Dar es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha miaka 30 tangu kufanyika kwa mkutano wa Beijing mwaka 1995, mitazamo potofu, uwepo wa mila na sheria kandamizi, ukatili wa kijinsia, mimba za utotoni, zinatajwa kama baadhi ya sababu zinazokwamisha kufikia usawa wa kijinsia hasa katika upande wa elimu.
Mwaka 1995, viongozi wa dunia walikusanyika jijini Beijing, China, kwenye mkutano wa nne wa Umoja wa Mataifa kuhusu wanawake.
Mkutano huo uliandika historia kwa kupitisha Azimio la Beijing na mpango wa utekelezaji, nyaraka muhimu zilizoahidi kusukuma mbele usawa wa kijinsia.
Akizungumza katika mkutano uliowakusanya wanawake vijana viongozi kujadili kuhusu miaka 30 baada ya mkutano wa Beijing kwa kuangazia haki ya elimu uliofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Msichana Initiative, Rebeca Gyumi alisema haki ya elimu imewekwa wazi katika katiba ya Tanzania, ambayo inasema kwamba kila mtu ana haki ya kupata elimu.
Pia alisema Serikali imetunga Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, iliyorekebishwa mwaka 2023 pamoja na kuanzisha mpango wa elimu bila malipo kwa lengo la kuhakikisha watoto wote wanapata elimu ya msingi na sekondari na kukamilisha mzunguko wa elimu.
Hata hivyo, anasema takwimu zinaonyesha kuwa ni asilimia tano hadi sita pekee ya wasichana wanaoendelea na elimu ya sekondari ikilinganishwa na asilimia 12,hadi 13 ya wavulana.
Anaongeza kuwa chini ya theluthi moja ya wasichana wanaomaliza elimu ya msingi, hawafanikiwi kumaliza elimu ya sekondari kutokana na kukumbana na vikwazo mbalimbali ikiwemo vikiwamo mimba na ndoa za utotoni.
“Msichana mmoja kati ya wanne tayari ni mama kabla ya kufikisha miaka 18, na msichana mmoja kati ya watatu anaolewa kabla ya kutimiza miaka 18. Wasichana kuacha shule, kupata mimba, na ndoa za utotoni vina uhusiano wa moja kwa moja. Pindi msichana anapopata mimba, ni vigumu sana kwake kuendelea na masomo na mara nyingi huishia kuolewa akiwa bado mdogo, ”anasema.
Anasema pamoja na changamoto ya ndoa na mimba za utotoni pia baadhi ya wazazi hasa maeneo ya vijijini bado hawatoi kipaumbele kwenye elimu ya wasichana, wakiamini ni upotevu wa rasilimali kwa sababu wasichana wataolewa na kwenda kwenye familia nyingine .
“Hili pia linarudisha nyuma jitihada za kumwezesha mtoto wa kike kupata elimu na kufikia usawa wa kijinsia, “anaeleza.
Kwa upande wake, Hellen Sisya anasema suala la wasichana waliopata ujauzito kurejea shuleni bado ni gumu, licha ya hatua za Serikali kutoa miongozo ya kuruhusu kurejea shule.
Anasema unyanyapaa na ubaguzi kwa mabinti walio na watoto wanaporudi shule, bado unakwamisha elimu kwa wasichana, kwani jamii ina mtazamo hasi kuhusu wasichana waliopata mimba wakiwa shule.
Anasisitiza kuwa ili kukabiliana na changamoto hizo kuna umuhimu wa kushughulikia changamoto kwa pamoja kupitia mfumo wa kisheria unaolinda haki ya elimu, kupambana na ndoa za utotoni na kudhibiti mimba za utotoni kwa wakati mmoja.