Mtoto wa Museven adai wanajeshi wa Uganda wataingia DRC wakati wowote

Kampala. Mkuu wa Majeshi nchini Uganda, Muhoozi Kainerugaba, amesema askari wa Jeshi la Uganda (UPDF) ama wapiganaji wa Kundi la M23 watawasili katika mji wa Kisangani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) chini ya wiki moja ijayo.

Katika chapisho lake la jana Jumapili, Kainerugaba amesema wanajeshi wake ama M23 watawasili Kisangani kwa agizo la Rais Yoweri Museveni ambaye ni baba yake, ili kuwaokoa wakaazi wa Kisangani dhidi ya matendo yanayofanywa na makundi mengine ya waasi nchini DRC.

Wanajeshi wa Uganda wapo nchini DRC, kwa ushirikiano na Jeshi la FARDC, kupambana na makundi mengine ya waasi likiwemo lile la CODECO.

Si mara ya Kwanza kwa mkuu huyo wa majeshi nchini humo kutoa kauli za kutatanisha kwa kutumia akaunti ya mtandao wake wa X.

Licha ya wapiganaji wa M23 kuwasili katika miji kadhaa ya mashariki mwa DRC, hawajaonesha nia ya kutaka kudhibiti jiji la kimkakati la Kisangani.

M23 awali ilidai kuwa inapanga kujiondoa katika mji wa Walikale ili kutoa nafasi ya mazungumzo na serikali ya Rais Felix Tshisekedi. Hata hivyo, bado hakuna dalili za kuanza kujiondoa katika mji huo.

M23, kundi la waasi wa DRC linalodaiwa kuungwa mkono na Rwanda , limechukua udhibiti wa maeneo makubwa mashariki mwa Congo katika miezi ya hivi karibuni ikiwemo Mji wa Goma, Bukavu na Walikale. Hata hivyo Rais wa Rwanda Paul Kagame amekuwa akikanusha mara kadhaa kuliunga mkono kundi hilo.

Hata hivyo, halijatoa ishara zozote za mipango ya kusonga mbele hadi Kisangani, jiji la kimkakati lililopo katikati mwa DRC.

Kainerugaba anajulikana kwa matamshi yake ya kichochezi na yasiyochujwa kwenye mtandao wa X, ambayo mara nyingine yamezua matatizo ya kidiplomasia.

Uganda ina nafasi tata katika mgogoro wa muda mrefu mashariki mwa DRC.

Ingawa inashirikiana na Serikali ya DRC kupambana na makundi tofauti ya waasi, pia ina uhusiano wa karibu na Rwanda na  Kainerugaba alikutana na Kagame Alhamisi iliyopita.

“Watu wetu wa Kisangani, tunakuja kuwaokoa. Jeshi la Mungu linakuja!” Kainerugaba aliandika kwenye X.

Aliongeza: “Ndani ya wiki moja, aidha M23 au UPDF (Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda) litakuwa Kisangani. Kwa amri ya Yoweri Museveni, Amiri Jeshi Mkuu wa UPDF!”

Kuchukuliwa kwa Kisangani na M23 kungesababisha kuongezeka kwa mgogoro, kwani kunaweza kuliingiza kundi hilo ndani zaidi ya ardhi ya DRC.

Kisangani ni kitovu cha biashara na kituo muhimu cha usafiri kilichopo kwenye makutano ya mito mitatu kuelekea Kinshasa, mji mkuu wa DRC.

Hili pia lingekuwa lengo kubwa kwa Uganda, ambayo imekuwa ikiendesha operesheni zake katika jimbo la Ituri mashariki mwa DRC. Mji mkuu wa Ituri, Bunia, umbali wa takriban kilomita 700 kutoka Kisangani.

M23 hapo awali liliwahi kutishia kuendelea na mashambulizi hadi Kinshasa na kuiangusha serikali ya Rais, Félix Tshisekedi.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.

Related Posts