WASOMI WATAKA CHADEMA WAFUATE USHAURI WA RAILA ODINGA

*Wasema majadiliano ni njia bora ya kupata suluhu ya masuala yao

Wachambuzi wa siasa na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Richard Mbunda na Dk. Frolence Rutechura, wamewashauri viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kufuata ushauri wa mwanasiasa mkongwe wa Kenya, Raila Odinga, wa kutafuta suluhu kwa njia ya majadiliano na serikali. Wanasiasa hao wamesisitiza kuwa Odinga ni mfano wa kiongozi aliyewahi kushiriki migogoro ya kisiasa nchini mwake, lakini baadaye alipata suluhu kupitia mazungumzo.

Kauli hii inakuja baada ya viongozi wa CHADEMA, akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, Makamu wake Bara, John Heche, na Mjumbe wa Kamati Kuu, Godbless Lema, kukutana na Raila Odinga jijini Nairobi, Machi 22. Mkutano huo, uliofanyika baada ya viongozi hao kutoka Zanzibar walikokwenda kujitambulisha kwa wanachama wao, umeibua mitazamo tofauti kutoka kwa wachambuzi wa siasa nchini.

Katika mahojiano maalum, Dk. Richard Mbunda alisema mkutano wa CHADEMA na Odinga unaonesha wazi kuwa chama hicho kinatafuta uungwaji mkono wa kimataifa kwa ajenda yao ya No Reform, No Election. Alisema hatua yao ya kwenda Kenya ni jitihada za kutafuta uhalali wa ajenda hiyo, huku akibainisha kuwa hata Raila Odinga, ingawa anaelewa madai yao, bado anasisitiza umuhimu wa uchaguzi wa amani.

“Baada ya kukutana na Msajili wa Vyama vya Siasa, CHADEMA walitangaza kuwa wataendelea kuhamasisha ajenda yao kwa Watanzania. Lakini pia wanatafuta uhalali wa kimataifa, ndiyo maana wamekutana na Raila Odinga. Ingawa Odinga anaonesha kuwaunga mkono, bado amesisitiza kuwa uchaguzi ni muhimu kwa ustawi wa demokrasia nchini,” alisema Dk. Mbunda.

Dk. Mbunda pia alizungumzia dhamira ya Rais wa Awamu ya Sita, Dk. Samia Suluhu Hassan, kuhusu falsafa ya 4R inayojumuisha Maridhiano, Ustahimilivu, Mabadiliko na Kujenga Upya. Alisema kuna hatua kubwa tayari zimechukuliwa kuhusiana na madai ya CHADEMA, lakini huenda chama hicho hakijaridhika na kiwango cha utekelezaji.

“Mh. Rais alipoingia madarakani, alianzisha kikosi kazi chini ya Prof. Rwekaza Mukandala kwa ajili ya kuboresha siasa nchini. Tayari baadhi ya mageuzi yamefanyika, lakini labda si kwa kiwango kinachowaridhisha CHADEMA. Hili ni suala la mjadala,” alisema.

Dk. Mbunda aliongeza kuwa, licha ya juhudi za maridhiano kati ya CCM na CHADEMA, bado haijafahamika ni kwa nini majadiliano hayo hayajazaa matunda yaliyotarajiwa.

 “Mh. Rais ametaka kuwe na majadiliano, na tayari mazungumzo yamefanyika kati ya CCM na CHADEMA mara kadhaa. Swali ni kwa nini hayajazaa matunda? Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga, anashauri mazungumzo hayo yaendelee ili wananchi wasiendelee kuishi katika hali ya sintofahamu,” alisema.

Hata hivyo, Dk. Mbunda alihoji faida ya ajenda ya No Reform, No Election, akisema bado haijawafikia wananchi ipasavyo.

“Katika maisha yangu sijawahi kuona faida ya ajenda hii, maana hata wananchi wa kawaida hawaelewi inamaanisha nini,” alisema

Related Posts