Wawili waliohukumiwa kifo kwa kumuua bodaboda waachiwa huru

Arusha. Mahakama ya Rufani imewaachia huru Fred Nyagawa na Isaya Mgimba, waliokuwa wamehukumiwa kunyongwa hadi kufa baada ya kukutwa na hatia ya kumuua dereva bodaboda, Mchape Mkosa.

Aidha, Mahakama hiyo imethibitisha hukumu ya kunyongwa hadi kufa aliyokuwa amehukumiwa James Mteleke.

Fred, Isaya na James walihukumiwa adhabu hiyo na Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Novemba 12, 2021 katika kesi ya mauaji iliyokuwa ikiwakabili.

Katika kesi hiyo, wote watatu na mtu mwingine aliyeachiwa huru, walidaiwa Desemba 16, 2015, marehemu, akimiliki pikipiki aliyokuwa akiifanyia kazi kama bodaboda, alikutwa eneo la Kibao cha Mkwavila, alifuatwa na James kwa ajili ya kumpeleka mahali kama abiria.

Ilidaiwa kesho yake, Desemba 17, 2015 alikutwa ameuawa katika Kijiji cha Mpogolo akiwa na jeraha la kukatwa na kitu chenye ncha kali,  ambapo uchunguzi wa mwili wake ulionyesha sababu ya kifo ni kuvuja damu kutokana na majeraha mengi ya kukatwa.

Hukumu ya rufaa iliyowaachia Fred na Isaya huru na kumng’ang’ania James, imetolewa Machi 21, 2025 na jopo la majaji watatu ambao ni Rehema Kerefu, Gerson Mgonya na Lameck Mlacha.

Majaji hao walifikia uamuzi huo baada ya kupitia mwenendo wa kesi na kusikiliza hoja za pande zote mbili na kubaini upande wa mashitaka ulishindwa kuthibitisha kosa bila kuacha shaka dhidi ya washtakiwa hao wawili.

Katika kesi namba hiyo ya mwaka 2017, washtakiwa hao walitenda kosa hilo katika Wilaya ya Wangingombe mkoani Njombe ambapo upande wa mashitaka uliwasilisha mashahidi saba na vielelezo tisa ili kuthibitisha kesi hiyo.

Shahidi wa nne ambaye ni kaka wa marehemu, Yohana Mkosa alisema siku ya tukio, wakiwa katika eneo la Kibao cha Mkwavila, alifika James (mrufani wa tatu) na kuondoka kama abiria na ndugu yake lakini hakurejea tena.

Alisema kesho yake alipata taarifa kuwa mdogo wake ameuawa katika msitu wa Kijiji cha Mpogolo na alipofika alikuta mwili wa ndugu yake ukiwa na jeraha huku akiwa amezungukwa na watu wengi wakiwemo polisi.

Alifafanua kuwa aliwaambia polisi kuwa alimshuku mtu aliyeondoka na marehemu siku iliyopita na kuwa hajui jina lake, lakini anaweza kumtambua kwa sura.

Shahidi wa tatu, Inspekta Raphael Mlangwa, alidai akiwa katika Kituo cha Polisi Makambako Machi 7, 2016, alipigiwa simu na Mkuu wa Polisi wa Wilaya na kupangiwa kufanya gwaride la utambuzi lililomuhusisha mtuhumiwa wa mauaji, James.

Alisema gwaride liliandaliwa nyuma ya kituo cha polisi na alipokwenda kwa ajili ya kumtambua muhusika alikuta washiriki 10 wakiwa wamejipanga huku mrufani huyo wa tatu akiwa miongoni mwao.

Alisema mahakamani kuwa James alisimama katika nafasi ya tatu kutoka kulia ambapo shahidi wa nne aliombwa kupita kwenye mstari na kumgusa mtu begani atakayemtambua na kuwa alimgusa James ambaye alipoulizwa kama ameridhishwa na utaratibu uliotumika kumtambua, alisema ameridhishwa.

Shahidi wa kwanza, Inspekta Kelvin  Lubera, aliyemuhoji James Machi 14, 2016 kuhusu mauaji hayo, na kuwa alikiri kumuua marehemu akiwa na watu wengine na kupora pikipiki ambayo aliiuza Mbeya na akakubali kuwapeleka Mbeya.

Shahidi huyo alikwenda Mbeya na polisi wengine, wakiongozwa na James hadi Kijiji cha Msheme, na kuwapeleka kwenye nyumba ya mnunuzi, Abraham Kidile.

