Moto wa nyika waua wanne Korea Kusini, chanzo chatajwa

Seoul. Korea Kusini imekumbwa na janga la moto wa nyika unaoteketeza maeneo ya misitu na makazi kusini mashariki mwa nchi hiyo.

Moto huo umeenea maeneo 24 tofauti, huku maelfu ya watu wakihamishwa ili kuepuka madhara ya kiafya.

Shirika la Habari la Yonhap, limeripoti leo Jumatatu Machi 24,2025, kuwa moto huo umeibuka maeneo 24 tofauti nchini humo, huku maelfu ya watu wakilazimika kuhamishwa kutoka kwenye makazi yao ili kuepuka madhara ya kiafya.

Taarifa zimeeleza kuwa juhudi za kuuzima moto huo zimehusisha wafanyakazi wa zima moto 9,000, polisi na helikopta 120, lakini juhudi za kudhibiti moto ziligonga mwamba kutokana na hali ya hewa kavu na upepo mkali.

Kwa mujibu wa taarifa moto huo ulianza Ijumaa katika mji wa Sancheong, Mkoa wa South Gyeongsang, na inadaiwa chanzo kilikuwa cheche kutoka kwenye mashine ya kukata nyasi.

Taarifa nyingine zilieleza kuwa katika jitihada za kuudhibiti moto huo wafanyakazi wanne wa uokoaji walipoteza maisha.

Taarifa zimeeleza kuwa moto huo umeathiri zaidi ya hekta 1,464 na kuwaathiri zaidi ya watu 2,740 ambao wamehamishwa kutoka kwenye makazi yao.

Takriban majengo 162, likiwamo hekalu moja huko Euiseong, yameharibiwa vibaya na moto huo.

Kaimu Waziri Mkuu, Choi Sang-mok ameagiza idara ya misitu kufanya kila linalowezekana kuwaondoa wakazi na kuhakikisha usalama wa wafanyakazi wanaopambana na moto huo unakuwa wa uhakika.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.

Related Posts