Chanzo watendaji SMZ kutoelewana ofisini chatajwa

Unguja. Licha ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi kukemea viongozi wa umma kugombana ofisi, bado changamoto hiyo imeendelea kuibuka na kukwamisha kazi za umma.

Akizungumza katika kongamano la pili la kiimani kwa viongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) lililofanyika ukumbi wa Idrissa Abdulwakil Kikwajuni, Zanzibar jana Jumapili Machi 23, 2025, Rais Mwinyi amesema kukosekana kwa utii wa vongozi kumekuwa chanzo cha fitina, majungu na mifarakano baina ya watendaji wakuu kwa baadhi ya taasisi za umma.

Amesema amekuwa akipokea taarifa nyingi za ugomvi kwa taasisi za umma baina ya watendaji wenye dhamana, jambo ambalo Serikali inadhamiria kuliondoa kwa kuchukua hatua.

“Serikali itahakikisha kuwepo kwa utii wa viongozi katika utendaji  wa taasisi za umma ili kuepusha mifarakano na majungu,” amesema Rais Mwinyi.

Hata Hivyo, hii si mara ya kwanza kwa kiongozi huyo kulalama juu ya watendaji wa umma hususani anaowateua kuendekeza ugomvi ofisini, akisema hatua hiyo inakwamisha kazi za kuwatumikia wananchi.

Novemba 20, 2023 Dk Mwinyi wakati anawaapisha wakuu wa mikoa na wilaya aliowateua na kuwabadilisha vituo vyao vya kazi, alionesha kukerwa na tabia ya ugomvi wa wateule wake akisema hali hiyo ikiendelea hatosita kuchukua hatua.

“Kila siku waziri kagombana na katibu mkuu wake, waziri kagombana na wakurugenzi wake, katibu mkuu kagombana na wakurugenzi wake, mkuu wa mkoa na mkuu wa wilaya hawaelewani, mkuu wa wilaya na katibu tawala hawaelewani, hii kazi itafanyikaje,” alihoji Rais Mwinyi.

“Mpo pale lazima kufanya kazi kwa pamoja, wale ni wateule wangu mimi, sio wenu ninyi, ninapomteua mtu wala siwaulizi kwa sababu sio uteuzi wako.

“Kwa hiyo, ningependa hili niliseme kwa Serikali nzima kuanzia sasa watu ambao hawawezi kufanya kazi kwa pamoja maana yake hawafai,” alisema.

Akizungumza kuendelea kulalamika kwa kiongozi huyo, mtaalamu wa masuala ya uongozi na utawala bora, Ali Haji Makame amesema licha ya kupanga na kupangua ni suala la Rais mwenyewe, lakini pengine anaona bado wanaogombana wana manufaa kwenye utendaji.

Hata hivyo, amesema ikiwa anasema bila kuchukua hatua, viongozi hao wanaweza kuona kama ni mazoea na wakaendelea kufanya wanachokitaka.

“Wakati mwingine kubadilisha watendaji kunahitaji uwe na akiba ya kutosha, kama kuna watu wanapwaya, nalo linaweza kumfanya asichukue hatua akawa anatumia kauli kama tishio,” amesema Makame.

Related Posts