Alieleza walifanya upekuzi katika nyumba yake na kupata pikipiki iliyokuwa, wakaandaa cheti cha kukamata na kurudi kituo cha polisi cha Makambako wakiwa na hiyo pikipiki.

Aidha, ushahidi ulionyesha zaidi kwamba, mrufani wa kwanza alikiri kutenda kosa hilo mbele ya shahidi wa pili, James na mrufani wa pili alikiri mbele ya shahidi wa saba ambapo wanadaiwa kushirikiana kwa pamoja kupanga kumvamia na kumuua marehemu katika harakati za kupora pikipiki yake waliyoiuza Mbeya.

Katika utetezi wa mrufani wa kwanza, alikana kuwafahamu warufani wenzake na kuwa ni wageni huku akidai maelezo ya onyo hayakuwa kauli yake na kuwa alipofikishwa kwenye chumba cha uchunguzi alikuta karatasi zikiwa tayari zimeandikwa na kutakiwa kusaini, ambapo alikataa lakini baada ya kupigwa sana alikubali.

Mrufani wa pili alisema kutokumjua mrufani wa kwanza lakini alimfahamu mrufani wa tatu na alinunua pikipiki hiyo kutoka kwake, kama dalali na kukana maelezo ya onyo.

Mrufani wa tatu alikana kuwapeleka polisi Mbeya kuchukua pikipiki, alikana kumuua marehemu lakini anamfahamu mrufani wa pili, hamjui wa kwaza na kuwa alikuwa anamfahamu mrufani wa pili kwani alimuuzia pikipiki hiyo kama dalali na kukana maelezo ya onyo na ungamo.

Kutokana na ushahidi wa shahidi wa nne, ungamo la mdomo la mrufani wa tatu lililotolewa kwa shahidi wa kwanza, makubaliano ya mauzo na risiti ya mauzo, na maelezo ya onyo ya mrufani wa kwanza na pili, jaji aliona mashitaka kuthibitisha kesi hiyo bila kuacha shaka, akawatia hatiani na kuwahukumu adhabu ya kifo.

Katika rufaa hiyo kila mrufani alikuwa na uwakilishi wa wakili huku wakiwa na sababu ikiwemo Mahakama ilikosea kisheria kuwatia hatiani warufani bila kutathmini ushahidi uliotolewa na upande wa mashitaka.

Mahakama ilikosea kisheria kwa kutegemea cheti cha kukamata ambacho kilichukuliwa kinyume cha sheria na Mahakama ilishindwa kutathmini ushahidi uliotolewa wakati wa kesi.

Jaji Mlacha amesema baada ya kupitia mwenendo wa kesi hiyo, wameona Mahakama iliyosikiliza kesi haikuendesha kesi ndani ya kesi na licha ya mrufani wa kwanza na wa pili waliwasilisha pingamizi chini ya kifungu cha 27 cha Sheria ya Ushahidi, kwa madai kwamba hawakutoa taarifa hizo za maelezo ya onyo popote.

Jaji amesema mapingamizi hayo yalitupwa kwa njia ya mawasilisho badala ya kesi ndani ya kesi.

“Tunadhani, kwa kuzingatia mamlaka zilizotajwa hapo juu, utaratibu uliopitishwa haukuwa wa kawaida wa kutengeneza vielelezo vya tano na tisa kinyume cha sheria mbele ya mahakama, tunafuta kwenye kumbukumbu vielelezo hivyo,” amesema.

Amesema swali linalofuata ni iwapo kuna ushahidi wa kuwatia hatiani warufani baada ya kufuta vielelezo hivyo na kuwa hilo linawapeleka kwenye uchambuzi wa ushahidi uliobaki.

Jaji Mlacha amesema wakiangalia ushahidi kwa makini hawaoni namna inavyoweza kuwaunganisha mrufani wa kwanza na wa pili kwa kosa waliloshtakiwa bila kuwepo kwa vielelezo vya tano na tisa na kuwa mrufani wa tatu alikiri kutenda kosa hilo na watu wengine lakini hawakutajwa.

“Kwa kuzingatia yale tuliyojaribu kuyaonyesha hapo juu, tunatupilia mbali na kufuta hukumu za kifo dhidi ya mrufani wa kwanza na wa pili, waachiwe huru mara moja isipokuwa kama wameshikiliwa kwa sababu nyinginezo. Rufaa ya mrufani wa tatu imetupiliwa mbali,” amehitimisha Jaji Mlacha.

Related Posts