba atolewe hospitalini kwa siku chache zilizopita.
Wiki iliyopita, Papa aliidhinisha mchakato mpya wa miaka mitatu wa mageuzi ndani ya Kanisa Katoliki, ishara thabiti kwamba ana mpango wa kubaki katika wadhifa wake licha ya kukaa hospitalini kwa muda mrefu.
Mageuzi yanayozingatiwa ni pamoja na namna ya kuwapa wanawake nafasi ndani ya Kanisa Katoliki, ikiwemo kuwapa daraja la ushemasi, pamoja na ushirikishwaji wa wale wasiokuwa makasisi katika uongozi na maamuzi.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.