Hakimu akwamisha kesi ya ‘Bwana harusi’ anayetuhumiwa kuiba gari

Dar es Salaam. Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, imepanga Aprili 14, kusikiliza hoja za awali (PH) katika kesi ya mfanyabiashara Vicent Masawe (36)’ ‘Bwana harusi’, baada ya upelelezi wake kukamilika.

Kesi hiyo ilipangwa leo Jumatatu Machi 24, 2025 kwa ajili ya Serikali kumsomea hoja za awali, lakini Hakimu anayeisikiliza, Beda Nyaki hayupo.

Wakili wa Serikali, Eva Kassa ametoa taarifa hiyo,  mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Geofrey Mhini.

“Mheshimiwa hakimu, kesi hii imeitwa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa hoja za awali, lakini hakimu anayesikiliza kesi hii hayupo, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea maelezo ya hayo,”amesema Kassa.

Hakimu Mhini, alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hiyo hadi Aprili 14, 2025 kwa ajili ya kusomewa ‘PH’ na mshtakiwa yupo nje kwa dhamana.

Kwa mara ya kwanza Masawe alipandishwa mahakamani Desemba 24, 2024 na kusomewa mashitaka yanayomkabili.

Anadaiwa kutenda makosa hayo Novemba 15, 2025 kinyume na  vifungu  namba 258 na 273(b) vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Katika shitaka la kwanza la wizi wa kuaminika, Masawe anadaiwa kuwa akiwa wakala, tarehe hiyo  Novemba 15, 2024 katika Jiji la Dar es Salaam, aliiba gari aina ya Toyota Ractis.

Gari hilo  lenye thamani ya Sh15 milioni, kwa mujibu wa upande wa mashitaka ni mali ya Silvester Masawe.

Anadaiwa kuwa aliazimwa gari hilo na  Silvester kwa lengo la kulitumia katika sherehe ya harusi yake, lakini baada ya hapo, hakulirudisha kama walivyokubaliana.

Katika shitaka la pili la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, anadaiwa kuwa tarehe hiyohiyo jijini Dar es Salaam, kwa lengo la kuiba na kutapeli, alijipatia fedha taslimu Sh3 milioni kutoka kwa Silvester, akiahidi kumrudishia baadaye ilihali akijua ni uongo na hakuzirudisha hadi alipokamatwa.

Kabla ya kukamatwa na kisha kufikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka hayo, Masawe mkazi wa Ungindoni, Kigamboni jijini Dar es salaam alidaiwa kupotea.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, Novemba 18, 2024 Masawe ambaye alikuwa fungate baada ya kufunga ndoa, alitoa taarifa kwa marafiki zake kuwa yupo Mbezi lakini anafuatiliwa na gari asilolijua.

Tangu siku hiyo, hakuonekana wala kupatikana kwenye simu zake.

Hata hivyo, Desemba 17, 2024 Kamanda wa Polisi Kanda ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro alitoa taarifa za kukamatwa kwake.

Kamanda Muliro alisema kuwa Masawe alikamatwa Desemba 15, 2024, akiwa kwa mganga wa kienyeji, Pemba  na alikuwa na tuhuma za wizi wa kuaminiwa na kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu.

Alieleza kuwa kutoka na tuhuma hizo ndio maana alitengeneza mazingira ya uongo kwamba amepotea kisha akaenda kujificha kwa mganga  huyo wa kienyeji.

Hata hivyo, alipopandishwa kizimbani na kusomewa mashitaka hayo alikana na aliachiwa kwa dhamana.

Related Posts